Thursday, March 8, 2012

WANANCHI WANA HAKI YA KUISHINIKIZA SERIKALI YAO
Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,

JE, wananchi wanaweza kuishinikiza Serikali au viongozi wao kufanya jambo? Iwe kwa migomo, kauli au tishio la mgomo? Je, wananchi waliochoshwa na jambo Fulani wanaweza kuamua kukaa na kufunga geti la ofisi hadi wasikilizwe na viongozi wao? Jibu la maswali hayo linategemea sana watu wanaichukuliaje Serikali yao.

Katika nchi ya kidikteta au yenye utawala wa kiimla wananchi hawana uwezo wala haki ya kufanya jambo lolote kuilazimisha au kuishawishi Serikali yao; Serikali hufanya lile ambalo inataka kufanya, na Rais wa nchi kama hiyo hana mtu yeyote wa kumsikiliza isipokuwa yeye mwenyewe.

Katika mazingira ya kawaida Serikali inatakiwa kufanya mambo yake kwa kufuata taratibu mbalimbali na sheria zilizopo. Watendaji wake wanatakiwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Katika mazingira ambayo taratibu na sheria hizo zinafuatwa wananchi wanatakiwa na kwa kweli wanapaswa kukaa pembeni na kuiangalia Serikali yao ikitekeleza majukumu yake mbalimbali.

Sasa wakati wowote ambapo Serikali inaonekana kusikiliza wananchi wake na kufanya kazi ikionesha usikivu huo wananchi hujenga imani kwa Serikali hiyo.

Lakini inapotokea kuwa mambo mbalimbali yanaanza kuparaganyika na wananchi wanalalamika bila mafanikio basi wananchi wanaanza kutumia haki yao ya Kikatiba ya kutawala.

Haki ya kutawala ni ya wananchi

Mojawapo ya vitu ambavyo bado havijaeleweka vizuri ni haki ya wananchi kujitawala (the right to self determination).

Wapo watu wanaofikiria kuwa wenye haki ya kutawala ni wale wanaochaguliwa kuwa viongozi; kwamba wananchi wakishachagua viongozi basi wanakuwa wamehamisha haki yao ya kujiamulia mambo yao mikononi mwa Serikali na hivyo Serikali inaweza kufanya lolote, kwa yeyote na wakati wowote bila kuulizwa.

Sasa, kama wananchi wanafikiria hivyo kuwa walipopiga kura walihamisha madaraka yao kwenda kwa viongozi basi wananchi hao wanatarajiwa kukaa kimya na kutoihoji Serikali.

Wananchi wanatarajiwa kukaa kimya Serikali ikiboronga na wanatarajiwa kupiga makofi kiongozi mbovu akipita na kuhutubia.

Wananchi katika mazingira hayo wanakuwa chini ya viongozi na viongozi wanaweza hata kuwatukana – hasa kama si mwaka wa uchaguzi!

Hata hivyo hizi ni fikra potofu; haki ya kutawala inatokana inabakia kwa wananchi. Viongozi wanawatumikia wananchi na kwa kweli inamaanishwa hivyo kuwa wanawatumikia tu. Yaani, wananchi wanapochagua viongozi hawawachagui watu watakaokuwa juu yao bali watu watakaofanya kazi na kuwatumikia.

Wananchi wakitambua hili basi watajua kuwa wanapolalamika au kutoa shinikizo fulani kwa watawala hawavunji sheria na wala hawafanyi kitu kinyume nao!

Kutaka watu wawajibishwe ni haki ya wananchi

Inapotokea kuwa kuna viongozi au watendaji wa umma ambao wanaonekana kuwa ni kikwazo cha utekelezaji wa majukumu mbalimbali wananchi wanayo haki ya kulalamika. Haki hii huweza kuitumia kwa kutoa maoni, kuandika barua au hata kutumia vyombo vya habari kuelezea kwa nini watendaji hao wanapaswa kuwajibishwa.

Katika mazingira ya kawaida watendaji wa juu wanapaswa kuyapa uzito mkubwa madai ya wananchi na kutoyapuuzia!

Na pale inapoonekana au ambapo hamna shaka kuwa ni kweli watendaji hawawajibiki basi chombo chenye madaraka juu ya watendaji hao kinapaswa kuwawajibisha mara moja; si kwa sababu ya kuogopa wananchi bali kwa sababu kimewasikiliza wananchi.

Endapo chombo hicho kinadharau malalamiko au madai ya msingi ya wananchi na kuyapuuzia basi wananchi wanaweza kabisa kutumia haki ya kuongeza shinikizo hadi wasikilizwe; ikumbukwe haki ya kutawala haitoki Ikulu au bungeni! Inatoka kwa wananchi!

Mgogoro wa madaktari ni mgogoro wa dharau

Kumekuwa na tabia mbaya sana ya baadhi ya watendaji kujiona wako juu ya wananchi kwa sababu wana magari makubwa, wanapigiwa saluti na kusindikizwa na vimulimuli. Nyerere aliita hili “pomposity” yaani “kujionesha”. Viongozi na watendaji hawa wanaamini kabisa kuwa wao ni zawadi ya Mungu kwa Watanzania na hivyo hakuna mtu wa kuwahoji, kuwauliza au kuwanyooshea kidole. Ole ni kwa yule atakayethubutu kufanya lolote kati ya hayo.

Hata hivyo, mwaka huu tumeoneshwa kitu ambacho tunakijua.Kwa muda madaktari walikuwa na malalamiko na wakayapitisha kwa kutumia taratibu mbalimbali za Serikali bila mafanikio. Walipotoa tishio la mara ya kwanza kuhusu mgomo watendaji wa juu walipuuzia kwa sababu hawakuamini kuwa madaktari wanaweza kufanya hivyo; na mgomo ulipoanza bado wapo walioona kuwa mgomo hautafanikiwa.

Nakumbuka gazeti moja la kila siku liliandika kuwa “Mgomo wa madaktari wafifia”! Waliombea kweli ufifie na siwezi kushangaa kuna watu walikuwa wanaambiana kuwa umefifia!

Matokeo yake tukapoteza karibu wiki mbili za viongozi wabishi! Sasa walipoamua kukaa na kutatua, tatizo la msingi kabisa lilikuwa ni uwepo wa Waziri na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na Mganga Mkuu ambao hawakuwa wakiwasikiliza, wenye kiburi na waliolewa madaraka.

Tulipoandika kuhusu vipimo vibovu vya HIV ilitosha kabisa kuwa sababu ya kuwafukuza wote hao kazi lakini haikutokea; kumekuwepo na kashfa nyingine kadhaa kwenye wizara hiyo lakini waliowateua watu hao inaonekana hawajali kabisa.

Badala ya kusafisha wizara watu walisimamishwa huku waziri na naibu wakiendelea bila kuonesha kuwa wanajali.

Sasa leo hii mgogoro mwingine unanukia na wapo watu wanaoshangaa kwa nini madaktari wanataka kugoma tena!

Kwa mara nyingine madaktari wanaitwa kuwa na umoja kwa sababu hakuna vitu vya kuchezea kama afya ya Watanzania. Serikali inaweza kabisa kupata waziri, naibu, katibu na mganga mkuu mwingine lakini haiwezi kuwarudisha Watanzania watakaopoteza maisha kwa sababu ya kuwakumbatia viongozi wabovu!

Ni matumaini yangu kuwa Mponda na Nkya wataaamua wao wenyewe kujiuzulu mara moja kabla ya mgomo huu mwingine kuiva tena kwani kama wanafikiria wananchi watawageuka madaktari wanajidanganya kwa sababu Serikali inatakiwa kupima tu – kuna faida gani kuwakumbatia watu wanne na kuangamiza mamia ya Watanzania?

Wizara inahitaji mwanzo mpya na mwanzo huo mpya hauwezi kuwahusisha watu hawa wanne; hili wananchi wana haki ya kulisema, kulisimamia na hata kulilazimisha kwa migomo. Nawaunga mkono madaktari.


RAIA MWEMA

No comments: