Thursday, July 26, 2012

KAMA WANGEKUWA NA VICHWA VYA KUFIKIRI TUSINGEFIKIA HAPA.Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,

SIPENDI kudhaniwa ni mjinga; sipendi zaidi kuchukuliwa kuwa ni mjinga; na kwa hakika sipendi kufanywa mjinga.


Yote matatu kwangu hayakubaliki na mtu yeyote mwenye kuweza kutumia ubongo wake vizuri hapaswi kukubali lolote kati ya hayo matatu.
Lakini zaidi kama sehemu ya jamii ya Watanzania naweza kusema hatupaswi kudhaniwa wajinga, kuchukuliwa wajinga au kufanywa wajinga. Yaani, kudhaniwa hatujui, kuchukuliwa hatujui, na kutendewa kama hatujui.


Tukikubali yote matatu au mojawapo ya hayo basi yote yanayotupata au yanayofanywa na watawala wetu ni yale tunayostahiki.


Kudhaniwa mjinga ni pale mtu anapoonyesha kukuheshimu, kukujali lakini anakufanyia hivyo huku mawazoni mwake anakufikiria kuwa wewe ni mjinga. Huyu anaweza kusema lolote au kufanya lolote akiamini kabisa kuwa wewe hujui au huna uwezo wa kujua.


Sasa huyu atakufanyia mambo - yanaweza kuwa mazuri - lakini kwa msingi kwamba anakutendea hisani. Na wewe unaposhukuru hata kwa “kidogo” alichokupatia wakati unachostahiki ni kikubwa huyu anakuwa amethibitisha kuwa wewe hujui kwamba unachostahili ni kikubwa zaidi ndiyo maana umefurahia kidogo.
Mtu anayekuchukulia kuwa wewe ni mjinga atafanya mambo akiamini kabisa kuwa wewe hujui anachofanya - kama ni kizuri au kibaya. Yule anayekudhania anaweza kukuonyesha heshima na staha wakati anazungumza nawe huyu mwingine yeye hajali kama anaonyesha heshima au staha. Huyu anafanya mambo huku akijua fika kabisa wewe huwezi kujua! Atakufanyia lolote na kwa kadiri wewe huwezi kumhoji basi ataendelea kufanya bila hofu ya lolote.

Hata hivyo, mtu anayekufanya mjinga yeye anaamini kabisa kuwa anachokufanyia wewe ni manufaa yako kwa sababu wewe huwezi kukifanya kwa sababu hata hujui kama unapaswa kukifanya. Kama umewahi kusikia mtu anasema “usinifanye mjinga bwana” kimsingi hataki kutendewa kama mtu asiyejua lolote.


Siyo tu kwamba afanywe kama mtu asiyeweza kujua bali asiyejua kabisa. Mfano mzuri ni kiongozi anapokuja na wazo la mradi mashuhuri ambao katika kichwa chake anaamini kuwa wewe mwananchi unauhitaji.
Haitaji kukuuliza, haitaji kujua kama unahitaji huo mradi bali yeye katika kichwa chake cha “kufikiri” anaamua kuwa wewe mwananchi unahitaji na hivyo anakuletea. Si kwa sababu anajua unajua unachohitaji; la hasha! bali anaamini hujui unachohitaji na ni yeye mteule anayejua unachohitaji. Na hivyo anaamua kukufanyia. Sasa anapokifanya vibaya au kuboronga na wewe unakubali hapo anakuwa amekufanya wewe mjinga!

Siku chache zilizopita Mwanasheria Mkuu wa Serikali Frederick Werema akijibizana na Tundu Lissu bungeni alisema kitu ambacho kimenifanya nihoji kama Werema na serikali anayowakilisha wanatudhania ni wajinga, wanatuchukulia wajinga au ndio wanatufanya taifa zima ni wajinga isipokuwa wao peke yao.
Mtu ambaye anaweza kuzungumza kama alivyozungumza Werema ni yule tu ambaye anaamini kabisa kuwa yeye pekee (ama na wenzake) ndio wanaju wanastahili kuvizungumzia. Werema alichodai kimsingi ni kuwa yeye anajua kuliko Lissu na Lissu haiwezekani kuwa anajua.

Kwa wanaokumbuka Werema alifanya hili hili (na kwa hoja ya Lissu) wiki kama mbili zilizopita pale alipoamua kumbeza Profesa Isasa Shivji kwa vile ati si msomi wa Katiba. Hiki tunachoshuhudia kwa Werema (labda hata kwa Lissu) ni kile ambacho tunachokiita kujitukuza kwa wasomi (elitisim).
Yaani, ndugu zetu hawa wanataka tuamini kwa vile wao “wamesoma” basi wanaweza kutuambia lolote bila kuhojiwa na watu wengine. Kwamba kwa vile Werema ni Mwanasheria Mkuu basi majibu yake ni sahihi kwa mambo yote na wakati wote. Hiki ni kiburi kinachostahili kukemewa.

Ndugu zangu, msomi mzuri si yule anayejitapa kuwa amemaliza shahada x, y na z. Msomi wa namna hiyo anaweza kabisa kujiita ni “mhitimu mzuri” lakini si msomi mzuri.
Msomi mzuri ni yule ambaye ana unyenyekevu wa kusema “nataka kujua zaidi”. Msomi anayeamini anajua tu ataamua kubisha hasa kama anayemuambia si “msomi” kama yeye.
Lakini msomi wa kweli kabla ya kujibu atasikiliza na kupima anachoambiwa na kama ni kitu ambacho anaweza kujifunza zaidi atakubali kuwa jambo hilo alikuwa halifahamu au angependa kupata maelezo zaidi.


Kusema hivyo hakumaanishi si msomi, bali kunamaanisha kuwa anataka kutoa maoni ambayo yamepatiwa taarifa sahihi (well informed opinion). Ukisikia msomi anakurupuka kujibu bila kutafakari si hoja kwamba ana nini kwenye jina lake (BA, BS, MA, MD au Phd) huyu ni mhitimu. Msomi hata mara moja hakurupuki kujibu na anapotoa jibu la swali au hoja hawezi kutoa na kejeli, hayo ni mambo ya wanasiasa.
Sasa tunapomuona Mwanasheria Mkuu anapozungumza bungeni kama mwanasiasa inabidi tuhoji hicho kichwa anachodai ni cha kufikiri kama kinafikiri vizuri. Kwa sababu, kufikiri peke yake hakutoshi kwa sababu kuna vichwa vingine vikikaa vinafikiri maboga na mayai angani.


Ndiyo maana nikajikuta nasema moyoni kuwa kama kweli ndugu zetu hawa (wa serikalini au watawala kwa ujumla) wangekuwa na vichwa vizuri vya kufikiri kwa hakika tusingekuwa hapa. Wanavyo vichwa vizuri tu vya kufikiria lakini sidhani kama wana vichwa vya kufikiria mazuri.
Jamani, kweli kama wangekuwa na vichwa vizuri vya kufikiria tungekuwa bado na tatizo la umeme? Kama kweli wana vichwa vizuri kweli wanaamini tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam ni kukosekana kwa barabara za juu kwa juu?


Kama kweli wana vichwa vizuri vya kufikiria wangefikiria kuanzisha Shule za Kata nyingi lakini zikiwa na ubora wenye shaka? Kama kweli wana vichwa vizuri vya kufikiria kweli kabisa wangeamua kuwafutia usajili madaktari wanaogoma ili kuwakomoa na hivyo kuwafanya washindwe kuja kufanya tiba nchini na hivyo wao wenyewe kuleta yale yale ambayo yameletwa na mgomo?
Kama kweli wangekuwa na vichwa vizuri vya kufikiria kweli kabisa Tanzania ingekuwa na tatizo la chakula? Kama kweli wana vichwa vizuri vya kufikiria inawezekana vipi ajali nyingine ya majini inatokea karibu katika mazingira yale yale kama ajali nyingine iliyotokea mwaka 1996?

Hivi kweli kabisa leo ikitokea ajali ya treni - Mungu aepushie mbali - kwa mazingira yale yale ya Bahi kuna watu watasema kuwa ni “mapenzi ya Mungu”? Kweli hawa wana vichwa vinavyofikiria mambo mazuri?
Naomba kupendekeza kwako msomaji kuwa ndugu zetu hawa walioko madarakani wanavyo vichwa, vinafikiria madudu.


 
 
RAIA MWEMA

No comments: