Saturday, June 16, 2012

WABUNGE CCM WAIPINGA BAJETI
MMOJA AJITOLEA KUFUKUZWA, WATAKA IUNDWE TUME KUICHUNGUZA HAZINANeville Meena na Mussa Juma, Dodoma


KAMATI ya wabunge wa CCM jana ilikutana kwa zaidi ya saa tano katika kikao ambacho wabunge hao waliibua hoja ya kutaka kuchunguzwa kwa Mfuko Mkuu wa Serikali kwa maelezo kwamba kuna dalili za kuwapo kwa ufisadi.Habari kutoka ndani ya mkutano huo ulioongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda zilisema msingi wa hoja hiyo iliyotolewa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka ni kutokuwapo kwa uwiano kati ya fedha zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) pia kutoka kwa wahisani, na zile zilizopelekwa katika wizara na Idara za Serikali.


Katika hoja hiyo ambayo iliripotiwa kwamba iliungwa mkono na wabunge wengine kadhaa, Ole Sendeka alipendekeza iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mfuko huo au iteuliwe Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Hesabu kufanya ukaguzi.


“Tumeshindwa kuelewa inakuwaje TRA inakusanya mapato asilimia 106, yaani zaidi ya asilimia 100, wahisani tunaambiwa wametoa fedha asilimia 80,halafu eti fedha za maendeleo zilizopelekekwa wizarani ni asilimia 22 tu, haiwezekani na hapa tunataka uchunguzi ufanyike,”alisema mmoja wa wabunge wa CCM.


Mbunge mwingijne alisema wamebaini kwamba taarifa ya Waziri wa Fedha kuhusu fedha zilizotolewa kwa mujibu wa bajeti ya 2011/2012 zinatofautina na uhalisia katika wizara ya idara za Serikali na kwamba hiyo ni dalili kwamba hizo ni dalili ya kuwapo kwa matundu kwenye hazina hiyo ya nchi yanayopaswa kuzibwa.


“Tumesema haiwezekani, tunahitaji kutekeleza Ilaani ya CCM na ahadi ambazo sisi wabunge, Rais na chama tulizitoa kwa wananchi, sasa kama tunapitisha bajeti, fedha zinakusanywa, lakini hazifiki kwa wananchi ndiyo tunafanya kazi gani? Hili tunasema haliwezekani,”alisema mbunge mwingine baada ya kikao hicho jana jioni.


Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho kilichoanza saa 5.30 asubuhi katika Ukumbi wa Pius Msekwa na kumalizika saa 11.30 jioni ziliwataja baadhi ya wabunge waliounga hoja mkono hoja hiyo kuwa ni Alphaxard Lugora (Mwibara), Godfrey Zambi (Mbozi Magharibi) na Livingstone Lusinde (Mtera).


Bajeti 2012/2013


Kuhusu Bajeti ya 2012/2013, wabunge hao wa chama tawala wanaelezwa kwamba waliigeukia Serikali wakieleza kutoridhishwa na bajeti iliyowasilishwa bungeni juzi jioni na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.


Miongoni mwa malalamiko makubwa ya wabunge ni hao ni kutozingatiwa kwa vipaumbele vya Taifa pia Mpango wa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011 - 2016 ambao ulipitishwa na Bunge mwaka jana.


“Wewe bwana wewe, sijui nikwambie nini, lakini wabunge tumesema tumechoka, maana hakuna mabadiliko kwenye bajeti, tunayaona mambo mengi kuwa ni danganya toto tu, tumejadili, lakini sijui kama kipo cha kubadilika,”alisema mmoja wa wabunge waliohudhuria kikao hicho.


Habari zaidi zilidokeza kuwa Waziri Mkuu Pinda alilazimika kutoa nafasi kwa kila mbunge aliyeomba nafasi ya kuzungumza ili kupunguza hasira ambazo zingeweza kujitokeza kwenye mjadala wa jumla keshokutwa.


“Ndiyo maana tumechukua masaa, Pinda ameamua kuwapa watu wote nafasi ili wazungumze, ila mimi nimetoka wala sikuchangia kitu nasubiri huko ndani Jumatatu au Jumanne nikipata nafasi,”alisema Mbunge mwingine.


Mbunge wa Viti Maalum, Sara Msafiri aliripotiwa akipinga ushuru kwenye muda wa maongezi ya simu na kutaka Serikali kuhakiki kwanza mapato ya kampuni za simu.


Kadhalika mbunge huyo alinukuliwa ndani ya kikao hicho akisema bajeti hiyo imejaa maslahi ya wakubwa tu, na kwamba lazima yafanywe marekebisho ambayo yataifanya ishuke chini kwa wananchi.


Mwingine ni Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba ambaye alinukuliwa akiishauri Serikali iwe wazi kuhusu msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vya gesi kwani mwanya huo unaweza kutumiwa vibaya kukwepa kodi.


Kadhalika Makamba alinukuliwa akitaka kubadilishwa kwa taratibu za kutoza kodi kampuni za mafuta kwa kuweka utaratibu wa kodi kulipwa baada ya biadhaa hiyo kuingizwa nchini badala ya siku 45 za sasa.


“Kwanini tuwape hawa wafanyabiashara mitaji kwasababu utaratibu wa sasa wanaingiza mafuta hata kama hawana senti tano, na sisi tunakubali kuahirisha kuchukua kodi hadi baada ya siku 15 na baadaye siku 30. Hili ni tatizo na tuangalie eneo hili vizuri,”chanzo chetu kilimnukuu Makamba akisema katika kikao hicho.


Kutokana na hoja za wabunge hao, Kikao hicho kiliazimia kuundwa kwa kamati ndogo ya wabunge wa CCM kuangalia jinsi ya kupanua wingo wa kukusanya mapato pia kupendekeza mgawanyo wa mapato hayo tofauti na Bajeti ya Serikali.


Baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi aliwaongoza wajumbe wa kamati yake kwenda kukutana tena na Waziri wa Fedha ili kuangaliwa kama wanaweza kufanya marekebisho ya bajeti hiyo kwa kuzingatia maoni ya wabunge wa CCM.


Mpina apinga hadharani


Wakati hayo yakiripotiwa kutokea ndani ya kikao cha wabunge wa CCM, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina jana alijitokeza mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma na kusema kwamba hataunga mkono bajeti hiyo na kwa maana hiyo “yupo tayari kufukuzwa” kutokana na uamuzi wake huo.


Licha ya kutangaza kutoiunga mkono bajeti hiyo, mbunge huyo alisema keshokutwa Jumatatu ataomba mwongozo kwa Spika kutoa hoja ya kuomba bajeti hiyo irejeshwe serikalini ili ifanyiwe marekebisho na kama Serikali ikiing’ang’ania ni bora Rais Jakaya Kikwete avunje Bunge na kurejewa uchaguzi.


Hata hivyo, alisema anaamini kwamba hatua ya kuvunja Bunge haiwezi kufikiwa ikiwa busara itatumika kumaliza mvutano uliopo.


Mpina alisema Bajeti ya Serikali inakiuka azimio la Bunge la kutengwa fedha walau asilimia 35 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.


Mbunge huyo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi alisema yapo makubaliano ya wabunge kwamba kila mwaka wa fedha, zitatengwa Sh2.7 trilioni kutoka fedha za ndani kugharamia miradi ya maendeleo ili kuwezesha fedha hizo kufikia walau asilimia 35 ya bajeti.


Alisema kwa mshangao bajeti iliyowasilishwa juzi iliweka kando mapendekezo na maazimio ya wabunge.


“Bajeti hii, tuliikataa katika kamati yetu, kwa kuwa inakiuka Azimio la Bunge na pia mpango wa serikali wa miaka mitano, na juzi iliposomwa niliomba Mwongozo wa Spika ili niitake Serikali irudishe bajeti hii na kurekebisha, lakini bila kufuata kanuni spika alinizuia kwa madai kuwa siku ya kusomwa bajeti hakuna mwongozo” alisema Mpina.


Mpina alisema, kanuni ya bunge ya 68 kifungu cha 7, inaeleza wazi kuwa mbunge, anaweza kusimamia wakati wowote anapoona hakuna mtu anayeongea.


“Naamini Spika hakunitendea haki na Jumatatu pia nitaomba mwongozo tusiendelee na mjadala wa bajeti hii na kama itaonekana kutetea fedha kupelekwa kwenye maendeleo ni kosa hasa wakati ni utekelezaji wa ilani ya CCM, nipo tayari kwa lolote,”alisisitiza.


Alisema kitendo cha Serikali kutenga Sh 2.2 trilioni badala ya Sh2.7 trilioni ambao ni upungufu wa Sh500 bilioni, kumesababisha miradi mingi kutengewa fedha kidogo na mingine kukosa fedha kabisa.

Alisema kibaya zaidi mapato ya ndani yameongezeka kwa kiasi cha Sh1.5 trilioni, lakini fedha hizo zimeliwa na matumizi ya kawaida ambayo yameongezeka kwa Sh1.9 trilioni, huku fedha za maendeleo zikipungua kwa Sh397.8 bilioni ikilinganishwa na mwaka 2011/12.


Mpina alisema kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiahidi kupunguza matumizi ya kawaida ili kuongeza kasi ya utoaji huduma na uwekezaji katika sekta zinazokuza uchumi na kupunguza umasikini, lakini hakuna kinachotekelezwa.


“Matumizi kama haya ya safari, posho,mafuta,ununuzi wa magari , samani, mawasiliano, sherehe,warsha ,makongamano,mafunzo,nje ya nchi yanaweza kuepukika,kupounguza au kuahirishwa”alisema Mpina.


Mbunge huyo alihoji inakuwaje serikali ilipata fedha za kufidia mabenki na wafanyabiashara walioathirika na mtikisiko wa uchumi Sh1.7 trilioni halafu ishindwe kupata Sh500 bilioni kugharamia miradi iliyoainishwa katika mpango wa maendeleo.MWANANCHI


No comments: