Thursday, June 7, 2012

TAASISI YA MKAPA YAKUSANYA SH. BILIONI 3 KUIMARISHA AFYA TANZANIANa Leon Bahati,TAASISI ya Mkapa imedhihirisha kuwa Watanzania wana moyo wa kuchangia maendeleo yao baada ya kukusanya Sh.3.2 bilioni katika harambee ya chakula cha hisani.

Fedha hizo ambazo ni zaidi ya lengo lake la kukusanya Sh3 bilioni zilipatikana kupitia programu ya Mkapa Fellows inayolenga kuendesha miradi ya kusaidia huduma za afya nchini hasa maeneo ambayo huduma hizo ni hafifu.
Rais Jakaya Kikwete akishirikiana na Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi na Benjamini Mkapa wa awamu ya tatu, waliwahamasisha watu binafsi, kampuni, mashirika na taasisi zilizoshiriki chakula hicho cha hisani kuchanga fedha hizo.


Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya Mkapa, Dk Ellen Senkoro alisema kuwa mchango huo wa hisani wa Sh3 bilioni ni bajeti ya mwaka mmoja katika kutekeleza mpango wa miaka mitano wa kuchangia jitihada za Serikali kuimarisha huduma za afya nchini.

Dk Senkoro alisema huduma zitakazoimarishwa kupitia mpango huo ni juhudi za kukabili janga la Ukimwi, kuzuia vifo vya kinamama na watoto ili kutimiza malengo ya milenia namba nne, tano na sita.


Alisema mradi huo ni wa miaka mitano na utagharimu Sh15 bilioni huku kila mwaka ukitumia Sh3 bilioni.


Alibainisha kuwa tayari taasisi hiyo imejitanua na kusambaza wafanyakazi nchi nzima, jambo alilosema linampa matumaini ya kufanikisha malengo yao kama walivyokusudia.


Mkurugenzi huyo, alisema huduma hizo zimejikita zaidi katika maeneo matatu aliyoyataja kuwa ni kuimarisha huduma kwa waathirika wa Virusi Vya Ukimwi (VVU), huduma za afya kwa ujumla, hasa kwa wanawake wajawazito na watoto na kuimarisha mifumo ya taasisi katika sekta hiyo.


Katika harambee hiyo, Rais Kikwete alikiri kwamba licha ya juhudi za Serikali kuimarisha huduma za afya nchini, bado huduma hizo hazijafikia kiwango kinachotakiwa kama inavyopendekezwa kitaalamu.


Alitaja matatizo hayo kuwa ni pamoja na upungufu wa watumishi wenye taaluma hiyo nchini, vitendea kazi na ukosefu wa huduma kwa baadhi ya maeneo.


Aliisifu Taasisi ya Mkapa kwa juhudi zake kupunguza tatizo hilo, huku akiwahamasisha watu mbalimbali kuchangia ili kuwapa matumaini Watanzania, hasa waishio vijijini.


“Tunaihitaji sana Taasisi ya Mkapa na ufanikishaji wa miradi yake unategemea kujitoa kwenu katika kuichangia,” alihamasisha Rais Kikwete.
Hii ni mara ya kwanza kwa Taasisi ya Benjamini Mkapa, iliyoanzishwa mwaka 2006, kuendesha harambee kwa kuhamasisha Watanzania kuichangia.


MWANANCHI

No comments: