Thursday, June 21, 2012

TUJIHADHARI, UPORAJI ARDHI WAJA
  • Wayahudi walinyakua Palestina wakinukuu Kutoka 3:8  • Makaburu wamevamia Tanzania kwa kunukuu Torati 32:8


Na Joseph Mihangwa,

BILA shaka msomaji umepata kujiuliza swali hili: “Kwa nini Makaburu wanaipenda sana nchi yetu, hasa baada ya uhuru wa nchi hiyo mwaka 1994? Kulikoni? Chinua Achebe, katika kitabu chake “Things Fall Apart” anasema, “Chura [mkubwa – Toad] hakimbii ovyo mchana ila kama kuna kitu nyuma”.

Tumeshuhudia siku za karibuni kwa wawekezaji hao weupe, kuchangamkia uwekezaji katika sekta nyeti za biashara kama vile Viwanda vya Bia (TBL), mitandao ya maduka (Shoprite), umeme (NET Group Solution); madini (Meremeta, Tangold, Deep Green, Merelani); ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu (BOT); na sasa wanakuja kuwekeza katika kilimo kikubwa cha kuhodhi.

Tayari wamekwishanyakua ardhi kubwa huko Angola, Msumbiji, DRC na Ivory Coast; na hivi karibuni wametiliana sahihi na Serikali ya Kongo (Brazaville) kuchukua ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 220,000 kwa mkataba wa Kisetla wa miaka 30.

Hapa kwetu, wabaguzi hao wa rangi wanaingia taratibu kunyakua ardhi kwa programu mbalimbali tata, kama vile KILIMO KWANZA, Mapinduzi ya Kijani, Kilimo cha Mkataba ambamo wakulima wadogo wadogo watagawanwa na wenye mitaji mikubwa kuwalimia kwa njia ya kupewa mikopo (kulimiwa, mbegu, pembejeo, mifuko/zana za kuvunia mazao n.k.) isiyolipika, hatima ya yote ni kupokonywa ardhi kwa kushindwa kulipa. Mkulima hapangi bei ya vitu anavyokopeshwa, ila yule anayekopesha.

Tangu lini bepari (mwekezaji) akawa na huruma kwa mvuja jasho?. Wapi “Mapinduzi ya Kijani” yameleta neema kwa mtu mdogo duniani?

Programu zote hizi, zinatekelezwa kwa kushirikisha wazalendo lakini nyuma kuna hao wenye kuwania kupora ardhi ya wanyonge hao. Lengo ni kunyakua ardhi bila kuwashtua wananchi ili kuepuka vita vya “mau mau” nchini.

Amini usiamini, mipango yote hii inatekelezwa na mataifa makubwa kupitia Shirika la Chakula Duniani (FAO), Shirika la Biashara Duniani (WTO), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambapo Afrika Kusini inatumika kama kivuko cha kutufikia na kupora ardhi yetu.

Uvamizi huu wa nchi za Kaskazini mwa Afrika Kusini unaendelezwa na Makaburu hao chini ya mwavuli wa kuanzisha ukanda wa chakula (Food Corridor), eti kuzifanya nchi husika zishinde vita dhidi ya njaa inayozikumba.

Kama nilivyoeleza katika mfululizo wa makala zilizotangulia katika gazeti hili, kusambaa kwa Makaburu kuelekea Kaskazini baada ya uhuru wa nchi hiyo, kulitokana na marekebisho ya sera ya ardhi nchini humo, iliyoporwa kutoka kwa wazalendo na Makaburu hao, tokea karne ya 19, na kurejeshwa mikononi mwa wazalendo.

Kwa sababu hii, serikali mpya ya Afrika Kusini iliwashawishi na kuahidi kuwasaidia Makaburu hao kuondoka kwenda kutafuta makao mapya. Kwa sababu hii, tukio hili si kwamba ni ajali au bahati mbaya, bali limepangwa na lina mizizi katika historia.

Kihistoria, Makaburu na Wayahudi wanafanana sana kimaisha, imani na kitabia. Kwanza, wote ni wahamiaji katika nchi walizomo. Wakati Wayahudi walivamia Israeli (Palestina) wakitokea (utumwani) Misri, Makaburu walivamia Afrika Kusini (kama tutakavyoona baadaye) kutoka Ulaya; wote sera zao ni za kibaguzi (Apartheid) kutokana na imani ya dini yao ya Uyuda (Judaism).

Kwa Wayahudi na Makaburu, ardhi ni ya pili baada ya Mungu na kufuatiwa na Biblia. Kwa hiyo, tunapowakaribisha nchini, tufahamu kwamba tunakaribisha masetla wa kudumu; na kwamba, jaribio lolote baadaye la kutaka kuwaondoa, litakuja zua vita kama ile ya Palestina, kwa sababu katika nchi za Afrika hatuna akina Mandela au Farao mwenye nguvu kama yule wa Misri, aliyewatia adabu Wayahudi wakalazimika kutorokea Palestina.

Makaburu na Wayahudi wanafananaje kutufanya tuhofie kuzuka kwa Palestina ya Tanzania?. Angalia mfano huu.

Mwaka 1971, Mkuu wa Kanisa la “Dutch Reformed Church” (DRC) la Afrika Kusini, Dakta B. Vorster, alipata kuulizwa na kipindi cha Televisheni cha BBC, aeleze sababu na uhalali wa mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid) kidini; na kwa nini Makaburu wasiwarejeshee wazalendo ardhi yao waliyopora karne ya 19. Naye, haraka haraka, akajibu kueleza uhalali wa uporaji huo na ubaguzi kwa misingi ya rangi: “Torati, sura 32:8”

Sehemu hiyo ya Agano la Kale inasema: “Yeye aliye juu alipowapa Mataifa urithi wao, Alipowabagua wanadamu; Aliweka mipaka ya watu kwa kadri ya hesabu ya wana wa Israeli”.

Na katika kitabu cha maelezo kwa Vijana wa Makaburu wanaoandaliwa kupata Sakramenti ya Kipaimara, wanafundishwa kwamba, Ubaguzi kwa njia ya kuwatenga Wanadamu kwa misingi ya rangi (apartheid), ni mpango wa Mungu unaopaswa kutekelezwa na waumini wote wa Kanisa la Afrika Kusini (DRC); na kutofanya hivyo ni kupingana na mpango wa Mungu”.

Mpaka harakati za Wazalendo zilipowang’oa wakaiachia ardhi kwa wananchi mwaka 1994, Makaburu waliamini kwamba ardhi hiyo waligawiwa na Mungu kwa mujibu wa Torati 32:8, na ubaguzi wa rangi ulikuwa mpango maalumu wa Mungu.

Makaburu na Wayahudi wote ni Ma-“Hapiru”, kwa maana ya wazururaji na majambazi, kwa lugha ya Kibabeli. Wakati Makaburu walivamia Afrika Kusini kijambazi kutoka Ulaya kwa kunukuu Torati 32:8, Mayahudi walivamia Palestina kwa kunukuu kitabu cha Biblia cha “Kutoka”, 3:8: “Nami (Mungu wa Babu zenu – MIMI AMBAYE NIKO) nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka Misri hadi nchi njema, ijaayo maziwa na asali, kisha pana, asema BWANA”.

Kama ambavyo Afrika Kusini ilikuwa ikikaliwa na wenyeji wake kabla ya uvamizi, ndivyo hivyo Palestina nayo, iliyokuwa na eneo la kilometa za mraba 83,200, ilivyokuwa na wenyeji wa makabila ya Wakanaani, Wahati, Waamori, Waperezi, Wahivi na Wayebusi (Kutoka 3:15 – 17; Anat E: Palestine Before the Hebrews).

Chini ya imani ya dini yao ya Uyuda, wakiongozwa na Torati 32:8, Mayahudi na Makaburu ni wabaguzi wakubwa wa rangi kwa mwili, roho na damu; wao wanajiona kama “superior race”, kwa maana ya kabila la daraja la juu miongoni mwa binadamu. Kwao, waumini wa dini nyingine ni Wapagani, watumwa au wanyama wa kazi (beasts of burden), wasiostahili hata kulegeza gidamu za kiatu cha Yahudi au Kaburu.

Kwa mtizamo wao, kwa binadamu mwingine kudai haki kwa lugha ya amani, ni sawa na Punda wa Balaam kusema lugha kama mtu; na kudai haki kwa nguvu, ni sawa na nyani kufanya ugaidi katika Bustani ya Edeni.

Kwao, kwa mtu kupinga au kupiga vita ubabe na uonevu, ni sawa na kumchokoza kaka yao na kiranja mkuu (Marekani), anayewakilisha na kusimamia utamaduni na ustaarabu wa kibabe wa nchi za Magharibi – Utamaduni wa Agano la Kale; wa Mungu wa wazururaji, mwenye wivu, mpenda maangamizi na umwagaji damu.

Wababe wanajuana na kusaidiana kwa uwezo wa misuli yao: Wakati Ufaransa na Marekani zilikuwa za kwanza kuisaidia Israeli (Wayahudi) kujenga mtambo wa kwanza wa Nyuklia sehemu ya Damona nchini Israeli, ili kupambana na Wapalestina na nchi zote zilizokuwa zikiiunga mkono harakati zao za mapambano dhidi ya Israeli, Israeli nayo iliwasaidia Makaburu wa Afrika Kusini kujenga mtambo wa kwanza kama huo kwa sababu hizo hizo, lakini waliweza kung’olewa licha ya silaha zao kali.

Wayahudi na Makaburu, kila mmoja anaamini kuwapo kwa nchi ya ahadi, yenye asali na maziwa. Kwa Wayahudi, mpaka sasa ni Palestina; na kwa Makaburu, licha ya kung’olewa Afrika Kusini, bado wanaamini Afrika nzima ni yao, ila ni suala la muda tu.

Wakati Wayahudi wanaamini kwamba, ile safari yao kutoka utumwani Misri (walikojipeleka kutafuta maisha – Mwanzo 12:10 – 14) kwenda Kanaani (Palestina), kati ya mwaka 1,300 na 1,200 Kabla ya Kristo [KK], kuwa ndiyo iliyowafikisha kwenye nchi ya “Ahadi”, Makaburu kwa upande wao, bado wanaamini kwamba ile safari yenye shari, kutoka Cape Colony kuelekea Kaskazini hadi Majimbo ya Orange Free State na Transvaal, kati ya mwaka 1836 – 1837 Baada ya Kristo (BK), maarufu kama “The Great Trek” na kuyafanya majimbo hayo kuwa makoloni yao, kuwa ndio ulikuwa mwanzo tu kuelekea Kanaani yao ya Afrika, na kwamba Afrika Kusini kilikuwa kituo chao cha kwanza safarini.

Na kwa kuwa ngome yao ya kwanza imevunjwa baada ya Afrika Kusini kuwa huru (1994), “The Great Trek” inaendelea kuelekea Kaskazini, ambako tayari wamejinyakulia ardhi nchini Msumbiji, Angola, na sasa wanakaribishwa Tanzania kuhodhi ardhi kama “wawekezaji”, chini ya Programu ya “KILIMO KWANZA”, ambayo kama tulivyoeleza katika makala zilizotangulia, imebuniwa na Majenerali wa Jeshi la Makaburu wa Afrika Kusini lililovunjwa.

Kama ni historia kujirudia, basi, ndiyo tunavyokumbuka kwamba, mwaka 1931, nusu ya ardhi ya Rhodesia Kusini (Zimbabwe) ilitengewa “wawekezaji” wa Kizungu wasiodizi 2,500 ambapo pia wakati huo asilimia 87 ya ardhi ya Afrika Kusini ilitangazwa kumilikiwa na Wazungu. Kuna tofauti gani kati ya 1941 na kile kinachokusudiwa hapa kwetu leo, chini ya KILIMO KWANZA? Je, si kweli kwamba tunakaribisha vita ya “Palestina” au “Mau Mau” nyingine?.

Hizi si nyakati za Torati 32:8 – 15; ni nyakati ambazo ubaguzi unaendelea kutupwa mkono na historia kote duniani; lakini baya zaidi, ni hili la kuwa ni nyakati za injili ya mitaji ya kibaguzi kwa utamaduni ule ule wa Ki-Yuda, ambamo “aliye nacho ataongezewa; asiye nacho hata kile kidogo atanyang’anywa”; ili kwamba wenyeji (wazalendo) ndio watakaolima mashamba ya wageni kama manamba.

Leo, badala ya kutumia Biblia/itikadi ya dini kupora ardhi kama hapo zamani, injili ya sasa ni “ubinafsishaji na uwekezaji” katika ardhi, na msahafu (Biblia) kwa sasa ni “mtaji”, madhabahu ni Sera za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Tunafahamu fika, kwamba mitaji ya Makaburu, wakisaidiwa na nchi za ubepari na ukoloni-mamboleo za Ulaya Magharibi, Benki ya Dunia na IMF, ndiyo inayoelekea kutawala nyanja zote za maisha na biashara hapa nchini, kwa shari, lengo na nia mbaya kwa Watanzania.

Licha ya ardhi yetu kunyemelewa na masetla hawa, waliotimuliwa Afrika Kusini kwa sera zao za Uyuda na Ki-uzayuni, sasa wameturubuni kwa msahafu mpya, nasi tumeruhusu kila kitu kutoka Afrika Kusini – upendeleo katika uwekezaji sekta ya viwanda, mabenki, madini na huduma za jamii. Sakata hili lilianzia Serikali ya Awamu ya Tatu ya Benjamin William Mkapa, wakati ambao nia ya Makaburu kutafuta makao mapya ilikuwa dhahiri.

Tulifarijika wakati ule, pale aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa, alipobaini shinikizo kutoka nje la kutaka kurekebisha Sheria ya Ardhi ili kuruhusu Makaburu hawa wahodhi ardhi, aliposema: “Serikali (yangu) haitakubali shinikizo la kubadili Sheria ya Ardhi kwa lengo la kukidhi matakwa ya wachache, badala ya matakwa ya umma”.

Alitamka hayo katika moja ya hotuba zake za mwisho wa mwezi, baada ya kugundua kuwa WB, IMF na Umoja wa Ulaya (EU), kwa kushirikiana na Chama cha Maendeleo ya Kilimo cha Afrika Kusini (SACADA), walikuwa wakishinikiza Makaburu hao wapatiwe ardhi ya Kilimo nchini Tanzania kama “masetla?”.

Mpango mzima wa siri, unatokana na Serikali Afrika Kusini kuwalazimisha Makaburu waiuzie Serikali hiyo ardhi, ili nayo iweze kuwarejeshea Wazalendo. Kwa sababu hii, Serikali hii imefanikiwa kuzirubuni nchi jirani Tanzania ikiwamo, zikakubali kuwakaribisha Makaburu hao kama “msaada kutoka nje” wa kiwekezaji.

Lengo la Serikali ya Afrika Kusini ni kuona kwamba angalau kilometa milioni 25 za ardhi zinakombolewa kutoka kwa Makaburu na kupewa Wazalendo ifikapo mwaka 2014.

Lakini kilichoshangaza baadaye kidogo, ni Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), kutangaza kuwa kitashirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), kuitangaza ardhi yetu na kuiuza kwa wateja kutoka nje. Hawa TIC na UNIDO wao ni nani kujiamlia kuuza urithi wa Watanzania?

Imeelezwa kwamba, kwa Kaburu (na Yahudi), ardhi ni ya pili baada ya Mungu na Biblia. Kumkaribisha Kaburu au Yahudi katika ardhi yako ni sawa na kumruhusu Ngamia kuingiza kichwa kwenye hema: litapasuka vipande!.

Tumejionea jinsi Kaburu alivyotuhujumu katika nyanja chache tu tulizomruhusu kuingiza kichwa: Iko wapi “Tanzanite” yetu, tangu tuliporuhusu Kampuni ya AFGEM katika mgodi wa Merelani? Liko wapi Shirika letu la Ndege (ATC) baada ya kukubali ubia na Shirika la Ndege la Makaburu (SAA); na iko wapi TANESCO imara kufuatia sisi kuagiza wasimamizi (NET Group Solution) kutoka Afrika Kusini, tukawaingiza ofisini kwa mtutu wa bunduki baada ya watoto wa wakulima kugomea ujio huo?

Nani aliye nyuma ya kashfa kubwa kubwa nchini; kama zile za Meremeta, Tangold, Deep Green, Mwananchi Gold na mradi wa majengo pacha ya Benki Kuu (BOT), kama si Makaburu hao?.

Tanzania si nchi ya “ahadi” kwa wageni na wenye mitaji tata; Tanzania ni mama yetu; ni mlezi na mlinzi wa wote, waliokufa, walio hai na ambao hawajazaliwa. Kwa sababu hii, hatima ya msingi wa uhai (ardhi) na maisha ya Watanzania haiwezi kuuzwa au kuwekwa rehani kwa kauli ya TIC au ya UNDP bila, kuchochea ghadhabu ya wananchi ambao ndio wenye nchi. Huko ni kuvuka mipaka.

Kama viongozi wetu hawalioni hili, Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika ya Kimataifa, kama Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) yameliona kiasi kwamba, kwa kutuhurumia, yanataka kuwekwe maadili (Code of Conduct) na Kanuni zitakazoongoza umilikishaji ardhi; vinginevyo, wakulima wadogo wamo hatarini kupoteza ardhi yao; jambo ambalo wanaona, linaweza kutishia amani na kufanya uwekezaji kuwa mchungu.

Na kama anavyoeleza mwanaharakati mmoja wa shirika moja la Misaada la Kimataifa, “Action Aid”, Alex Wijeratna: “Kuna kupigana vikumbo sasa miongoni mwa wageni kugombea ardhi barani Afrika; na kuna usiri mkubwa kiasi kwamba, wakulima wadogo masikini hawapewi taarifa ya kinachoendelea, wala hawaombwi ushauri”.

Wijeratna anaona kuwa, kuna haja kwa Afrika kusimamisha kwanza uuzwaji wa ardhi yake kwa wageni hadi hapo mchakato wa kuweka maadili na mwongozo huo utakapokamilika; bila hivyo sehemu kubwa ya ardhi itakuwa mikononi mwa wageni muda si mrefu.

Usiri huu ndio unaotawala programu nzima ya uwekezaji hapa nchini, chini ya mpango wa KILIMO KWANZA, ambao sehemu yake ni kutekeleza sera ya Chama tawala cha African National Congress (ANC)] cha Afrika Kusini, ya kuwatafutia ardhi Makaburu wa nchi hiyo nje ya nchi, ili wao waiuzie Serikali ya ANC ardhi ambayo wanamiliki, iweze kurejeshwa kwa matumizi ya Wazalendo.

Kama kweli wataalamu wetu wanaosimamia Sera za Uwekezaji na wanasiasa hawalioni hili pamoja na uzandiki unaoambatana nalo, basi, kuna kila sababu ya kutilia shaka uwezo wao wa kuona mbali, uzalendo wao, uadilifu wao na mapenzi kwa Taifa hili.RAIA MWEMA

No comments: