Wednesday, June 6, 2012

MWAKYEMBE APELEKA KILIO ATCL
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ametengua uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Paul Chizi na amewasimamisha kazi wakurugenzi wanne kutokana na “ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, ambao umetishia uhai wa shirika hilo muhimu kwa taifa.”Kutokana na hatua hiyo, Dk Mwakyembe amemteua rubani wa siku nyingi katika shirika hilo, Kapteni Lusajo Lazaro kukaimu nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Chizi.


Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Omary Chambo alisema Dar es Salaam jana kwamba Waziri amefikia uamuzi huo kutokana na taratibu za uteuzi kwa wafanyakazi wa umma kutokufuatwa.


Alisema nafasi aliyopewa Chizi haikutangazwa kama sheria na kanuni zinavyotaka... “Uteuzi wake haukufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, hivyo kupitia Sheria Na 8 ya mwaka 2002 na kanuni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2003 Na 17(4), Dk Mwakyembe ametengua
uteuzi huo kuanzia jana.”


“Kanuni hii inaeleza bayana kuwa kama mtumishi atakuwa ameteuliwa kwa kukiuka Kifungu cha 17(1 au (3) za Kanuni za Utumishi za mwaka 2003, itakuwa ni mamlaka ya uteuzi wa kutengua uteuzi wa utumishi wake mara moja.”


Kabla ya kuteuliwa na kushika wadhifa huo na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Chizi aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Community Airline.


Wakurugenzi wanne waliosimamishwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Uhandisi, John Ringo, Mwanasheria wa ATCL, Amini Mziray, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Justus Bashara na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Josephat Kagirwa.


Mhandisi Chambo katika taarifa yake kwa umma, alisema kutokana na ukiukwaji huo wa taratibu, itaundwa kamati yenye wajumbe watatu wenye uelewa wa mambo ya fedha na sheria kuchunguza matumizi ya fedha zilizopokewa kuanzia mwanzoni mwa Mei mwaka huu.


Alipoulizwa ni fedha kiasi gani kilichopotea, alisema tu kwa kifupi: “ni fedha nyingi sana kutoka idara mbalimbali.”


Hatua hiyo ya Dk Mwakyembe imekuja siku chache baada ya kuonya kwamba atalifumua Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) ambalo pia lipo chini yake baada ya kuona linasuasua kama ilivyo ATCL.


ATCL lilianza kuwa hoi baada ya kuingia ubia na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) mwaka 2002 na baada ya kuvunjika kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATC).


Tayari Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amewahi kuishauri Serikali kuwa vema ingelivunja shirika hilo na kuliunda upya.


CAG katika ripoti yake ya mwaka huu alipendekeza kwamba uongozi uliokuwapo ulishindwa kuonyesha mikakati ya namna gani wangelitoa shirika hilo lilipo na kulipeleka mbele.
MWANANCHI

No comments: