Monday, May 7, 2012

DK. KITINE: VIONGOZI WENGI NI WEZI


Elias Msuya
 
SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kupangua Baraza la mawaziri, viongozi wa wastaafu wa Serikali Dk Hassy Kitine na Balozi Dk Ahmed Kiwanuka wamesema hali hiyo inasabishwa na kushuka kwa maadili viongozi na kwamba mawaziri wengi ni wezi. 

Wakizungumza katika kipindi cha ‘Je, Tutafika’ kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten cha Dar es Salaam juzi usiku, viongozi hao walisema kuwa viongozi wa Serikali ya sasa wanatumikia mabwana wawili kinyume na iliyokuwa miiko ya viongozi ya Azimio la Arusha.

“Ndiyo mawaziri hawa wamemetajwa kuhusika na ubadhirifu, lakini wapo wengine ni wezi tu, wezi tu….kuna waziri mmoja kapewa hela za nchi, kaenda sijui huko Comoro kapeleka hela huko. Wengine sisi tunajua, eeh kapeleka hela huko, naambiwa sasa anajenga hoteli makao makuu ya mkoa mmoja wa Kusini. Sasa wewe hizo hela umezipata wapi? Na si yeye tu wapo wengi, wezi tu,” alisema Dk Kitine na kuongeza: 

“Tatizo kubwa ni pale tulipoua azimio la Arusha, watu wanasema kuwa tuliweka Azimio la Zanzibar, hakuna azimio la Zanzibar. Kama alivyosema mwenzangu, huwezi kutumikia mabwana wawili. Uongozi na pesa, utakwenda kwenye pesa zaidi, huwezi kuwa na muda wa kuongoza, kwasababu pesa zinavutia zaidi.”
Akifafanua jinsi Mwalimu Nyerere alivyokuwa akiteua Baraza lake la mawaziri, Dk Kitine aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, alitaja mambo matatu yaliyozingatiwa.
“Kwanza alikuwa anaangalia uzalendo. Pili, uwezo kwanza awe amesoma japo kidogo. Ndiyo,  kuna watu walikuwa hawajasoma lakini walikuwa na uwezo.
Kigezo cha tatu ambacho ndiyo kikubwa zaidi, alikuwa anaangalia kama mtu atakayeteuliwa atafanya kazi kwa uadilifu? Kwa hiyo lazima awe mzalendo, awe na uwezo lakini pia awe mwadilifu. Mambo yote anayofanya ni kuwasaidia Watanzania.” alisema Dk Kitine.
Hata hivyo Dk Kitine huku aliwataja baadhi ya mawaziri wa sasa na waliopita, alisema siyo mawaziri wote wenye tabia chafu.
“Lakini nasema wako wafanyakazi waadilifu. Kwa sababu kuna watu wanaofanya vizuri na Watanzania wanajua.Kwa mfano yuko Gideon Cheyo alifanya vizuri, alikuwa Mbunge wa Ileje. Akabadilishwa akawekwa Chiligati halafu akatoka akawekwa yule mama naye ni ngangari, Profesa Tibaijuka. Katika Wizara zenye rushwa nchini ni Wizara ya Ardhi, kuna uchafu mwingi kweli kweli,” alisema.
Naye Balozi Kiwanuka alisema kuwa kubadilishwa kwa Baraza la mawaziri mara kwa mara kunatokana na viongozi hao kutumikia mabwana wawili. 

“Siku hizi mambo yamebadilika. Viongozi wetu wamo kwenye biashara, wamo kwenye kutuongoza, wao wanajua wanavyotekeleza wajibu wao kote kote, lakini ni ngumu na matatizo haya yanayojitokeza ni matokeo ya vurumai hizi,” alisema Balozi Kiwanuka na kuongeza,
“Huwezi ukawatumikia mabwana wawili, ni ngumu, unachagua nitafanya hili, nitaacha hili. 
Mambo haya yanayotokea ni kama kukiuka maadili kwa viongozi”. 

Aliongeza kuwa wakati wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na utaratibu maalum wa kuwapata viongozi tofauti na sasa ambapo maadili yameshuka.
Alitoa mfano wa utawala wa wakoloni wa Uingereza akisema kuwa wakati huo hata magavana hawakuruhusiwa kufanya biashara.
“Kwa, mfano tulitawaliwa na Waingereza, huwezi kuteuliwa kuwa gavana halafu uje kufanya biashara nyingine. Hawakutoi Uingereza uje kuwa na kampuni kwenda kuwinda nje.
Malkia alisema ukitaka kuwinda niachie ugavana wangu, ukitaka kulima, mashamba makubwa tutakupa, lakini ugavana tuachie. Huwezi ukafanya yote,” alisema Balozi Kiwanuka.
Kuhusu umasikini unaoikumba nchi, Balozi Kiwanuka alisema ni aibu  Kwa sababu zipo rasilimali nyingi zinazotuzunguka.
“Umasikini wetu kwa miaka 50 iliyopita tumejitahidi kupambana nao, ungelitegemea kwamba mipango yetu ya kuimarisha maendeleo ya watu wetu. Na hii ni aibu sisi ni watu tulio huru, tunafundisha watu wetu, unashindwa kuelewa kwa nini mambo haya yanatokea sasa hivi. Inatisha kabisa,” alisema.

Balozi Kiwanuka ambaye amekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu na kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubalozi na ukuu wa mkoa, alitoa pia mifano ya nchi za Ulaya na Marekani akisema kuwa watu wanapopewa uongozi wa umma hutakiwa kuacha kazi zao binafsi.
“Labda nichokoze jambo moja, uongozi unahitaji uadilifu wa hali ya juu. Mimi nimepata bahati ya kusoma Ulaya na Marekani na nimewasomasoma hawa jamaa, ukiwa kiongozi, hata kama umeacha shughuli zako binafsi, kwa mfano wewe ni mlevi na wenzako wamethibitisha, kuwa huyu kiongozi wetu mara kwa mara yuko bar? Watakutoa. Au wanakuona mitaani na mabinti,” alisema.


MWANANCHI

No comments: