Thursday, April 5, 2012

MJADALA WA WAFANYABIASHARA WA UBUNGO NA MBUNGE WAO ( MH. MNYIKA)


Baadhi ya masuala na maswali ambayo wafanyabiashara ndogo ndogo wamenieleza au kuniuliza ni kwenye mkutano niliofanya na wajasiriamali hao zaidi ya 500 tarehe 04/04/2012:

Stella Mbuba-Yeye alieleza kuwa hawajakutana na serikali na kukubaliana maeneo mbadala kama inavyodaiwa kwenye vyombo vya habari. Anasema baada ya kusikia matangazo kwenye vyombo vya habari kuwa kuna maeneo mbadala wametengewa walikwenda kwa mtendaji tarehe 29 Machi 2012 lakini wakajibiwa kuwa ‘aliyewaleta eneo hilo ndiye atayewapeleka anakokujua na mkiendelea kuuliza tutawaitia polisi’.

Omari Cheka-Yeye anasema kwamba biashara ndogo ndogo katika eneo hilo zilipata baraka ya serikali kwa muda mrefu. Mvutano ulijitokeza tu pale wanaojiita ‘matembo’ walipoanza kufanya vitendo vya wizi na ubabe katika eneo hilo. Kufuatia hali hiyo mwezi Januari na Februari 2012 walikaa mikutano kati ya wafanyabiashara wote, serikali za mitaa na viongozi waandamizi wa jeshi la polisi na kuamua kuweka mfumo wa ulinzi shirikishi ili kulinda eneo husika. Katika mikutano hiyo walielezwa wazi waendelee na biashara kwenye eneo hilo kwa kuzingatia utaratibu waliopanga mpaka pale watakapopatiwa maeneo mbadala.

Mama Peter- Yeye anafafanua kwamba masoko yaliyotajwa wanayopaswa kwenda ya Shekilango na Mabibo tayari yamejaa wafanyabiashara wengine. Anasema kuwa sababu kuwa eneo hilo ni hatarishi ilipaswa pia kuhusu kituo cha mabasi ambacho kinamzunguko mkubwa zaidi wa watu siku nzima tofauti na biashara zao ndogondogo ambazo wamekuwa wakizifanya jioni mpaka usiku. Hivyo, hofu ya mitambo kulipuka haiwezi kuwa kwa wafanyabiashara ndogondogo bali hata kwa wananchi wengi wanaotumia kituo cha daladala mpaka sasa.

Rombo Mswaki-Yeye anaeleza kuwa baada ya kukubaliana na serikali na kuweka mfumo wa ulinzi na usafi walifanya pia zoezi la kuandikisha wafanyabiashara ndogo ndogo. Wakapata idadi ya wafanyabiashara waliokuwa na meza na walikuwa kila siku wanakaa na kufanya biashara ni 1440; hawa ni nje ya wafanyabiashara ndogo ndogo wanaoshika bidhaa mikononi. Wafanyabiashara wanachoomba ni kupatiwa eneo mbadala la kuendelea kujiajiri lenye kuwatosha na pia lenye ukaribu na wanunuzi.

Baada ya kuwasikiliza niliwajibu moja kwa moja kwamba siungi mkono biashara kufanyika katika maeneo hatarishi na maeneo yasiyoruhusiwa kisheria; niliwapa maelezo kuhusu chanzo cha matatizo yanayowakabili na kuwaeleza kwamba nipo tayari kuungana nao kuisimamia serikali katika kufanikisha yafuatayo:

Mosi; Tarehe 5 Aprili 2012 kila mmoja wao kwenda Manispaa ya Kinondoni saa 4 Asubuhi kufuatilia eneo mbadala ambalo manispaa imeahidi, kwa kwa maeneo yaliyotajwa yamejaa Manispaa ielekeze eneo ambalo imewatengea. Diwani wa kata husika pamoja na mimi mwenyewe tutawaongoza kufuatilia iwapo Manispaa haitatoa majibu ya msingi. Jimbo la Ubungo linayo maeneo katika eneo jirani na viwanda (Ubungo Industrial Area) ambalo lina baadhi ya viwanja wazi ama viwanda vilivyokufa baada ya kubinafsishwa kiholela; pamoja na mkakati wa ujumla wa kufufua na kuongeza viwanda serikali itekeleze mapendekezo niliyotoa kwa nyakati mbalimbali bungeni na kwa manispaa ya kutwaa au kununua sehemu ya maeneo hayo kwa ajili ya viwanda vidogodogo na biashara ndogondogo ili kuchangia katika ajira kwa vijana. Baada ya hatua hii tutaungana nao kufuatilia katika Mamlaka zingine mpaka kieleweke.

Pili; Nimetoa siku tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kueleza hatua walizochukua katika kutekeleza ahadi waliyoniahidi wakati wa vikao vya kamati ya nishati na madini nilipohoji kuhusu hatma ya wananchi wanaoishi na kufanya biashara katika maeneo hatarishi jirani na mitambo ya umeme Jimboni Ubungo. Ikumbukwe kwamba mwaka 2004 baada ya mitambo kulipuka serikali iliahidi kuwalipa fidia wananchi husika na kuwahamisha, mwaka 2009 Serikali ikarudia tena ahadi hiyo lakini mpaka sasa haijatekelezwa hata kwa mtu mmoja. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa hatua za haraka kuhusu suala hili mara baada ya kuchaguliwa niliendelea kufuatilia kwa njia mbalimbali za kibunge na kuanzisha pia mazungumzo kuhusu umuhimu wa Wizara na TANESCO kuchangia katika azma ya kununua eneo mbadala kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo kama sehemu ya mkakati endelevu wa kuwaondoa karibu na mitambo. Sehemu kubwa ya operesheni inayofanyika hivi sasa inagharamiwa na TANESCO, hivyo ikiwa shirika hilo lina fedha kwa ajili hiyo njia bora zaidi ni kizielekeza kwenye kuchangia ununuzi wa eneo mbadala kwa ajili ya wafanyabiashara na pia kulipa fidia kama ambavyo serikali iliahidi.

Tatu; nimetoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kueleza hatua iliyofikiwa katika kutekeleza ahadi yake ya aliyoitoa tarehe Oktoba 2010 wakati wa kampeni ya kujenga Machinga Complex nyingine tano; ili kuwe na maeneo ya namna hiyo ya biashara mawili kwenye kila manispaa. Kama serikali ingekuwa imetekeleza ahadi hiyo katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja toka Rais Kikwete aingie madarakani kungekuwa hivi sasa na eneo la wafanyabiashara ndogondogo zaidi ya elfu saba katika Jimbo la Ubungo. Ahadi hii ingeweza kutekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa kuwa Rais Kikwete alisema mwenyewe Oktoba 2010 kuwa tayari serikali ilikuwa imepata ufadhili wa bilioni 100 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo. Serikali inayokusanya kodi kwa wananchi wote ikiwemo wafanyabiashara ndogo ndogo inawajibu wa moja kwa moja kushughulikia chanzo cha mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati yake wafanyabiashara hao badala ya matokeo. Serikali inatumia nguvu kubwa kwenye kushughulikia vyanzo badala ya matokeo, kama nguvu hizo hizo zingetumika kushughulikia mafisadi wanaoua viwanda na kukosesha ajira kwa vijana au wanaohujumu ruzuku katika kilimo nchi ingepiga hatua kwa haraka zaidi. Hivyo, kusimamia utawala wa sheria kusiishie kwa wafanyabiashara ndogondogo bali nguvu kubwa hiyo itumike pia kuwaondoa katika maeneo yasiyoruhusiwa wafanyabiashara wakubwa ambao wengine wamepora viwanja vya wazi vya umma na wengine wamevamia maeneo ya hifadhi ya barabara.

Nne; Wafanyabiashara ndogondogo pamoja na kuungana nami katika kuisimamia serikali nimewaelekeza nao kwa upande wao waunganishe nguvu yao kutafuta eneo dogo ambalo wanaweza kulitumia wakati huu wa mpito tunaposhughulikia kupata eneo la kudumu. Wamekubali kuchangishana kufanikisha azma hiyo na tumekubaliana kwamba kwa hatua ambayo watakuwa wamefikia watujulishe kwa haraka na wengine ili tuweze kuchangia. Suala hili halihusu tu haki ya wafanyabiashara kujiajiri kwa kuuza bidhaa bali haki pia ya wananchi kupata bidhaa kwa urahisi ndio maana tunapaswa kuunganisha nguvu za pamoja kupata maeneo mbadala ya wafanyabiashara.

Tano; Nitaendelea kuungana na wafanyabiashara ndogondogo na wananchi kufuatilia masuala haya bila kujali kauli zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa kuwa ‘wanasiasa’ hawapaswi kuingilia masuala haya. Mkuu wa Mkoa amesahau kwamba na yeye ni mwanasiasa na hili ni suala la kisiasa linalohusu mgawanyo wa rasilimali za umma. Viongozi wa serikali wamesahau kwamba Mwalimu Nyerere alisema ili nchi iendelee inahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Nimekuwa nikifuatilia masuala haya kuanzia mwaka 2011 bungeni, jiji, mkoani na manispaa; yaliyojitokeza hivi sasa yatasaidia kuongeza msukumo wa hatua za haraka kuchukuliwa. Nitaendelea kufanya siasa safi katika suala hili kwa kuwa ndio kazi ambayo wananchi walinichagua kuifanya na sitaacha kuweka wazi pale wanasiasa au watendaji wa serikali wanapofanya siasa chafu za propaganda hewa bila kushughulikia masuala ya msingi yanayoyakabili makundi ya kijamii nchini na taifa kwa ujumla. Maslahi ya Umma Kwanza.


No comments: