Tuesday, May 22, 2012

HAWA NDIO MA-DC TUNAOWATAKA , WALA SIO MAKADA MASWAHIBA

UTEUZI huu wa wakuu wa wilaya (ma-DC) zaidi ya 130 uliofanyika wiki hii na Rais Jakaya Kikwete umeonekana kuwa na dosari kadhaa.

Hadi sasa zimetolewa sababu nyingi au mbalimbali ambazo baadhi yake zinaweza kukubalika na kuwa na mantiki na nyingine ambazo zinaweza kuwa zaidi za kisiasa tu.

Binafsi, sitaki kusimama au kuunga mkono mojawapo katiya makundi mawili au zaidi kati ya hayo, yaani yale yanayoukubali uteuzi huo wa Rais Kikwete ambao umetangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Sipo pia upande wa watani wao wa kisiasa (yaani wapinzani) na ndiyo maana mimi kwa hili ninajisoza pembeni ili niweze kusema hiki ninachokitaka.

Lakini, ninapata ujasiri wa kuanza kwa kuwapongeza wateule wote wa U-DC kwa kukabidhiwa majukumu hayo ambayo naamini ni mazito mno kuliko pengine wengi wanavyofikiria kwa sasa kuhusu DC wa sasa na wajibu wake katika wilaya.

Pia, ninapenda kuwapongeza zaidi wanahabari wenzangu kadhaa ambao Rais Kikwete au JK kama anavyoitwa na wengi ambao amewaamini, kisha kuwakabidhi kazi hii nzito ya kuongoza wilaya, ingawa si mara yake ya kwanza kwa JK kufanya hivi kwa kundi hili.

Tayari, tunao hata magavana wa mikoa (RC) ambao pia ni wanahabari na ambao sijasikia kwamba wameshindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo!

Huu ni ushahidi mwingine kwamba kuwa na ujuzi wa kukusanya, kuandika au kutangaza habari kamwe hakuwezi kumzuia mtu au mwanahabari kuongoza jamii na kwamba dhana potofu iliyojengeka miaka nenda rudi kuwa wanahabari wa Tanzania si weledi, haina mashiko tena.

Ushahidi wa karibuni ni jinsi ambavyo mwanahabari mwenzetu, Benjamin William Mkapa alivyoweza kuiongoza Tanzania kwa miaka 10, akaweka nidhamu ya kweli ya watu kulipa kodi, kiasi kwamba aliitwa na wengi kuwa bwana kodi.

Mkapa, alifika mahali hataakaitwa mtu mbaya, yaani yule ambaye aliikausha mifuko ya wengi kwa ukosefu wa fedha kwani shilingi ilipotea katika mifuko ya Watanzania walio wengi wakiwamo wafanyabiashara, wachuuzi na wengineo ambao walikuwa ama wamekuzwa au kulelewa katika mazingira ya kutowajibika na kisha kusahau kwamba kulipa kodi ni wajibu na ndiyo msingi wa maendeleo katika nchi yoyote.

Baada ya kuondoka madarakani kwa bwana kodi mwaka 2005, tunasikia vilio siku hizi kwamba hata Serikali haina fedha za kulipa mishahara kwa wakati, tunamkumbuka Mkapa ambaye aliweka kila tarehe 25 ya mwezi kuwa ya malipo ya mishahara.

Tunasikia kwanba hata makusanyo ya kodi ambayo yanafanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) yamepungua, ingawa wao wanadai kuwa yameongezeka!

Inashangaza kuona kwamba mbali ya mishahara ya watumishi, leseni za wafanyabiashara, ingawa si wote, kodi katika vinywaji kama bia, soda na sigara, ndivyo vyanzo vikuu vya mapato ya nchi yetu, hakuna vingine vipya.

Ni ajabu kwamba TRA imesahau kubuni mbinu kama za kushirikiana na mamlaka kama za serikali za mitaa, vijiji hadi wilaya katika kutoza kodi kwa wachuuzi (wamachinga) ambao ni wengi mitaani mwetu na wao wamekuwa sikuzote wakikimbizana na askari polisi au mgambo katika miji yetu, huku bidhaa zao ama zikipotea, kutaifikishwa na nyingine nyingi kuharibiwa!

Matokeo yake, walipa kodi tumebaki wachache, wengi wetu ni wale ambao kipato chetu ni cha dirishani, kwa maana kwamba waajiri wanabanwa na sheria, kiasi kwamba ile Pay As You Earn (PAYE) imegeuka kuwa kitanzi, kilio chetu watumishi tulio wengi iwe wa sekta ya umma au binafsi, ingawa Watanzania wenzetu ambao wanadai huduma wanaishi raha mustarehe, bila kodi, kwa ufupi wanapeta!

Itakumbukwa kwamba hata kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), pamoja na mambo mengine ilizungumzia kitanzi hiki kwa mtumishi aliyeko katika ajira ambaye anateswa na mfumo huu wa PAYE, lakini inaelekea kuwa Serikali haina masikio tena.

Nikiachana na hili la usikivu wa Serikali, nizungumzie mategemeo mapya kwenye majukumu ya wakuu wa wilaya ninaowaita wa karne ya 21, ambao JK amewateua.

Kama ilivyokuwa wakati JK alipoingia madarakani mwaka 2005, tumeambiwa kwamba nao watapewa kwanza darasakule Dodoma, jambo ambalo ninaliafiki, ingawa kwa tahadhari.

JK alianza kazi kwa kuendesha semina elekezi kwa mawaziri na wasaidizi wao, kule Ngurdoto, Arusha lakini kwa miaka saba wengi hatuoni ni kitu gani kipya walichojifunza au kufundishwa na ambacho wamekiishi na ambacho kina tija kwa Watanzania.

Matokeo yake, ndiyo maana kilio kile kile cha ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi, kutowajibika kimeendelea kuitesa Serikali ya JK, ambaye wiki mbili zilizopita amebadili baraza la mawaziri na kuwatupa nje baadhi ya wateulewake aliowapa darasa kule Ngurdoto.

Nakumbuka darasa lile lilifanyika pia kwa makatibu wakuu na wakurugenzi katika hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam muda mfupi baadaye, lakini nao pia wameshindwa!

Hivyo, linapokuja suala hili la uteuzi na majukumu ya ma-DC, ninashawishika kuanza kwa kuwapa wosia na angalizo kwamba nao wasijisahau, wakumbuke kwamba wamepewa majukumu wakati nchi yetu ikiwa katika hali mbaya kiuchumi, haina pa kushika!

Ndiyo maana ninalazimika kumshauri JK na hata Mwana wa Mkulima (Mizengo Pinda), ambaye ndiye msimamizi mkuu kwamba tuna mategemeo mengi kwama-DC.

Mojawapo ya mategemeo yetu kwa walio wengi, ni uwezo wao wa kuwa wabunifu, kusaidiana kwa karibu na wakurugenzi watendaji ili kuhakikisha nchi, kwa maana ya kuanzia wilaya zao, inapiga hatua kimaendeleo kuliko wakati huu ambao kilio ni kuzidi kudorora kwa uzalishaji, maendeleo ya mtu mmoja mmoja au jamii kwa ujumla wake.

Ninashauri kila DC akipewa hadidu za rejea, awekewe malengo ya kazi ambazo zinatarajiwa kufanyika katika wilaya yake na endapo atashindwa kuyatimiza, basi aongoze au kuwa wa kwanza kujiuzulu.

Sidhani kwamba wakuu wa wilaya 133 wanatakiwa kupewamajukumu yaliyo sawa au yenye kufanana, kwani kijiografia Tanzania imetofautiana na hivyo kila DC apewe wajibu na jukumu linalofanana na wilaya aueneo lake.
Hili ni jukumu la msingi na pengine la kwanza ambalo kila DC mteule au yule ambaye amebahatika kubakia baada ya chekecheo lile la JK na wasaidizi wake, ajiangalie upya.

Ajipime, kwamba je, ataweza kuwaongoza wananchi katika wilaya ile kuondokana na maadui wakuu watatu, yaani, umaskini, ujinga, maradhi, ambao wamepigwa vita isiyokwisha tangu nchi yetu ipate uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita?

Mbali ya jukumu lile la msingi la kisiasa la kumfanya DC awe mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakati huu wa amani, utulivu katika nchi yetu, hauna budi kuangaliwa upya.

Ninadhani kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), chini ya Dada Hawa Ghasia itachangamka, kubadili pia mtazamo wake, mwelekeo na hata majukumu ya wakuu wa sasa wa wilaya, ili waishi kweli kama wale wa karne ya 21!

Mbali ya hilo, kila DC akabidhiwe jukumu la kuongoza wataalam waliomo katika wilaya kubuni, kusimamia kikamilifu harakati kama za kilimo cha kisasa, umwagiliaji, kuuza mazao yaliyosindikwa, kwa maana ya kusaka masoko, kusindika mazao kule kule katika maeneo yao.

Kwa mfano, mahindi yanazalishwa kule Rukwa, Mbeya, Ruvuma,maweseyaKigoma, karanga na ufuta ya Dodoma au Singida, kahawa ipo Kagera, Kilimanjaro, Mbinga lakini yote yakivunwa yanasafirishwa kama malighafi hadi Dar es Salaam.

Yakifikishwa hukoama yakasagwe na kuwa nafaka au yasindikwe au kukamuliwa kuwa mafuta, tena kwa gharama kubwa.

Usishangae kwamba kisha yatasafirishwa kwa gharama kubwa zaidi na kurejeshwa kule kwa wakulima na kuuzwa kwa bei mbaya, huku viongozi wetu, yaani ma-DC na wakuu wao mikoa (ma-RC) wapo kimya!

Ninadhani kwamba sasa kuwa DC usiwe mzaha, bali kazi ambayo itatendwa, kupimwa matokeo na anayeshindwa aondoke mwenyewe!


MWANANCHI

No comments: