Friday, May 4, 2012

CHADEMA WANA WANANCHI CCM INA DOLA
Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,

SIPENDI na sitaki kujaribu kumhusisha Mungu na chama kimoja cha kisiasa. Na sipendi zaidi kusikia kuwa kuna watu wanaamini kuwa Mungu yuko nao zaidi kwenye siasa kuliko wengine.

Ninachozungumzia ni vile dhamiri yangu imekataa kuitikia kauli kuwa “tulianza na Mungu na tutamaliza na Mungu”.

Kwa kufuatilia mwamko wa kisiasa nchini ambao umedumu kwa miaka sasa na ambao kwa maoni yangu unazidi kujikita, mpaka uliochorwa sasa hivi kati ya CHADEMA na CCM ni kuwa CHADEMA kina wananchi na CCM ina dola! Mungu ni wetu sote!

Hatari kubwa ya kumhusisha Mungu na chama cha siasa ni kuwa tunaweza kutengeneza kikundi cha watu ambacho kinaweza kujiaminisha kuwa kimeteuliwa ili kije kututawala na hivyo kukipinga, kukisoa au kutokubaliana nacho ni sawasawa na kutokubaliana na mapenzi ya Mungu. Hili ni jambo la hatari.

Hatari yake inakuwa kubwa zaidi pale ambapo maamuzi ya kisiasa yanapoweza kupendekezwa na kusukumizwa kwa wananchi kama maamuzi ya Mungu au yanayotokana na mapenzi ya Mungu.

Ndugu zangu, Mungu hana sera! Mungu hana sera ya miundombinu, ya ulinzi, ya maji au ya nishati! Mungu hatungi sheria na kwa hakika kabisa Mungu hapigi kura! Wanaofanya haya yote ni sisi wanadamu katika unyonge na umaarufu wetu na kwa hakika katika udhaifu wetu na nguvu zetu. Maamuzi tunayochukua au kuyasimamia ni yetu sisi, si ya Mungu!

Ni muhimu kulielewa hili na kulikubali kwani kinyume cha hapo tunaweza kujikuta tunashindwa kuwawajibisha watu hasa kama tunaamini ni “Mungu” ndiye aliyewaongoza na baadaye tukagundua kuwa waliyoyafanya yana makosa!

CHADEMA, kama vyama vingine nchini, kimeanzishwa na wanadamu na kinaundwa na wanadamu. Sikumbuki kama kuna malaika alikuja na kuwapa watu mwanga wa jinsi ya kuanzisha chama na kuwapatia katiba, ilani na sheria zao!

Ni watu walikaa na kuamua kuanzisha chama na ushahidi kuwa ni chama cha wanadamu CHADEMA kimekuwa kikifanya mabadiliko mbalimbali kuendana na muda na nyakati.

Lakini kuna jambo jingine muhimu la kuliangalia katika hili kwani naamini ni kweli zaidi. CHADEMA kinaendelea kukubaliwa na wananchi zaidi huku CCM watu wakikikimbia.

Matokeo ya uchaguzi ya 2010 yanaonyesha pasipo shaka kuwa CHADEMA ndicho chama ambacho kinakubalika zaidi na wananchi na msingi wa hili ni kukubalika kwa ajenda yake.

Ajenda ya CHADEMA ni ya mabadiliko – na si mabadiliko tu ya juu juu bali mabadiliko yenye lengo la kuvunja vunja na kusambaratisha mifumo iliyoundwa kwa miaka 50 na CCM, mifumo ambayo imesimika ufisadi nchini, imelea kutokuwajibika na kubembeleza uzembe!

Ajenda hii imekubalika zaidi kuliko ajenda iliyozoeleka ya “tudumishe amani, umoja na mshikamano” wakati watu wanaishi katika dhuluma.

Msingi wa ajenda hii ya CHADEMA kusema ukweli ni wananchi wenyewe na si Mungu. Kabla ya uchaguzi wa 2010 na hasa kabla ya kujulikana kama CHADEMA itamsimamisha Dk. Slaa kama mgombea wake wa urais wananchi wengi walikuwa wanaiangalia CHADEMA kwa shuku, wasiwasi, na aina fulani ya woga.

Wengi walishaaminishwa kuwa cha CHADEMA ni chama cha Wakristu huku wengine wakiamini kuwa ni chama cha watu wa Kaskazini; wengine waliaminishwa tu kuwa ni chama cha wafanyabiashara huku wengine wakiaminishwa kuwa ni chama cha kupenda vurugu! Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi mkuu yamethibitisha pasi ya chembe ya shaka kuwa CHADEMA si sehemu ya hilo.

CHADEMA ilikubalika kuanzia Kaskazini hadi Kusini, Mashariki hadi Magharibi; kuanzia Hai hadi Mbozi, kutoka Meatu hadi Biharamulo, Mwanza hadi Arusha, Dar es Salaam hadi Kigoma. Kwa mara ya kwanza CHADEMA ilivunja na kuzitupilia mbali sifa zote mbaya za kuwa ni chama cha mahali, kabila au kikundi cha watu.

Watanzania walijikuta wanafunguliwa! Walifunguka na kutambua kuwa tumaini jipya kwa Tanzania ni CHADEMA na hili kwa kweli halikuhitaji mjumbe kutoka mbinguni kuja kuwaambia Watanzania. Wao wenyewe waliona, walitambua, na waliamua!

Lakini kukubalika kwa CHADEMA kwa kiasi ambacho tunakiona leo hii hakukubadilisha kitu kimoja – CCM ina dola! Chama cha Mapinduzi ndicho kilichounda serikali na ndicho sera zake zinaongoza nchi nzima na ni wao ndio wenye kusimamia serikali nzima. Ndio wanaoshilikia Ikulu, ndio wao wameunda baraza la mawaziri lililoshindwa na ndio wao waliojazana bungeni.

Ni wao ndio wanaweza kuzungumza na Polisi na polisi wakatetemeka! Kushikilia huku kwa dola ndiyo asili ya nguvu za CCM. Si kupendwa, si kukubalika, si sera zake, bali ni dola.

Sasa kushikilia dola kuna faida zake. Faida ya kwanza ambayo iko wazi ni kuwa ukiwa na dola unaweza kufanya lolote kwa yeyote bila kuulizwa. Kimsingi, serikali inaweza kutumiwa na wanasiasa kutekeleza mambo mbalimbali bila kuulizwa.

Tumeona Arumeru Mashariki, tumeona Mwanza, na tumeona Songea. Kuna katabia fulani kuwa serikali inaweza kufanya lolote . Fikiria tu kwa mbali kama wabunge waliocharazwa mapanga kule Mwanza wangekuwa ni wabunge maarufu wa CCM, na wanaotuhumiwa kufanya hivyo wakawa ni watu wenye kuhusiana na CHADEMA. Kila mtu anajua mwitikio ungekuwaje!

Faida moja nyingine ni kuwa huhitaji kutumia nguvu nyingi sana kushinda uchaguzi; unahitaji kutumia watu wako “kwenye system” kuhakikisha ushindi unakuja. Sote tunajua kwa kiasi kikubwa tu jinsi uchaguzi wa 2010 ulivyoendeshwa kiasi cha kutishia kabisa amani.

Tunajua nguvu iliyotumika – na ambayo bado tunaiona – kushinda uchaguzi kwa mbinde na kwa upinde. Sasa, chama tawala kwa kweli ndiye mnufaika mkuu wa kuwa na dola.

Lakini haya yote hayaondoi ukweli mkubwa zaidi na ninaamini wenye nguvu zaidi, kwamba CHADEMA wana wananchi. Hakuna nguvu yenye kuweza kuleta mabadiliko nchini kama kutambua kuwa wananchi ndio sauti ya mwisho na yenye nguvu zaidi.

Si polisi na nyota zao, si jeshi na vifaru vyao wala si watawala na vimulimuli vyao. Ni wananchi. Na hii ndiyo nguvu ambayo tunaiona sasa. Maneno ya CHADEMA ya “People’s Power” huwa yanatafsiriwa kuwa ni “nguvu ya umma” lakini kwa haki zaidi yana maanisha “nguvu ya wananchi”.

Sitaingia kwenye tofauti ya kimaneno (semantic difference) hapo ila ninachotaka watu waelewe ni kuwa nguvu ya wananchi haiko katika wingi wao (masses) bali iko katika uhuru wao kama binadamu.

Sitaki kuzama kwenye falsafa hapa zaidi, lakini ninachosema ni kuwa nguvu ya dhamira ya mwanadamu haijawahi kuzuiwa na dola yoyote. Dola inaweza kuzuia mwili wa mwanadamu kwa pingu na kuta za gereza lakini kamwe haiwezi kuweka gerezani fikra na dhamira ya mwanadamu.

Dola inaweza kumshtaki mwanadamu lakini haiwezi kuyatia hatiani mawazo yake! Sasa nguvu ya dola iko katika kulazimisha – kwa sheria, vyombo vya dola, au hata kwa matumizi ya nguvu.

Nguvu ya dhamira hata hivyo iko katika kukataa. Mwanadamu ana uwezo wa kukataa kitu hadi mauti! Ninaamini sasa hivi tunachoshuhudia ni kuwa wapo watu kati yetu waliovuka mpaka huu sasa hivi kiasi kwamba hawaigopi tena Serikali, hawajali CCM inasema nini na kwa hakika wanapuuzia kabisa vitisho kutoka kwa watawala. Hawa wameamua kuwa watii kwa dhamiri zao zaidi kuliko kitu kingine chochote.

CHADEMA basi isichezee wala kuchukulia kiurahisi wakati wake huu wa kupendwa na wananchi. Isije kujidanganya kuwa itaendelea kupendwa vyovyote vile. Viongozi wake wasije kujivika kilemba cha ukoka wakiamini kuwa wanapendwa kwa sababu wao ni vijana, wanazungumza vizuri, wanavaa magwanda vizuri n.k.

Wajue kabisa wanapendwa kwa sababu watu wameamua kuikataa CCM “na mambo yake yote”. CHADEMA hawawezi kudai kuwa ni haki yao kupendwa au kuungwa mkono kwani historia ina mafunzo mazuri kweli – si hoja mtawala anapendwa vipi, siku moja anaweza kuchukiwa.

TANU chama kilichotuongoza kufikia uhuru na ambacho ndicho mtangulizi wa CCM kiliishi katika uhai wake wote kikipendwa na wananchi. Kutoka vijijini na mijini TANU ilikuwa ni zaidi ya chama cha kisiasa; kilikuwa ni chama chetu. Watu walijitolea kwa kila namna kukisaidia – kwa wazi na wengine kwa vificho.

Walijitokeza watu wengi ambao walitumia rasilimali na vipaji vyao kukisaidia kushinda na wengine historia iliwasahau kweli kweli. Hata hivyo, kama sote tunavyojua kilipogeuka na kuwa CCM bado kilipendwa sana na wapo watu ambao hata leo hii wanaiona CCM kama mama yao yaani hata kuwazia vibaya hawawezi.

Lakini tunafahamu kuwa hata watu waliokuwa ni wana CCM mashuhuri nao wameanza kuikataa CCM na kwa kadiri siku zinavyokwenda ndivyo watu wanavyozidi kufunguliwa na kuikataa CCM. Kama CCM iliyowahi kupendwa leo inakataliwa, CHADEMA kisije kujidhania kuwa kitapendwa daima.

Kwa kadiri CHADEMA kitakavyoendelea kusimamia haki, kupiga vita ufisadi na kujitahidi kulazimisha mabadiliko nchini – iwe ndani ya madaraka au nje yake – kitaendelea kuungwa mkono.

Lakini siku kitakapogeuka chama “teule” na kuanza kujifikiria kina upendeleo wa pekee wa Mungu basi kitakataliwa. Kwani, watu watakuja kukipima na kuona nacho kimepunguka.

Ninachosema ni kile kilichowahi kusemwa na watu wengine – kila mtu na lwake ila Mungu ni wetu sote. CHADEMA wana wananchi, CCM ina dola! Mara zote – hata baada ya maumivu makali – wananchi hushinda na dola husalimu amri mbele ya wananchi


RAIA MWEMA

No comments: