Thursday, June 28, 2012

MAELEZO YA DK. DEOGRATIUS MICHAEL KUHUSU KUDHURIWA KWA ULIMBOKA


Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la Dkt. Ulimboka kudhuriwa, Dk. Deogratius Michael, alisema:


“Jana (juzi) usiku, tulikuwa na Dkt. Ulimboka maeneo ya Leaders Club Kinondoni na ghafla walifika watu watano wakiwa ndani ya gari aina ya Suzuki Escudo lenye rangi nyeusi lisilokuwa na namba za usajili.

“Watu hao walikuja mpaka mahali tulipokuwa na kujitambulisha kuwa ni askari polisi na wanamhitaji Dkt. Ulimboka Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.

“Baada ya askari hao kumchukua Dkt. Ulimboka na kuondoka naye, sisi tulikwenda kituo hicho cha polisi ili kujua kwa nini wamemchukua, lakini tulipofika hatukumkuta na badala yake tulitoa maelezo na kuondoka.

“Pamoja na kutomkuta, tuliendelea kumtafuta kwa njia ya simu lakini hakupatikana hadi tulipopigiwa simu leo asubuhi na msamaria mwema akitueleza kuwa Dkt. Ulimboka yupo Mabwepande ametelekezwa na amejeruhiwa vibaya.

“Nilipopokea taarifa hiyo, niliwatafuta watu wengine, tukaondoka kwenda Mabwepande na kumkuta Dkt. Ulimboka akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na meno yote pamoja na kucha zikiwa zimeng’olewa na inaonekana walitumia ‘plaizi’ na tulipomchunguza vizuri, tuligundua pamoja na kung’olewa meno na kucha pia amevunjwa taya.

“Nilipomuona sikuamini kama yule ni Dkt. Ulimboka, alikuwa uchi na mwili mzima ulikuwa na majeraha makubwa, nilizungumza naye akawa anaongea kwa shida, lakini nilimuelewa.

“Kwa mujibu wa Dkt. Ulimboka, anieleza kuwa baada ya kuchukuliwa pale walianza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili na kuishiwa nguvu na walipoona yuko hoi walianza kushauriana.

“Walikuwa wanashauriana kwamba wampige risasi, wengine wanakataa, wakapendekeza wamweke barabarani na kumgonga na gari ili ionekane amegongwa na gari, mwingine akakataa, akasema wamdunge sindano yenye sumu na kumuua lakini pia hawakukubaliana.

“Dk Ulimboka alinieleza kwamba, baada ya kutafakari yote walifikia uamuzi wa kumpeleka msitu wa Mabwepande baada ya kuonekana muda wowote anaweza kufariki na kumvua nguo zote na kuchukua simu zake zote,” alisema Dk. Deo.

Kutokana na hali hiyo, alisema walitoa taarifa Kituo cha Polisi Bunju na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kupata gari la wagonjwa.

“Jambo la ajabu ni kwamba, Muhimbili waligoma kabisa kutoa gari la wagonjwa, hivyo tukalazimika kukodi gari jingine la wagonjwa kutoka Kampuni ya AAR,” alisema.

Alisema kampuni hiyo iliwapatia gari lenye namba za usajili T151AVD na kumleta Hospitali ya Muhimbili ili kupata matibabu. Hata hivyo alisema hali yake wakati anafikishwa ilikuwa mbaya na alilazwa katika Chumba cha Wagonjwa mahututi (ICU).

No comments: