Friday, May 11, 2012

MABADILIKO BARAZA LA MAWAZIRI: JARIBIO LA MWISHO LA KUOKOA CCM
Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,

KUNA msemo wa Kiswahili kuwa ‘siku ya kufa nyani miti yote huteleza’. Upo pia msemo mwingine kuwa ‘mfa maji haachi kutapatapa’. Misemo yote hii na mingine mingi yenye maudhui kama haya inataka kutukumbusha tu kuwa kuna wakati mtu anafanya kila awezalo ili kujiokoa na janga au jambo fulani ambalo kwa kweli haliepukiki. Misingi ya misemo hiyo ni kutufanya tuelewe na kutambua kuwa kile kinachojaribiwa kufanywa ili kujiokoa kwa kiasi kikubwa hakitakuwa na matokeo yanayotarajiwa. Waingereza wanasema ni ‘an exercise in futility’ yaani ‘jaribio lisilozaa matunda’.

Tangu aingie madarakani Rais Jakaya Kikwete amejaribu na kujitahidi sana kutawala na kuongoza nchi. Ndani ya miaka sita sasa tumekuwa na mabaraza ya mawaziri manne – karibu kila baraza likikaa kwa miaka miwili tu hivi na kama rekodi hii itaendelea basi kabla kidogo ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kutakuwa na mabadiliko mengine ya Baraza la Mawaziri ukiondoa udharura mwingine wowote unaoweza kusababisha mabadiliko mapema zaidi.

Baraza la kwanza ni lile aliloingia nalo mwaka 2005 mara baada ya Uchaguzi Mkuu. Kimsingi baraza lile lilitakiwa liwe la ‘timu ya kufikirika’ kwamba ni timu nzuri zaidi na ambayo imebeba ridhaa kubwa ya Watanzania. Baadhi yetu tuliamini – kwa makosa – kuwa baada ya kupata asilimia 80 ya wapiga kura Rais Kikwete angeongoza mabadiliko makubwa zaidi hasa tukirejea ile hotuba yake ya bungeni mwishoni mwa 2005. Katika hotuba ile alizungumza maneno mengi yenye kuleta matumaini kwa wananchi.

Matumaini yetu yalizidishwa sana na kile kilichofuatia baada ya baraza kuundwa – ambacho sasa yawezekana kimeshasahauliwa yaani ‘semina ya Ngurdoto’. Kwa mara ya kwanza tulipewa matumaini kuwa labda mawaziri hawajui sana mambo wanayotakiwa kufanya na hivyo ile semina ilikuwa ni ya kuwaweka sawa ili wote wajue wanachezea timu gani na wanataka kufanya nini kutimiza matamanio ya Watanzania. Hotuba za Ngurdoto zilitutia matumaini sana kuwa Kikwete amepania kweli kuonesha uongozi! Najua wengi wameshaisahau lakini miye nimejaliwa kumbukumbu kidogo kwani naelewa hakuna kitu ambacho kinachofanywa leo na CCM ambacho hakijawahi kufanywa nyuma.

Katika ufunguzi wa ‘semina elekezi’ ile ya Ngurdoto Machi, 2006 Rais Kikwete alizungumza mengi sana ya matumaini kwa makamanda wake wa timu ya kwanza. Rais Kikwete alisema kitu ambacho kilikuwa kweli mwaka 2006 kama vile ni kweli leo hii.

Alisema hivi; “Changamoto kubwa na mtihani mkubwa tulionao sote ni ule wa kutimiza matumaini ya Watanzania kwetu kama viongozi wao na kwa Serikali tunayoiongoza kama chombo cha utekelezaji. Wajibu wetu wa kwanza hapa ni kujua kwa uhakika wananchi wanataka nini? Wana shida gani? Wanakerwa na lipi baya tuliondoe? Kwa maoni yangu Watanzania wanapenda kuwa na viongozi ambao wanawasikiliza, na wanaojali kushughulikia mambo yao (wananchi). Wananchi wanapenda kuona Serikali yao ina viongozi na watumishi wanaoheshimu maadili ya utumishi wa umma. Wachapa kazi hodari, wanaosikiliza shida za wananchi, wanaojali na wepesi kutekeleza. Kadhalika wangependa kuona viongozi na watumishi wa umma waadilifu, wasioomba wala kupokea rushwa katika kuwatumikia. Wanaochukia maovu na dhuluma. Watumishi wa umma wanaotenda haki na kuendesha mambo yao kwa uwazi na ukweli.”

Sasa, ni wazi kuwa alijua kabisa wananchi wanatarajia nini kwani jambo hilo halijabadilika. Watanzania hawahitaji viongozi wabovu, wabinafsi, wanyanyasaji, au wenye kutumia madaraka yao vibaya. Watanzania wanataka viongozi ambao wanaweka maslahi ya wananchi na ya taifa juu kuliko kingine chochote. Lakini, sote tunatambua siyo viongozi wengine tu hata yeye mwenyewe inaweza kujengwa hoja kuwa hakuishi kutimiza ndoto hiyo au matamanio hayo. Je, yeye mwenyewe alikuwa mwepesi kutekeleza (fikiria suala la mgomo wa madaktari au mambo ya Jairo); je, yeye mwenyewe amekuwa upande gani wa dhuluma (tumeona ya Arusha, Tarime, Mwanza na Songea alikuwa wapi?); je, kwenye maadili ya umma yeye amekuwa upande gani kuyasimamia hasa baada ya ripoti sita za CAG?

Pamoja na semina ya Ngurdoto Watanzania pia wanakumbuka ‘ziara’ za Rais kwenye wizara mbalimbali katika kile alichokiita ‘kueleweshana’. Tunakumbuka alivyotembelea wizara mbalimbali na kutoa maneno mengi ya kutia moyo. Sasa zote hizo zilitarajiwa kuwa ni kuwekana sawa na ya kwamba viongozi wangeelewa ni kitu gani kiko mbele yao.

Kama vile watu waliopoteza uwezo wao wa kukumbuka, tangu mwaka 2006 hadi leo tumekuwa na mabaraza kimsingi manne haya. Baraza la kwanza lililoundwda kwa mbwembwe zote halikudumu kwani mwaka 2008, Februari lilivunjika baada ya Waziri Mkuu kujiuzulu. Baraza lililofuatia likadumu kwa kiasi huku mabadiliko kadhaa yakifanyika kidogo hadi uchaguzi na baadaye baraza jipya baada ya uchaguzi wa 2010 na sasa haya ya juzi.

Hata hivyo mabadiliko ya juzi yanalengo moja tu lililo wazi – kusaidia kupunguza kasi ya CCM kuvuja damu kufuatia kuchapwa vibaya na CHADEMA kwenye Uchaguzi Mkuu na sasa wimbi la wananchi waliofunguka kuanza kuikataa CCM kwa mamia yao katika kile kinachoitwa ‘vua gamba, vaa gwanda’! Baraza hili kwa kweli kabisa limeundwa ili kuhakikisha kuwa CCM inaokolewa na kuopolewa katika kuzama kuliko dhahiri.

Kwa kuangalia kwa ukaribu unaweza kuona kitu kimoja kiko wazi sana kwenye baraza hili – makada wa CCM wamepangwa kushika nafasi nyeti. Si kwa sababu wana weledi mkubwa au ni viongozi wazuri la hasha bali ni kwa sababu ni makada wazuri wa CCM. Tunachotakiwa kutarajia basi ni kuwa baraza hili la sasa ni baraza la vita (war council); litashambulia watu wote walio kinyume nao, litakuja na mapendekezo ya ajabu kwenye sera, na halitakuwa na msalia mtume na mtu yeyote ambaye anaifanya CCM ionakane mbaya. Tutarajie haya kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Jeshi la Polisi, Mawasiliano na Teknolojia na kwa uhakika kabisa kwenye Utawala Bora (usalama wa taifa). Sehemu hizi zote zitajipanga kujibu mashambulizi na hakuna ambaye atakuwa salama.

Ukweli ni kuwa hakuna wa kuwalaumu kwani wao kama wana CCM wana kila sababu ya kupigania CCM kwani wasipofanya hivyo, baraza hili ndilo ambalo litashuhudia kuanguka kwa CCM kuanzia 2014 (kwenye serikali za mitaa) na kutimilika kwa anguko hilo kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015. Kwani unabii lazima utimilike na tayari umeanza kutimilika kwa kasi kubwa.

Habari mbaya kwa baraza hili ni kuwa hakuna lolote watakalofanya sasa hivi ambalo litaokoa CCM; kwani litakapoanza mapambano yake ya kuokoa CCM ndivyo litakavyozidi kupandikiza chuki na hasira dhidi ya chama hicho kikongwe nchini. Kitu pekee wanachoweza kufanya sasa ni kuhakikisha kuwa CCM itakapoondoolewa madarakani isije kusambaratika kabisa! Na hili litakuwa.


RAIA MWEMA

No comments: