Thursday, April 5, 2012

MANISPAA ITAFUTE MUAFAKA WA SAKATA LA WAFANYABIASHARA WA UBUNGO
Na Baraka Mfunguo,

Kwa wale ambao tunaifahamu vyema Ubungo ya miaka ya 80, kabla ya ujenzi wa Stendi ya daladala na hata ujenzi wa ofisi ya Tanesco ya makao makuu, tunafahamu vyema kwamba kulikuwa na soko kubwa la vyakula , mbogamboga, maduka ya nyama ambayo wakaazi waliozunguka eneo hilo na hata wale wa Chuo Kikuu walikuwa wakijipatia mahitaji yao madogo madogo.

Baada ya Ujenzi wa kituo cha mabasi ya daladala, achana na ile stendi ya mkoa ambayo pia ilikuwa Depo ya UDA na serikali ikaamua kubadilisha matumizi yake kwani stendi ya mabasi ilikuwa ni Kisutu ,Mnazi Mmoja na Kariakoo mtaa wa msimbazi. Ujenzi ule wa Stendi ya Dala dala uliwafanya wengi wa wafanyabiashara hao kuhamishwa kwa nguvu na bila kupewa eneo mbadala na wengi kuishia kufanya biashara zao bara barani na wengine kuhamisha biashara zao karibu na tanki kubwa la maji ambalo sasa hivi kuna biashara kubwa ya matofali.

Kitu ambacho Manispaa ingetakiwa kuliangalia, ni namna ambavyo itakavyo weza kujaribu kusuluhisha kadhia hii na sio kuwatupia virago wafanyabiashara ndogo ndogo kwani wao watafuta rizki zao kwa jasho lao. Manispaa ingejaribu kuwekeza kama walivyojaribu kuwekeza wale wenzao wa Ilala kwa kujenga Machinga Complex ambayo nadhani ingekuwa na tija. Mfano mdogo tu ni namna walivyoweza kuwahamisha wauza Mitumba wa Manzese na kuwapeleka katika eneo la Urafiki ambalo pia sasa hivi limejaa na wachuuzi wameanza kurudi kwa kasi maeneo ambayo walihamishwa huko nyuma.

Kamwe hatua hii isitumike na kutazamwa na wengine kama turufu ya kisiasa kwani wapo ambao watalichukulia suala hili kisiasa na kuanza kujenga uhasama ni vyema Manispaa ikajipanga na kuwatafutia wahusika eneo mbadala ili wao waweze kujipatia rizki zao pamoja na wale walaji. Naamini wapo watu wengi ambao hujipatia mahitaji yao pale Ubungo Mataa , Stendi , Darajani pamoja na maeneo yanayoizunguka Ubungo sasa kuwafukuza wafanyabiashara pekee kwa sababu kwanza wanafanya katika eneo hatari , ni sahihi lakini kuwapatia eneo mbadala ni changamoto ingine.

Mwisho matumizi ya nguvu kamwe hayasaidii katika kufikia makubaliano na muafaka wa jambo isipokuwa mazungumzo. Utaratibu uandaliwe ili wawakilishi wa wahusika yaani wafanyabiashara ndogo ndogo na watendaji wa Manispaa wakutanishwe na kutafuta suluhu kwa pamoja na ndio maana kuna serikali. Serikali sio diwani, Mbunge, Mkurugenzi, Waziri ama Rais au CCM. Serikali inatokana na watu ambao wamepelekea kuwapo kwa watu hao na suala hili lisipelekee uchochezi na masuala ya uhasama kwani ni la muda sasa na wahusika wamelikalia kimya.No comments: