Monday, April 2, 2012

SAUTI PEKEE WATAWALA HUISIKIA NI KURANa Lula Wa Ndali Mwana Nzela,

WAPO wananchi wanaofikiria kuwa watawala wanasikia lugha ya maneno. Kwamba, ukitaka viongozi wa chama tawala wakusikilize basi ni lazima uandike barua ndefu, uwatafute na kuwabembeleza au utafute mtu wa “kukuunganisha” na kiongozi ili waweze kukusikiliza.

Wapo na wengine ambao wanafikiria watawala wanasikia lugha ya kuzomewa, kushangiliwa au kupigiwa makofi. Ndugu zangu, kwenye nchi ya kidemokrasia lugha pekee ambayo watawala husikia ni lugha ya kura.

Kura katika demokrasia ni lugha ambayo inasemwa na mtu mmoja mmoja lakini kwa pamoja. Watu wanaweza kupinga jambo au kuunga mkono jambo lakini njia pekee ya kujua ni kwa kiasi gani wanapinga au kuunga mkono jambo hilo ni kuwauliza na kuwapa uchaguzi. Watu ambao kweli wanajua wanachokitaka basi watachagua kile wanachokitaka.

Uandikishaji wapiga kura ni kuuliza nani anataka kuzungumza

Lengo la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wowote ule ni kutaka kujua mtu gani mzima anataka kuzungumza na kuwaambia watawala kitu. Ndio maana sisi wengine tunaamini mfumo wa Tume ya Uchaguzi wa kuandikisha wapiga kura ulivyo sasa ni kinyume cha Katiba kwani inawanyima maelfu ya watu nafasi ya kuzungumza. Kwa mfano, inashangaza kwa nini daftari la wapiga kura haliboreshwi karibu kila mwezi ili kupata watu wote ambao wanatimiza vigezo vya kupiga kura.

Kwa mfano, kwenye uchaguzi unaofanyika wiki hii maelfu ya watu hawatoweza kupiga kura kwa sababu majina yao hayamo kwenye daftari la wapiga kura kama lilivyokuwa 2010. Watu wote waliotimiza miaka 18 tangu Oktoba 31, 2010 hadi Machi 31, mwaka huu hawatopiga kura hata kama wanasifa zote za kupiga kura.

Watu waliohamia katika maeneo mbalimbali yatakayopiga kura au ambao hawakujiandikisha 2010 hawaruhusiwi kupiga kura. Kwa maneno mengine hawa wote wamekatazwa kuzungumza na kuwaambia watawala wanachotaka kuwaambia.

Mojawapo ya vitu ambavyo vinanishangaza sana ni ukiritimba usio wa lazima wa uandikishaji wapiga kura. Kwa nini kwa mfano, ni Tume ya Uchaguzi tu ndiyo iwe na jukumu la kuandikisha wapiga kura? Hivi ni kweli pamoja na watu wote wenye akili na wasomi tumeshindwa kubuni mfumo mzuri wa kisasa wa kuhakikisha daftari la wapiga kura linaboresha mara kwa mara ili kulifanya liwe linaendana na wakati (current)?

Kwa mfano, kwa nini posta zisitumike kuandikishia wapiga kura? Wapo watu wengi ambao huenda kupata huduma posta kwa nini kusiwe na nafasi ya mtu kujiandikisha pale pale posta alimradi anavyovitambulisho vyote halafu ofisi ya posta inatuma taarifa hizo zote (kwa mtandao wa kielectroniki) kwenda Tume ya Uchaguzi na kuwapatia taarifa zilizopatikana? Posta ni mojawapo ya ofisi ambazo zimeenea sana nchini na zinaweza kabisa kutumiwa kufanya kazi hiyo?

Au kwa nini ofisi za Halmashauri ya Miji, Manispaa na majiji zisitumike kuandikisha wapiga kura? Nchini Marekani kwa mfano, kujiandikisha kupiga kura hakufanywi na tume ya taifa ya uchaguzi bali karibu kila mji una utaratibu wa kuandikisha wapiga kura wake.

Unapohamia kwenye mji wowote ukishapata tu kitambulisho chako cha ukazi ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi ya mji ule inakutumia fomu yako kujaza kama unataka kupiga kura katika mji ule.

Sasa yawezekana tusiweze kuwa na mfumo kama huo lakini ni kweli hatuwezi kufikiria namna ya kushirikisha halmashauri hizi ambazo zimeenea kila sehemu ya nchi katika kuandikisha wapiga kura? Ni kweli kabisa Serikali nzima haina watu wenye kuweza kufikiria mtindo na mfumo rahisi, wa haraka na bora wa kuandikisha wapiga kura?

Leo hii kwa mfano tunatumia simu za mkononi kufanya mambo mengi sana na yakakubalika; je tumeshindwa kabisa kutumia mfumo huo kuweza kujiandikisha kupiga kura? Kwa mfano, japo inaweza kuwa ngumu kukamilisha taratibu zote za uandikishaji upigaji kura kwa njia ya simu lakini je haiwezekani kuanza na kukamilisha baadaye?

Kwa mfano, mtu anaweza kutuma taarifa zake muhimu kasoro picha na sahihi yake tu – vitu ambavyo angeweza kuvipeleka kwenye ofisi ya halmashauri au tume au hata Posta vikachukuliwa na kuunganisha na taarifa zake za awali ambazo zitakuwa tayari zinapatikana kwenye mtandao?

Kuuza shahada au kupoteza shahada ni kujinyima haki

Mtu anayeuza shahada yake ya kupiga kura ni mtumwa! Amekubali kunyamazishwa; ni sawa na mtu ambaye kwa hiari yake mwenyewe amekubali kufungwa kitambaa mdomoni asiseme kitu. Kukubali kuuza shahada ya kupigia kura ni kukubali kuwa mnyonge na dhaifu; ni kukubali kuendekeza njaa ya kitambo na utumwa wa kudumu.

Mtu ambaye kwa hiari yake hajali cheti chake cha kupigia kura kiko wapi au hajali kama anacho ni sawa sawa na mtu ambaye anajua anakandamizwa na kuonewa lakini akiambiwa asimame kuelezea juu ya ukandamizaji huu anasimama huku hana la kusema. Ni kama mtu aliyepoteza sauti yake na anasimama akizungumza kwa ishara tu zisizoeleweka na kuonekana kama mchekeshaji.

Ni kwa sababu hiyo siku hizi tatu zilizobakia sehemu zote ambazo zinafanyika uchaguzi wapiga kura ni lazima wajiulize kwanza kama wanavyovitambulisho vyao na kama majina yao yanatokea kwenye orodha ya wapiga kura. Kama mtu ana kitambulisho chake asikubali kabisa kukataliwa kupiga kura hata kama ikibidi kusababisha ugomvi.

Kitambulisho chako cha kupigia kura ni kibali chako cha kupiga kura. Hakuna mtu – hajalishi kama ana nyota mabegani – anayeweza kukuzuia kupiga kura. Kama jina lako lipo na unachokitambulisho kutokupiga kura ni kudharau haki yako.

Wananchi wetu wanapopiga kura wajue kabisa wanatumia haki yao ya kuwaambia watawala kile wanachokitaka au wasichokitaka. Wasiogope, wasitishwe na wakishasema wanachotaka kusema ni lazima wahakikishe hakichakachuliwi au kuvurugwa.


RAIA MWEMA

No comments: