Wednesday, June 20, 2012

C.A.G KUHAKIKI MALI ZA NMC

Patricia Kimelemeta

OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG)imeanza kuhakiki na kuchunguza mahesabu ya lililokuwa Shirika la Usagishaji la Taifa(NMC) baada ya kubaini kuwa shirika hilo bado liko hai.

Mahesabu hayo yanahusisha mali za shirika,vinu vya kusagisha pamoja na viwanja kikiwemo kitalu namba 10 kilichosababisha aliyekuwa Waziri wa |Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kujiuzulu baada ya kudaiwa kukiuza bila ya kufuta taratibu za kisheria kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises(MeTL).

Akizungumza kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG)Ludovick Utouh alisema awali shirika hilo lilikuwa halisikiki, jambo ambalo waliamini kuwa limekufa.

Alisema kutokana na taarifa zilizotolewa hivi karibuni za kuwepo hai kwa shirika hilo, wameanza kuwasiliana na ofisi husika ili waweze kubaini ukweli wake, na kuanza kuhakiki mali za shirika hilo.

Alisema kutokana na hali hiyo wataanza kukagua tangu lilipotangaza limekufa,hadi walipofikia sasa ili waweze kujiridhisha uhalali wake pamoja na mali wanazomiliki.

“NMC iko chini yetu, lakini tulijua kuwa limekufa,ila baada ya kupata taarifa kama lipo hai tumeanza mchakato wa kulifuatilia ili tuweze kufanya ukaguzi wa mali na mahesabu yake tangu lilipotangazwa limekufa hadi sasa,”alisema Utouh.

Aliongeza kutokana na hali hiyo, wanaamini kuwa uhalali wake wa kuendelea kuishi utabainika ikiwa watamaliza kazi ya kuhakiki mali za shirika hilo.

Hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC)imeunda Tume ndogo ya kuchunguza mali zinazomilikiwa na NMC.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya POAC kudai kuwa mali za NMC hazijulikani vema,lakini mpaka sasa shirika hilo lina Mkurugenzi ambaye analipwa mishahara kutokana na pango la majengo yake,lakini mpaka sasa hawana kitabu cha benki kinachoonyesha kiasi cha fedha zilizopo ambazo zimetokana na pango la majengo yake.

Kamati hiyo ilifafanua kuwa kuna nafasi kubwa ya kuwapo kwa wajanja ambao wamerithi mali za NMC bila ya Serikali kujua jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa kuna ubabaishaji ndani yake.


MWANANCHI

No comments: