Thursday, May 10, 2012

MAWAZIRI WAACHE AHADI TUNAHITAJI VITENDO

Moja ya mambo tuliyoshuhudia baada ya mawaziri wapya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete na kuanza kazi zao rasmi juzi ni ahadi lukuki za mawaziri hao kuhusu mambo watakayoyapa vipaumbele katika wizara zao na jinsi watakavyopambana kufa na kupona dhidi ya rushwa na ufisadi. Katika masikio ya watu wengi, ahadi hizo zilisikika kama marudio ya ahadi zilezile zilizowahi kutolewa na mawaziri waliowatangulia.

Pamoja na mawaziri hao kutoa ahadi hizo lukuki, wananchi wengi hawakuguswa na ahadi hizo au kuamini kwamba sasa nchi inaelekea kule inakopaswa kwenda, kwa maana ya kuwa na mawaziri wa miavuli na wachapakazi wenye dhamira, uadilifu na uwezo wa kusimamia uchumi na kupiga vita rushwa na ufisadi. Baadhi ya wananchi walibeza ahadi hizo, huku wengine hata wakithubutu kusema baraza hilo ni sawa na mvinyo mpya katika chupa ya kale.

Mtazamo huo wa wananchi siyo tu lazima uwazindue wote walioteuliwa kuunda Baraza la Mawaziri, bali pia na Rais Kikwete mwenyewe ambaye aliwateua na hakika ni ishara tosha kwamba wananchi wamechoshwa na maneno matupu na ahadi hewa zinazotolewa na viongozi. Mawaziri sharti wasome maandishi yaliyo ukutani kwamba wananchi hawako tayari kutumiwa tena na wanasiasa kama ngazi ya kutafuta madaraka na kwamba wanachotegemea kutoka kwao ni utendaji wenye ufanisi utakaoweza kuwapunguzia mateso yatokanayo na umaskini wa kutisha unaowakabili.

Hivyo, mawaziri hao hawana namna nyingine ya kufanya isipokuwa kukaa chini na kuchapa kazi kwa ufanisi, huku wakihakikisha hawaingii katika mtego wa rushwa na ufisadi uliowanasa na kuwaumbua baadhi ya watangulizi wao. Mawaziri hao hawategemewi kupoteza muda katika kusherehekea uteuzi wao na tunathubutu kusema kwamba hawawezi kufanya hivyo kwa sababu siyo tu hawana muda wa kusherehekea, bali pia hakuna kitu cha kusherehekea. Tunasema hivyo kwa sababu kazi waliyopewa ni nzito kiasi cha kuwafanya waone dhamana waliyope kuwa mzigo. Bahati mbaya wananchi wamechoka na hawana subira tena, hivyo mawaziri hao wanategemewa waonyeshe mafanikio katika kazi zao katika muda mfupi tu ujao.

Kwa maana hiyo, hatutegemei mawaziri hao wapya na wale waliohamishiwa katika wizara nyingine waendeleze utamaduni uliopitwa na wakati wa kutembelea idara na taasisi zilizo chini ya wizara zao kwa kisingizio cha kujitambulisha na kubadilishana uzoefu na wafanyakazi. Kwanza, hawana muda wa kupoteza. Pili, ziara kama hizo zilizofanywa na watangulizi wao hazikuleta mafanikio yoyote. Tatu, muda waliotumia katika makabidhiano ya ofisi juzi ulitosha kabisa kwa kila waziri siyo tu kujua matatizo yaliyopo katika wizara aliyopewa kuiongoza, bali pia kujua vipaumbele anavyopaswa kuvifanyia kazi kwanza.

Kwa mfano, Waziri Mwakyembe haitaji kutembelea ATCL, Reli ya Kati, Tazara na Bandari ili kujua madudu yaliyopo. Anajua kwamba viongozi serikalini ndio walioua ATCL ili kununua hisa katika mashirika binafsi ya ndege na kwamba ndiyo walioua reli za Tazara na Kati ili waanzishe makampuni binafsi ya kusafirisha mizigo na abiria kwa njia ya barabara. Madudu yaliyoko bandarini ni siri iliyo wazi kwa kila mtu.

Hivyohivyo, Waziri Mwinyi hana sababu ya kutembelea hospitali, kwani matatizo ya rushwa, ufisadi, ukosefu wa dawa, wajawazito kujifungulia sakafuni na wagonjwa sita kulala kitanda kimoja, kwa mfano, bado yapo palepale. Mawaziri wa masuala ya nishati, madini, kilimo, Tamisemi, maliasili, utalii, fedha na nyingine nyingi pia hawana sababu ya kupoteza muda eti kwa lengo la kujitambulisha na kadhalika, kwani wanapaswa kujua fika nini matatizo yaliyoko, kiini chake na mbinu za kuyatatua.

Tumesema yote hayo kwa lengo la kuwasaidia mawaziri hao kutambua kwamba nyakati za viongozi kuwaghilibu wananchi na kutumia ofisi za Serikali kama mali binafsi zimekwisha. Kama tulivyosema hapo juu, wananchi wamepoteza matumaini. Ni matumaini yetu kwamba mawaziri hao watafanya kila wawezalo kurudisha imani yao kwa Serikali, vinginevyo wategemee suluba muda siyo mrefu kutoka sasa.MWANANCHI

No comments: