Thursday, June 28, 2012

RAI YA JENERALI







ACHA KELELE, TOA HOJA




Na Jenerali Ulimwengu,

WIKI jana nilijadili hatua ya chama-tawala ya kufanya mkutano mkubwa wa hadhara na kujibu mapigo ambayo yamekuwa yakielekezwa kwake na vyama vya upinzani, hususan chama-kikuu cha upinzani, CHADEMA.

Nilisema kwamba kwa chama ambacho kimekuwa kikimbia na kukwepa mihadhara hii, ilikuwa ni dalili njema kwamba sasa kimegundua kwamba kinapata hasara kwa kuwaachia wapinzani watambe bila majibu.

Hata hivyo, nilikitahadharisha chama-tawala kuhusu hatari ya kufanya makosa mengine na kuyaongeza juu ya yale kilichokwisha kuyafanya, ambayo nayo si haba. Leo napenda kuendelea na ushauri wangu kwa chama hicho, kama kinao uwezo wa kusikiliza na kujifunza kutoka kwa watu wasiokuwa makada wake.

Hata kama hakina uwezo huo, huu ni ushauri unaoweza kuchukuliwa na kufanyiwa kazi na wanasiasa wa chama cho chote, pamoja pia na watu wasiokuwa wanasiasa ambao wanajishughulisha na ujenzi wa hoja katika nyanja zao.

Wahenga walisema kwamba kisichotumika huvia, kwa maana kwamba chombo cho chote kikiachwa bila kazi au mazoezi kwa muda fulani kitapoteza ukali wake, au uwezo wake wa kufanya kila ambacho kilitarajiwa kifanye. Jembe lisilolimishwa, au panga lisilofyekewa hupoteza makali yake na kuwa butu. Tunajua pia kwamba hata misuli ya mwili wa binadamu inahitaji mazoezi ili iwe na nguvu, na kama itaachwa bila mazoezi, itadhoofu na kulainika.

Ubongo wa binadamu nao vivyo. Ubongo usipotumika kufikiri na kutatua matatizo na kufumbua mafumbo hupoteza uwezo wake na ukali wake, hatimaye ukawa butu. Athari hii inakuwa kubwa zaidi kadri ubongo unavyokua, ukapevuka na kuanza kuzeeka. Ubongo wa mzee unahitaji mazoezi zaidi ili kuuweka katika hali ya kufanya kazi kuliko ubongo wa kijana. Mara nyingi hata weledi unaodhihirishwa na wazee juu ya vijana hutokana na uzoefu wa wazee kuliko ukali wa bongo zao.

Hii inanipeleka moja kwa moja katika shughuli ambayo chama-tawala kinaelekea kinataka kuifanya, nayo ni shughuli ya kwenda kwa wananchi na kujibu shutuma kilichoelekezewa na wapinzani, ambao, kama tunavyojua, nia yao ya wazi kabisa ni kukiondoa chama hicho madarakani. Sasa kinataka kujibu, na kimeanza pale Jangwani.

Kama nilivyosema wiki ilyopita, jambo la kwanza ni lazima kifanye mikutano ya hadhara ili kufanya kazi ya kisiasa. Kielezee kwa ufasaha mkubwa falsafa yake ni nini, itikadi yake ni ipi na sera zake zimejengeka juu ya itikadi na falsafa ipi. Sina uhakika kama chama hiki bado kimesimama juu ya misingi ya falsafa ya Usawa wa Binadamu ambayo ilifafanuliwa katika Azimio la Arusha, ambalo ndilo lililoasisi siasa ya chama hicho ya Ujamaa na Kujitegemea. Iwapo bado chama hicho kimesimama juu ya falsafa hiyo na itikadi na siasa hiyo, kijitokeze na kusema hivyo.

Iwapo kilikwisha kuondoka huko, kama ambavyo mimi binafsi nashuku, sasa kijitokeze kiseme kwamba kilikwisha kuachana na mambo hayo, kitoe sababu za hatua yake hiyo, na kisha kitamke waziwazi ni falsafa ipi inakisukuma kwa sasa, na itikadi yake mpya ni ipi ambayo ndiyo inaelekeza na kuendesha siasa zake na sera za utekelezaji katika kuliongoza Taifa hili. Kwa maneno mengine, hakiwezi kikaendelea hivi hivi, bila falsafa, itikadi, siasa wala sera.

Chama-tawala kina bahati mbaya, kama aliyo nayo mtoto wa imamu anayekuwa mlevi, kwa sababu watu watamsuta kwa kumkumbusha juu ya baba yake. Wala chama-tawala hakiwezi kuwa kama vyama vya upinzani, ambavyo navyo havitamki falsafa yake, bali vinachosema ni kwamba vinataka mabadiliko tu, basi. Kwa vyama vya upinzani, kutaka mabadiliko tu inatosha, lakini haiwezi kutosha kwa chama-tawala kusema hakitaki mabadiliko, basi!

Hii ni kwa sababu hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kuwambia wananchi wa Tanzania kwamba hali ya mambo kama ilivyo leo haihitaji mabadiliko. Tunaweza kulumbana juu ya aina ya mabadiliko na nani atakayeyaongoza, lakini ni rai yangu kwamba haiyumkiniki kusema kwamba hatuhitaji mabadiliko. Mabadiliko yanahitajika JANA.

Maisha ya wanachi yamezidi kuwa dhalili; kila ishara tuzionazo zinasharia maisha magumu zaidi; watu wanashindwa kumudu maisha ya msingi kabisa katika mahitaji ya chini kabisa kama chakula cha kawaida, malazi ya kawaida, mavazi ya kawaida na usafiri wa kawaida.

Wakati huo huo, wanaiona nchi yao na utajiri wake ulivyo mkubwa kupindukia bila kuwapa ahueni ya maisha; wanajiuliza maswali mengi lakini hawapati majibu, na badala yake kila swali wanalouliza linazua maswali mengine badala ya majibu.

Wengi wanashuku kwamba viongozi wao hawawatendei haki, na kwamba wanachofanya ni kujinufaisha wao na watu wao wa karibu, wakishirikiana na matajiri wa ndani na nje ya nchi ambao ndio wamesabiliwa rasilimali za Taifa ambazo wanazitumia watakavyo.

Wananchi si wajinga, si vipofu, lakini hata wajinga na vipofu leo wanatambua na leo wanaona. Chama-tawala kinayajua haya, na kiko tayari kutoka nje na kufanya mikutano mikubwa kama ule wa Jangwani majuzi, na kuyazungumzia haya? Au kitaendelea kutoa taarifa za utendaji kazi wa Serikali, ambalo bila shaka ni jambo jema lakini si jukumu la chama kwenda Jangwani kueleza.

Napenda sana kusikiliza takwimu za idadi ya kilometa zilizojengwa “kwa kiwango cha lami,” lakini hizi naweza kuzipata katika mitandao nikitaka. Iwapo tunataka kujadili “viwango vya lami” ni bora tujadili “viwango vya lami” hivyo ni viwango vya lami inayobanduka, kuchimbika au kuumuka kama mabonge makubwa ya ugali mweusi baada ya miezi mitatu ya kukabidhiwa?

Viwangio gani vya lami, ile ya Barabara ya Kilwa au ile ya Mlandizi /Chalinze, yenye mawimbi yanayoyumbisha gari kiasi cha kutishia maisha? Huwa najiuliza, na naamini watu wengine pia hujiuliza, hivi inawezekana barabara kama hizi zikakabidhiwa kwa wakuu wa serikali nao wakazipokea, halafu asiwepo mtu aliyekwenda jela, aliyefukuzwa ukurugenzi, au kufutwa katika orodha ya makandarasi?

Waziri aistuhesabie kilometa za kukariri; ubongo wa waziri unatakiwa ufanye kazi nyingine, ngumu zaidi kuliko kukariri, nayo ni kuongoza sekta ya miundombinu kwa kutekeleza sera za serikali yake zinazotokana na itikadi ya chama chake, iliyojengeka juu ya falsafa inayojulikana, kama nilivyosema hapo juu. Iwapo ni falsafa ya Usawa wa Binadamu, waziri bila shaka atausumbua ubongo wake kujua iwapo miundombinu inayojengwa inawapa watu wote fursa sawa za usafiri na usafirishaji; kwamba mikoa yote itatendewa haki, wilaya zote zitaangaliwa kwa usawa; kwamba maeneo ya watu wa kipato cha chini hayatatelekezwa; kwamba watemnbea kwa miguu na wapanda baisikeli nao ni raia wenye haki ya kutumia barabara kwa usalama wa maisha yao, na kadhalika.

Kisha, waziri asituambie kwamba idadi ya kilometa za barabara alizojenga zingejengwa Burundi nchi hiyo isingebakiwa na eneo la kulima. Ndiyo maana yeye si waziri wa Burundi, ni waziri wa Tanzania, na napaswa kuiangalia Tanzania. Na wala hakuna sababu ya kuwabeza wapinzani eti watatumia barabara hizo hizo kuandamana kutaka kuking’oa chama-tawala madarakani. Kumbei wangepita wapi?

Nimesema hapo juu kwamba kisichotumika huvia. Tumepoteza mazoea ya kujadili na kupambanisha hoja. Ndani ya chama-tawala, mazoea hayo yamekuwa yakimomonyoka taratibu kwa muda wa miongo miwili hivi, kiasi kwamba chama hicho kimejiruhusu anasa ya kwenda kwa miaka 20 bila mijadala ya maana, badala yake kikisherehekea kaulimbinu za kishikaji, mipasho ya uwani na vijembe vya kijiweni.

Kubishana na kupambanisha hoja (argumentation and disputation) imekuwa ni dhana ngeni, ingawaje ndani ya chama chenyewe wamo wasomi waliobobea ambao wamejiruhusu kuvia kwa sababu hawatakiwi kutumia umahiri wao katika argumentation and disputation. Wamekubali kuongozwa na wenzao ambao kwao mambo haya ni mageni. Ni hasara iliyoje tunaposhuhudia kipofu akimuongoza mwenye kuona !

Katika miaka ya 1970 Mwalimu Julius Nyerere aliwaasa wanadiplomasia wa Tanzania katika kijitabu kidogo, Argue, don’t shout (Toa hoja, usipige kelele). Nadhani wanasiasa wote wangekitafuta kijitabu hiki muhimu na wakidurusu kwa makini.

Ni namna gani chama-tawala kinaweza kujirudi, kikakumbuka (kama bado kina kumbukumbu) kilikotoka na kikafanya kazi ya kujijenga upya, mimi sijui, lakini hakina budi kujikagua kwa makini kama kinataka kushiriki katika mijadala inayokikabili zaidi kadri tunavyokaribia mwaka 2015.


RAIA MWEMA

No comments: