Thursday, April 12, 2012

MUDA WAYOYOMA BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU KILIMANJARO.
  • Lazidi kupungua ukubwa mwaka hadi mwaka
  • Ni matokeo ya uharibifu mkubwa wa mazingira
  • Wakati wowote uzalishaji umeme utasitishwa


Na Johnson Mbwambo,

HAMZA Sadik hana raha. Akiwa ofisa wa maji wa Ofisi ya Maji ya Bonde la Mto Pangani (Pangani Basin Water Office – PBWO), kitu kimoja kinatawala fikra zake: Hali itakuaje kama mvua za masika mkoa wa Kilimanjaro hazitanyesha kwa kiwango kinachotarajiwa?

Kwa miaka mitatu mfululizo, mkoa huo umekosa mvua za kutosha za masika. Na sasa Hamza Sadik anawaza hali ya Bwawa la Nyumba ya Mungu, wilayani Mwanga, itakuaje kama safari hii pia mvua za masika hazitanyesha kiasi cha kutosha.

Akizungumza na ujumbe wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), ofisini kwake, mjini Moshi, hivi karibuni, Sadik alisema ya kuwa, hali ya sasa ya maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu inasikitisha.

Kwa mujibu wa maelezo yake, kina cha maji cha bwawa la Nyumba ya Mungu hadi kufikia Machi 19, 2012, kilikuwa mita 682.37 juu ya usawa wa bahari.

Kina hicho kipo chini ya usawa wa chini unaoruhusiwa kwa uzalishaji umeme (mita 683.35) kwa mita 0.98. Na hapo ndipo lilipo tatizo la Sadik: Je, PBWO ishauri uzalishaji umeme usimame au iachie hali hiyo iendelee kwa matumaini kwamba mvua za masika zitanyesha kwa wingi karibuni?

Sababu kubwa ya kina cha bwawa kuwa chini kiasi hicho ni ukame uliosababishwa na uhaba wa mvua; hususan mvua za vuli za mwaka 2011 ambazo hazikuwa nyingi katika maeneo ya upande wa juu wa bwawa la Nyumba ya Mungu.

Lakini wakati bwawa hilo likikosa maji ya mvua, na hivyo kuzidi kuwa dogo, maji yake yanaendelea kutolewa na kutumika kwa mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzalishaji umeme, kilimo cha umwagiliaji, mifugo na matumizi ya nyumbani kwa wananchi wa maeneo ya chini ya bwawa.

Takwimu za PBWO zinaonyesha kuwa kiasi cha maji kinachoingia bwawani (inflow); hususan kutoka mito yake tegemeo kama Kikuletwa na Ruvu, ni kidogo kuliko kile kinachotolewa (outflow) .

Kwa mfano, wastani wa maji yaliyoingia katika bwawa la Nyumba ya Mungu kati ya mwezi Januari na Machi 2012, ni chini ya mita 10.5 za ujazo kwa sekunde wakati kiasi kinachotolewa ni wastani wa mita za ujazo 15 kwa sekunde!

PBWO, ambayo ndio yenye mamlaka ya kusimamia raslimali maji katika Bonde la Mto Pangani, inasita kupunguza kiasi hicho cha maji kinachotolewa katika bwawa la Nyumba ya Mungu kwa sababu mbili kubwa.

Kwanza, kupunguzwa huko kutasababisha kusimamishwa kwa uzalishaji umeme katika vituo vitatu vya uzalishaji umeme nchini vya Nyumba ya Mungu, Hale na Pangani. Vituo hivyo, kimsingi, vinatumika kuimarisha gridi ya taifa ya umeme.

Uamuzi unakuwa mgumu; hasa katika kipindi hiki ambacho uzalishaji umeme, hivi sasa, nchini unategemea zaidi umeme wa mabwawa baada ya ule wa majenereta kusimamishwa na wenyewe kutokana na kucheleweshewa malipo na serikali.

Pili, upunguzaji kiasi cha maji kinachotolewa katika bwawa la Nyumba ya Mungu kutasababisha upungufu wa maji kwa matumizi ya nyumbani kwa watu wa maeneo ya uwanda wa chini (ambao ni makame) ya wilaya za Mwanga, Simanjiro na Same ikiwa pia ni pamoja na kukwamisha shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo hayo.

Katika mazingira hayo, PWBO imebakiwa na mikakati miwili tu mikubwa ya kusaidia kulinusuru bwawa la Nyumba ya Mungu.

Kwanza ni kuwahamasisha na kuwashawishi watumia maji waliopo maeneo ya juu ya bwawa la Nyumba ya Mungu kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya maji.

Hili linakwenda sambamba na kuhamasisha wananchi kupanda mazao yanayohitaji maji kidogo, na pia kuepuka ulimaji karibu kabisa na vyanzo vya maji; hasa kwenye vijito vinavyoingiza maji yake katika mito ya Kikuletwa na Ruvu inayoingiza maji yake katika bwawa hilo.

Vijito vinavyoingiza maji yake katika mto Kikuletwa ni pamoja na Karanga, Weruweru, Kikavu na Sanya wakati vijito vinavyoingiza maji yake katika mto Ruvu (maarufu kama mto Pangani) ni Rau, Dehu na Mue.

Hakuna shaka kwamba kazi hii ni ngumu; hasa kutokana na ugumu wa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika kubadili tabia zao mbaya kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji.

Hata hivyo, kazi hii inaweza kufanywa kwa ufanisi kabisa kama kutakuwa na ushirikiano mkubwa kati ya wananchi, PWBO, Kituo cha Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro, Halmashauri za wilaya za Moshi Vijijini, Mwanga, Same na Simanjiro.

Mkakati mwingine ambao PWBO inautumia kusaidia kulinusu bwawa hilo ni kuhimiza matumizi ya vyanzo mbadala vya maji ikiwa ni pamoja na maji ya chini ya ardhi ambayo athari zake si za moja kwa moja kwa bwawa hilo.

Bwawa litanusurika kukauka kabisa?

Kwa tathmini ya haraka haraka ambayo JET iliifanya wakati wa ziara yake ya hivi karibuni katika wilaya za Moshi Mjini, Moshi Vijijini na Mwanga, bwawa la Nyumba ya Mungu linaweza kutoweka kabisa katika uso wa dunia baada ya miaka 10 kama uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea hivi sasa katika misitu ya vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro, hautakomeshwa.

Si siri kwamba mito na vijito vingi ambavyo ndiyo tegemeo la bwawa hilo huanzia au huimarikia kwenye misitu ya maeneo ya Mlima Kilimanjaro; na hivyo uharibifu wa mazingira wa maeneo hayo ndio pia kifo cha bwawa la Nyumba ya Mungu.

Na kama ilivyoelezwa, kwenye ukurasa huu, kwenye makala ya toleo lililopita, hali ya uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo imekuwa kubwa kiasi kwamba sasa mji wa Moshi tayari umeonja mgao wake wa kwanza wa maji katika kipindi cha miaka 20.

Hali hii ya kusinyaa kwa vijito vinavyoingiza maji katika mito miwili mikubwa inayotegemewa na bwawa hilo ya Kikuletwa na Ruvu imesababisha kusinyaa kwa mito hiyo miwili mikubwa, hali ambayo nayo imesababisha kusinyaa kwa bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo maji yake mengi ni kutoka katika mito hiyo miwili mikubwa.

Bwawa hili ambalo lilianza kujengwa kati ya mwaka 1965 hadi 1968 lilikuwa na ukubwa wa Kilomita za mraba 140 na mwambao au ufukwe wa Kilomita 37, lakini sasa limepungua mno kutoka katika ukubwa wake wa asili. Inakisiwa kuwa limepungua kwa theluthi mbili kutoka katika ukubwa wake wa asili.

Ingawa haujafanyika upimaji mpya rasmi kutambua ukubwa wa eneo ambalo bado lina maji, lakini hata kwa kutazama kwa macho tu inaonekana dhahiri jinsi bwawa lilivyosinyaa na kupungua ukubwa.

Kwa mfano, ujumbe wa JET ulipita katika vijiji kadhaa vya kata ya Lang’ata na kujionea eneo kubwa ambalo zamani lilikuwa sehemu ya bwawa la Nyumba ya Mungu likiwa na maji tele, lakini sasa likiwa kame kabisa baada ya maji kusogea mbele kabisa.

Lakini kiasi eneo la bwawa linavyozidi kuwa kame na maji kuzidi kusogea mbele zaidi; ndivyo pia wavuvi na wakulima wa vijiji hivyo wanavyoyafuata kuendesha shughuli zao kwa njia zisizo endelevu.

Ujumbe wa JET ulishuhudia mashamba ya mahindi pembezeni kabisa mwa bwawa, jambo ambalo zamani isingewezekana kutokana na sheria kusimamiwa vyema.

Hili la kilimo cha mahindi ndani ya eneo la bwawa lilithibitishwa hata na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Willy Joseph Njau, aliposema: “Watu wamejikatia maeneo ya kulima karibu kabisa na bwawa na kuyazungushia uzio wa miti. Huu ni uvunjaji sheria na tunaendelea kupambananao.”

Samaki nao sasa pia adimu

Madhumuni ya kujengwa bwawa hilo (1965 -1968) yalikuwa ni kuzalisha umeme, kuendesha kilimo cha umwagiliaji maji na pia uvuvi wa samaki. Kwa sasa, karibu shughuli zote hizo ni shaghalabagala kwa sababu ya ukubwa wa bwawa kuzidi kupungua na kusinyaa.

Mfano mzuri ni shughuli za uvuvi. Mara baada ya bwawa hilo kufunguliwa mwaka 1968, ni wavuvi wachache tu walioanza kuvua samaki kwa ajili ya kitoweo. Baadaye, uvuvi ukawa ni wa kibiashara zaidi baada ya wavuvi wengi kumiminika katika bwawa hilo kutoka Ziwa Jipe, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Rukwa, na hata wengine kutoka nchi jirani ya Kenya.

Idadi hii kubwa ya wavuvi katika bwawa ambalo linazidi kusinyaa mwaka hadi mwaka kwa sababu ya ukame, kumesababisha samaki pia wawe adimu. Zamani kulikuwa na aina saba ya samaki wanaopatikana ndani ya bwawa la Nyumba ya Mungu – Perege, Kambale, Kuyu, Ngogogo, Ningu, Dagaa na Mkunga, lakini sasa ni perege tu na kambale wanaopatikana ndani ya bwawa hilo – tena kwa uchache.

Na kwa sababu ya uchache huo wa samaki, wavuvi katika bwawa hilo sasa wameugeukia uvuvi haramu wa kutumia makokoro, vyandarua (tena vile vya dezo vya kampeni ya malaria), vimila na nyavu za macho madogo.

Ingawa Halmashauri ya Mwanga huendesha, mara moja moja, operesheni za kuwakamata wavuvi hao haramu, lakini mafanikio sio ya kujivunia ukilinganisha na ukubwa wa tatizo. Kwa mfano; kwa mwaka mzima wa 2011, ni makokoro 18 tu na vyandarua 23 tu vilivyokamatwa.

Tatizo kubwa, kama ambavyo JET iliweza kung’amua, ni uswahiba wa sirisiri kati ya wavuvi hao na viongozi wa baadhi ya vijiji vya uvuvi katika bwawa hilo. Viongozi hao wana kawaida ya kuwatonya mapema wavuvi hao juu ya operesheni za halmashauri kwa ‘malipo’ ya kupewa samaki wa bure!

Operesheni pekee kubwa iliyofanyika na kuwa na mafanikkio makubwa, ni ile ya mwaka 2007 iliyosimamiwa na aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, John Magufuli. Swali la kujiuliza: Kama Magufuli aliweza, kinamshinda nini waziri wa sasa?

Vyovyote vile, kuna ushahidi wa kutosha kuwa muda unayoyoma kwa bwawa la Nyumba ya Mungu. Kiasi mazingira yanavyoharibiwa katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro, ndivyo pia vyanzo vinavyoingiza maji katika bwawa la Nyumba ya Mungu vinavyozidi kukauka.

Ni dhahiri, hivyo basi, kwamba kama Serikali haitachachamaa kulinda mazingira ya Kilimanjaro, na kama haitachachamaa kuwadhibiti wavuvi na wakulima wanaoendesha shughuli zao ndani ya bwawa hilo kwa njia zisizo endelevu, itakuwa ni “bai bai” kwa bwawa la Nyumba ya Mungu mkoani Kilimanjaro.


RAIA MWEMA

No comments: