Thursday, June 28, 2012

SERIKALI IELEZE KILICHOMTOKEA DK. ULIMBOKA
Boniface Meena

MBUNGE wa Nzega, Dk Khamis Kigwangala ameitaka Serikali kutoa majibu fasaha kuhusu kilichomtokea Dk Stephen Ulimboka akieleza kuwa kilichomtokea kiongozi huyo wa madaktari kinasikitisha. Dk Kigwangala alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu tukio lililomkuba Dk Ulimboka.

Alisema kuwa ni muhimu kwa Serikali kufanya hivyo kwa kuwa Dk Ulimboka alikuwa katika harakati za kudai haki za madaktari ambapo kabla hawajafikia azma yao amekutwa na jambo la kusikitisha.

“Ukimwangalia picha zake huwezi kumtambua, tumefikia mahali kitu kama hiki kinatokea, inasikitisha sana. Kuna haja kwa Serikali kuthibitisha kuwa haijahusika kwa tukio hilo kwani taarifa silizosambaa zinaeleza kuwa imehusika,”alisema Dk Kigwangala. Alisema ni lazima Serikali iwajibike kwenye suala hilo ingawa haamini kama inaweza kufanya tukio kama hilo.

Dk Kigwangala alisema taarifa zilizopo ni kwamba Daktari huyo alipigiwa simu na mtu wa Serikali ili kuangalia namna gani wanaweza kuzungumzia kusitisha mgomo huo. Akizungumzia historia ya Dk Ulimboka alisema kuwa ni mtu mwenye msimamo mkali na asiyependa kuyumbishwa waliyekutana Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS) mwaka 1998 walipokwenda kusomea udaktari.

Alisema kabla ya Dk Ulimboka kujiunga na MUHAS alitokea Shule ya Sekondari Mzumbe ambapo alikuwa amesomea mchepuo wa Sayansi(PCB).


MWANANCHI

No comments: