Friday, May 25, 2012

KUTOKA 'CAMP DAVID' HADI KIJIJINI NANJILINJI MTWARANa Godfrey Dilunga,

KWA vigezo vyovyote vile, kuna umbali mrefu sana na tofauti kubwa kati ya wanakijiji wanaoishi kijijini Nanjilinji, mkoani Mtwara, kusini mwa Tanzania na eneo la makazi ya mapumziko ya Rais wa Marekani, yaani Camp David, Jimbo la Maryland.

Camp David ni eneo la mapumziko ya Rais wa Marekani. Ni eneo ambalo wakuu wa nchi nane tajiri duniani (G8) wamekutana kwa ajili ya kupanga mikakati yao ya namna ya kuendelea kuwa matajiri na kwa upande mwingine, kuahidi kusaidia masikini katika nchi masikini, ikiwamo Tanzania.

Ndiyo, si tu umbali kati ya Kijiji cha Nanjilinji-Mtwara na Camp David – Maryland ni mkubwa, bali pia samani na nakshi zinazopamba Camp David bila shaka gharama zake kwa ujumla zimevuka kwa mbali mno mapato yanayotokana na uvunaji wa rasilimali asilia zilizopo Nanjilinji.

Maryland ni eneo ambalo halina utajiri wa kuvunwa ikilinganishwa na Mkoa wa Mtwara. Lakini Maryland kuna Camp David na Mtwara kuna vijiji, kikiwamo Nanjilinji. Mtwara kuna korosho pamoja na hazina ya gesi inayoweza kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu za mwanzo duniani katika uuzaji nje gesi.

Matajiri hawa waliokutana pale Camp David, Maryland msingi wa utajiri wao ni viwanda. Bila shaka, wao ni miongoni mwa wanunuzi au wawekezaji wakubwa katika kuja kuvuna gesi ya Mtwara.

Kwangu, naiona Mtwara pamoja na Nanjilinji yake ni muhimu zaidi kwa matajiri hawa kuliko ilivyo Camp David isiyo na rasilimali nyingi za kuvunwa kuendeleza viwanda.

Swali muhimu ni je, viongozi wetu wanaona hivyo au wanaitamani tu Camp David kuliko Mtwara? Je, bado wataendelea kutamani kuzishinda nchi nyingine (masikini) katika kinyang’anyiro cha “nchi za kwanza Afrika kusaidiwa na matajiri wa G8?”

Au wataanza kuhisi aibu na kisha kutafakari namna gani wanaweza kutumia rasilimali zilizopo kwa umakini ili hatimaye maisha ya Watanzania yawe bora zaidi na siku moja, wakubwa wa G8 waalikwe katika Camp David ya Tanzania?

Ndiyo, korosho za Nanjilinji na gesi ya Mtwara ni uchumi imara wa kutengeneza Camp David yetu itakayokuwa ishara ya maisha mazuri miongoni mwa Watanzania ili siku moja tushiriki katika vikao G8 tukiwa na uwezo wa kuahidi misaada kwa nchi masikini ambazo Tanzania haitakuwa mojawapo tena.

Ni aibu kwa sasa. Kwa mfano, nyasi na maua yaliyooteshwa kwenye bustani ya Rais Obama pale Camp David bila shaka yanatunzwa kwa fedha nyingi mno ikilinganishwa na mikorosho ya mkulima wa Nanjilinji.

Mikorosho ambayo inatarajiwa kuvunwa ili kumlipia ada mtoto, kununua chakula cha familia pamoja na kugharimia matibabu ya wanafamilia na hapo hapo, Serikali ya Tanzania kumkamua kodi mkulima huyo kila anaponunua bidhaa za msingi kama sabuni au dawa.

Kodi ambayo wakati mwingine ndiyo inachangia nauli inayotumiwa na Bwana Mkubwa kuhudhuria mialiko ya Camp David na kwingine.

Lakini pamoja na hayo, korosho kutoka katika mikorosho ya mkulima wa Nanjilinji zinauzwa zikiwa ghafi, hazitoi mchango mkubwa katika kuinua hali za maisha za Wananjilinji.

Yule mtoto wa mkulima anayelipiwa ada kwa fedha za mauzo ya korosho ghafi atakapomaliza masomo, anakabiliwa na kitisho cha kukosa ajira. Anakosa ajira kwa sababu kijijini kwake au wilayani kwake hakuna kiwanda cha kubangua korosho anazolima baba au mama yake.

Ni busara kiwanda cha namna hiyo kijengwe kama si kijijini kwao angalau wilayani kwao na matarajio ni kwamba ajira kwa mtoto au watoto wanaosomeshwa kwa fedha za mauzo ya korosho ipatikane, lakini kwa sababu zisizo na mantiki, hakuna kiwanda cha namna hiyo na kama vipo katika baadhi ya maeneo tatizo ni umeme.

Viwanda cha namna hiyo tena vyenye ubora kiteknolojia vipo nchi nyingine, vinaendelea kutoa ajira kwa vijana wa nchi hizo. Kwetu hapa wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, tuliwahi kuamua kuanza safari ya kuwa nchi ya viwanda lakini tukaviua, sasa tunaalikwa na nchi ambazo msingi wa utajiri wake ni viwanda.

Tuliwahi kuwa na viwanda vya nguo (Sungura textiles na vingine vingi) vinavyoongeza thamani mazao ya mkulima kiasi cha kutoa bidhaa zinazopunguza matumizi ya fedha za kigeni ambazo zingeweza kutumika kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

Tusipoangalia ipo siku tutaagiza korosho kutoka nje kama tunavyofanya sasa kuagiza mchele kutoka China na Taiwani wakati mabonde lukuki ya kilimo yapo nchini.

Hizi korosho ghafi kutoka Nanjilinji na vijiji vingine pale Mtwara pengine ndizo zilizokuwapo mezani pale Camp David na pengine, Rais Jakaya Kikwete aliyealikwa na Rais wa Marekani, Barack Obama kushiriki vikao vya G8, amekula korosho zetu za Nanjilinji akiwa huko Camp David.

Inawezekana Kikwete na wenzake pale Camp David ambao ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi; Rais wa Benin, Yayi Boni (Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika); Rais wa Ghana, John Mills wamekula korosho zetu za Nanjilinji ambazo hawakuzitambua kwa sababu makasha yake yamepigwa muhuri wa moja ya viwanda vya nchi nane tajiri duniani (G8).

Inawezekana wamelishwa korosho za Nanjilinji na kusifu kuwa ni tamu bila kujua zimetokana na jasho la wakulima wao barani Afrika. Kama si korosho labda wamekula vinono vingine ambavyo asili yake ni mazao ya Afrika.

Lakini kwa upande mwingine, viongozi hawa wa Afrika wakiwa huko wameahidiwa kusaidiwa katika sekta ya kilimo ili kukabiliana na juhudi za Marekani na wana-G8 kukabili njaa duniani.

Suala la usalama wa chakula duniani limejadiliwa huko Camp David, kimsingi unapozungumzia suala la chakula bila shaka unamzungumzia mkulima. Lakini je, mkulima anayezungumzwa hapa ni kama yule wa Nanjilinji ambaye msaada husika utamfikia ili alime hekari nyingi zaidi za korosho na hatimaye apate mapato mengi zaidi na korosho zake zibanguliwe na kiwanda kitakachojengwa pale kijijini au wilayani kwake?

Au wakulima waliolengwa na ahadi za G8ni wawekezaji wakubwa watakaokuja nchini na kukatiwa hekari kadhaa, wakawekeza mtaji wa fedha na teknolojia na kuajiri wakulima wa Nanjilinji kama vibarua katika mashamba hayo?

Nauliza hivyo kwa sababu tumesikia mradi wa “usalama wa chakula duniani” utatekelezwa kwa kushirikisha sekta binafsi Tanzania, Ethiopia na Ghana. Je, ni nani hao kutoka sekta binafsi? Je, ni wawekezaji wakubwa pamoja na wakulima wadogo nchini au ni wakubwa peke yao na wadogo wageuzwe vibarua wao?

Haya ni maswali muhimu ili kupima manufaa ya uamuzi wa Camp David unavyowiana na unafuu anaopaswa kuutarajia mkulima wa Nanjilinji, moja ya vijiji masikini kabisa Tanzania lakini vyenye rasilimali ya korosho.

Kwa mtazamo wangu ili wanakijiji wa Nanjilinji na vijiji vingine nchini wafaidike na msaada wa aina hii katika sekta ya kilimo ni lazima kuwe na viwanda vya usindikaji mazao yao ambavyo ni fursa ya ajira kwa watoto wa wakulima.

Lakini pia namna bora ya uendeshaji wa kilimo kinachoweza kumkomboa Mtanzania si kuleta wawekezaji wa kigeni katika mashamba makubwa na kisha kuwageuza wakulima wetu wadogo wanaoendesha kilimo cha kujikimu kuwa vibarua wao.

Njia bora ya kushirikisha sekta binafsi ni kuleta wawekezaji wakubwa ambao wataingia ubia au mkataba wa namna fulani na wakulima wenyeji ili kuinua hali zao za maisha, kujenga uhusiano mwema kati ya wageni na wenyeji lakini pia kukusanya juhudi za pamoja kuelekea kilele cha mafanikio.

Sitaki kueleza mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima wenyeji uwe vipi kwa sababu hiyo ni kazi ya wanasheria na watalaamu wengine waliosomeshwa kwa kodi za wakulima ili hatimaye waisaidia nchi na watu wake.

Hata kama ujio wa wakulima wakubwa utasaidia kuondoa njaa nchini lakini tungependa kuona msaada wa G8 unawanaufaisha pia wakulima wadogo katika vijiji vya Tanzania na hii ndiyo kazi ya msingi ya Serikali. Serikali isijirahisishe kwa kuwanyenyekea wawekezaji wakubwa kutoka nchi za G8, bali ilinde maslahi yao kwa usawa na wakulima wetu wadogo.

Je, Kikwete alikwenda Camp David akiwakumbuka wakulima wa Nanjilinji na wenzao wa vijiji vingine nchini? Ni juu ya Kikwete na wenzake serikalini kuanza kutafakari na kutekeleza ndoto ya kuhamisha furaha waliyoikuta Camp David, Maryland na kuipandikiza katika nyuso za wakulima wetu nchini.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika


RAIA MWEMA

No comments: