Monday, July 16, 2012

MAHAKAMA INAPOTUMIWA HOJA ZINAPOSHINDWA KUJIBIWA

Na. M. M. MwanakijijiWanaposhindwa hoja wao huleta vioja; wanaposhindwa hoja wao huleta kejeli; wanaposhindwa hoja wao hutumia nguvu; na wanaposhindwa hoja wao hukimbilia mahakamani. Baada ya mbinu zote za kukwepa hoja kushindikana watawala dhaifu huamua kutumia mahakama katika kuzuia wao kuhojiwa, kukwepa kuwajibishwa au kuahirisha kuchukuliwa hatua na wananchi. Kwa watawala wa aina hii mahakama huwa kichaka cha kufichia maovu yao! Ndugu zangu, mahakama zinapoanza kuingizwa katika malumbano ya kisiasa na zenyewe zinapokubali kutumiwa kisiasa kuficha aibu ya watawala maana yake utawala ulioko madarakani siyo tu umekalia kuti kavu, bali mnazi wenyewe ndani umeshaliwa na wadudu na kubakia mtupu.


Kwa wale wanafunzi wa historia ya siasa kama mimi wanaweza kwa haraka kabisa kuona kwa mifano dhahiri hiki nilichokisema hapo juu. Baada ya Nelson Mandela na kundi lake kuanza kudai haki za watu weusi na hasa haki ya kuwa na nafasi ya kutawala nchi yao wakiwa haki na wananchi wengine watawala wa zama zao waliona kuwa hoja zao haziwezi kujibiwa kiakili. Watawala wa wakati huo walishindwa kutoa majibu kufuatia kuandikwa kwa Azimio la Uhuru la Kongresi ya Wananchi. Azimio lile kimsingi liliwakilisha na kuwasilisha matamanio ya watu weusi na wengine wasio weupe wa Afrika ya Kusini. Serikali ya Makaburu haikuwa na majibu; ikaamua kuanza kamatakamata na matokeo yake kama wengi tunavyofahamu ni kesi ile ya kina Mandela ambayo hatima yake ni kifungo cha maisha kwa kina Mandela, Walter Sisulu na wenzake.


Huko Marekani nako ilikuwa hivyo hivyo wakati wa mwamko wa kudai haki za kiraia. Wakati kina Mandela kesi yao inaendela Martin Luther King alijikuta akiwekwa kizuizini baada ya kuingia kwenye hoteli ambayo ilikuwa haitoi huduma kwa weusi na kukaa kusubiri kuletewa chakula na kugoma kuondoka. Alishtakiwa na kuhukumiwa miezi minne jela. Aliachiliwa baada ya Kennedy Brothers kuingilia kati. Hakubadilisha hoja bali hoja zake ziliendelea! Mwaka 1963 akipuuzia agizo la polisi lililomkataza kuandamana alikamatwa tena (kabla ya hapo alishakamatwa mara kadhaa). Alikaa lockup kwa siku kumi na moja na ni wakati huu alipoandika Barua kutoka Jela ya Birmingham - barua ambayo kwa kiasi kikubwa imenijenga mimi mno kifikra za kukataa uovu wa watawala.


Hata katika Tanzania kipindi hicho hicho harakati za kudai uhuru zilikuwa zimekolea. Na kama kawaida watawala wa zama hizo nao hawakusita kutumia mahakama kujaribu kuzima sauti za wale wanaopigania uhuru au wenye kutoa hoja hoja za moto. Nani atasahau kesi ya kina Makange na Kheri Rashid (waandishi wa gazeti la "Mwafrika" ) ambao baada ya kutoa hoja zenye maneno makali walijikuta wakiwekwa ndani kwa miezi sita? au nani anaweza kusahau kuwa Nyerere naye alikosaakosa kwenda jela baada ya kukutwa na hatia ya uchochezi na akakubali kulipa faini ili kuweza kushiriki uchaguzi wa 1958?


Naweza kutoa mifano ya Misri, Algeria, Sudan, Urusi na hata China ambapo watawala wanapokosa hoja za kujibu au uwezo wa kujenga hoja za kiakili hutumia mahakama kuficha udhaifu wao. Na kwa bahati mbaya sana kwenye baadhi ya nchi za namna hiyo mahakama zimejiingiza katika mdumange wa wanasiasa na hivyo kujikuta vikiwa ni vikaragozi wa watawala.


Leo hii naweza kusema pasi ya shaka kuwa kuna uamuzi wa makusudi kabisa ambao umefanywa ambapo mahakama za Tanzania zianze kutumika kuzuia hoja zisizopendwa na watawala. Siyo tu kuzuia hoja zenyewe kwa kusema "jambo hili liko mahakamani" lakini sasa kuwafikisha mahakamani watoa hoja hao ili hatimaye wakae kimya. Kwenye hoja ya madaktari serikali imeshindwa na sasa imeanza kamatakamata ya madaktari kuwafikisha mahakamani - japo sababu haitolewi ya kushindwa hoja bali ya kukataa kusitisha mgomo! Tumeshaona hili pia kwa waandishi - kuna kesi inaendelea yenye kuhusisha wahariri - ambapo waandishi kadhaa wanatuhumiwa kufanya uchochezi na hivyo wao wenyewe kushtakiwa. Hata kwa wanasiasa tumeanza kuona mahakama zikitumiwa kama kichaka cha kukwepesha hoja zisizojibika.


Kinachosikitisha na labda hata kuudhi ni kuwa mahakama zimeanza kukubali kuwa hivyo. Tunavyozidi kwenda ni rahisi kuona kuwa mahakama zetu zisipoangalia zitajisokota kwenye nyuzi chafu za siasa na kujikuta siyo tu zinapoteza uhuru wake lakini pia umaana wake. Tuliona kwa upande wa jeshi lilivyojiingiza na kutukera wengine na sasa taratibu tunaanza kuona mahakama nazo zinaanza kujiachilia mikononi mwa wanasiasa. Mahakama hazipiganii uhuru wake! Hakuna watetezi wa uhuru wa mahakama; na inawezekana hawapo kwa sababu wadau wa mahakama hawaoni tishio hili kuu ambalo linatanda juu ya mahakama kama wingu zito jeusi.


Huku tunakokwenda mahakama zetu zinaweza kujikuta zinashindwa tena kutoa hukumu au kusimamia haki na badala yake badala ya kuweka kitambaa machoni mahakama zitakuwa zinachungulia kwa jicho moja kuona nani anasimama upande wa pili wa upanga wa haki.


Na kinachoudhi ni kuwa wanaharakati wetu bado hawajaamu kuzilazimisha mahakama kuamka. Njia kubwa - ambayo imefanikiwa sana sehemu nyingine - ni kwa wanaharakati kulazimisha kwenda mahakamani na kusababisha overwhelming ya kesi za kisiasa. Kwa mfano, haki ya kuandamana ni haki ya msingi lakini kama polisi wanaamua kuzuia haki hiyo kiholela wananchi wanayo haki ya kupuuzia agizo hilo (kama alivyofanya MLK na wenzake au Nyerere na wenzake) na hatima yake ni kuwa wengi wanakamatwa siyo kwa kufanya vurugu au kusababisha madhara bali kwa kuandamana. Hili likiendelea polisi lazima wafikirie kama wana mahabusu za kutosha na mahakama kuona kama zina mahakimu au majaji wa kutosha na magereza kufikiria kuona kama ina uwezo wa kufunga watu wote watakaokuwa wanaandamana bila kibali.


Na sisi wananchi tuanze kuwa waangalifu. Tusikubali wanasiasa watumie mahakama kama kichaka chao cha kufichia maovu. Tuwe makini kugundua wakati ambapo mahakama inaingizwa kwenye malumbano ya kisiasa na kuanza kukataa hili. Tusikubali mahali pekee ambapo haki inatakiwa kutafutwa pawe sehemu ambapo haki inachezewa. Lakini ni jukumu la majaji na mahakimu kuamua kama wanataka kuwa wapiga zumari wa wanasiasa. Ni wao watakaomua mahakama zinakuwa huru kwa kiasi gani. Je watakuwepo mahakimu na majaji mashujaa kutetea uhuru wa mahakama?


Historia itaamua.

No comments: