Friday, March 30, 2012

WAFADHILI WAJITOA KUISAIDIA TACAIDS


Raymond Kaminyoge,

NCHI tisa za Ulaya na Asia zilizokuwa zikiisaidia Tanzania fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi, zimesitisha msaada wake katika kile kilichoelezwa kuwa, kuiwezesha Serikali kuanza kujitegemea.

Nchi hizo ni Japan, Sweden, Ireland, Norway, Switzerland, Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji na Uholanzi.

Uamuzi huo umekuja wakati ambapo Serikali imekuwa ikitegemea sehemu ya fedha za wafadhili kutoka Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi na Kifua Kikuu (Global Fund) kwa ajili ya kuhudumia waathirika na ununuzi wa dawa.

Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Fatma Mrisho alitangaza uamuzi wa nchi hizo kusitisha misaada hiyo na kuitaka Serikali iharakishe mpango wa nchi kuanza kujitegemea.

Dk Mrisho alitoa kauli hiyo wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala iliyotembelea ofisi hizo zilizopo jijini Dar es Salaam jana.

Alisema mbali ya nchi hizo, Jumuiya ya Ulaya (EU) na Benki ya Dunia (WB) pia zimesitisha misaada ya Ukimwi kwa Tanzania.

Dk Mrisho alisema waliobaki ambao wanaendelea kuisaidia Tanzania kudhibiti Ukimwi ni Marekani na Global Fund.

“Serikali ya Marekani na Global Fund ambao ndio wafadhili wakubwa, programu zao zinaishia mwaka 2013, hatuna uhakika kama wataendelea kutusaidia,” alisema Dk Mrisho.

Aliongeza kuwa shughuli za Ukimwi hapa nchini zinahitaji Sh1 trilioni kwa mwaka, ambapo asilimia 97 ya fedha hizo, zimekuwa zikitolewa na wafadhili.

“Fedha za Ukimwi zinategemea zaidi wafadhili tuombe Mungu waendelee kutusaidia wakisitisha wote tutafanya nini?” Alihoji Dk Mrisho.

Alisema ili kukabiliana na hali hiyo, Tacaids iko kwenye mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Ukimwi Tanzania.

Mwenyekiti huyo alisema, nyaraka za mchakato huo zimeandaliwa kwa ajili ya kufikishwa kwenye Kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC).

Dk Mrisho, alisema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kukusanya rasilimali kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kudhibiti Ukimwi.

Alisema pia ni kukidhi matakwa ya sera ya Taifa ya Ukimwi ambayo inatamka bayana kwamba Serikali itaanzisha mfuko huo.

Alisema kama ilivyo kwa sekta nyingine nchini, mahitaji ya fedha kwa ajili ya shughuli za Ukimwi ni makubwa kuliko kiasi kinachopatikana.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Pindi Chana alisema kamati yake inapitia taarifa za utendaji wa Tume hiyo, kama sehemu ya maandalizi ya kupitisha bajeti yake ya mwaka 2012/13.

Alisema katika vikao hivyo, wabunge watapata fursa ya kuhoji utendaji wa shughuli mbalimbali za Tacaids ili kufahamu mafanikio na matatizo ya Tume hiyo.

“Namna mtakavyowaelewesha vizuri wabunge kuhusu utendaji wenu, ndiyo wanavyoweza kupitisha bajeti yenu kwa sababu watakuwa wanafahamu fedha mlizopewa mwaka uliopita mlizitumia vipi,” alisema Chana.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu aliilaumu Tacaids kwa kile alichosema, imeshindwa kutoa tamko kwa wakati baada ya vifaa bandia vya kupimia Ukimwi kuingizwa nchini.

“ Tacaids ndiyo wahusika wakuu wa kudhibiti Ukimwi nchini, vifaa feki (bandia) vya kupimia Ukimwi vimeingizwa lakini mkashindwa hata kutoa tamko. Mnajenga taswira gani?” Alihoji Mtemvu.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Angellah Kairuki, aliitaka Tacaids kutekeleza majukumu yake kwa uwazi.

Alisema baadhi ya wananchi wanashindwa kufahamu namna Tume hiyo inavyofanya kazi kwa kushirikana na wadau mbalimbali.

MWANANCHI

No comments: