Monday, March 5, 2012

SOFIA SIMBA ADAIWA KUPORA ARDHI RUFIJI
Amin Yasin, Rufiji na Shakila Nyerere, Kondoa


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake Tanzania, Margareth Chacha pamoja na maofisa kadhaa waandamizi wa Serikali wanadaiwa kuwarubuni wananchi wa Kijiji cha Chumbi B kilichoko katika Kata ya Chumbi, Rufiji mkoani Pwani na kupewa ekari 1,500 za ardhi.

Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Abdulrahman Ngongwa zimewataja vigogo wengine kuwa ni ofisa mmoja mwandamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ndugu zake wawili na dereva wake, ofisa mmoja mwandamizi katika Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na mfanyabiashara maarufu wa vinyago nchini ambao hawatajwi kwa kuwa hawakupatikana kujibu tuhuma hizo zinazowakabili.

Waziri Simba na Chacha walikiri kutambua mgogoro huo lakini wakasema kuwa hawahusiki moja kwa moja. Baadhi ya vigogo hao akiwamo waziri huyo hawajawahi kufika kijijini hapo, lakini wanadaiwa kumtumia mfanyabiashara huyo wa vinyago kwenda kijijini hapo kuwaombea ardhi.

“Huyo ndiye aliyewaombea ardhi wenzake hao na akaleta orodha ya watu 30 wote kutoka Dar es Salaam," alisema mmoja wa wanakijiji hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Ofisa Mtendaji huyo alisema majina ya watu yapo ofisini kwake akisisitiza kuwa idadi yao inafikia 30 na kwa pamoja, wanataka ekari 1,500 ili wagawane kila mmoja ekari 50.

Baadhi ya viongozi wanaopinga kutolewa ardhi hiyo, Juma Mng’ombe na Saidi Mpapu walisema kuwa hawakushirikishwa katika kuridhia utoaji wa ardhi hiyo kwa kuwa kijiji hicho kina watu karibu 5,000 lakini waliohudhuria mkutano ulioidhinisha ardhi hiyo ni 94 tu.

Tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani humo imebaini kuwa ardhi hiyo ya Kijiji cha Chumbi B ilitolewa kwa kundi hilo la watu 30 baada ya baadhi ya wananchi na wajumbe wa Serikali ya kijiji hicho kupokea rushwa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara aliouitisha katika Kijiji cha Chumbi A, Februari 22 mwaka huu, Kaimu Kamanda wa Takukuru Wilaya ya Rufiji, Fredrick Msae alisema baada ya kusikiliza kero za wananchi wanaopinga na wale wanaokubali kutoa ardhi, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Chumbi B wamepewa kiasi cha Sh5,000 kwa kila mwanakijiji aliyehudhuria mkutano huo.

Alisema baadhi ya wajumbe wa Serikali na wananchi waliohudhuria Mkutano Mkuu wa kijiji hicho uliofanyika katika Kitongoji cha Kipoka, Novemba 26 mwaka jana walisema katika mkutano huo kuwa walipokea fedha kuanzia Sh5,000 kila mmoja na mwenyekiti wa kijiji hicho ndiye aliyekuwa akigawa fedha hizo.

“Niliona ni busara nifike kijiji na niitishe mkutano wa wananchi wa vijiji vitatu vya Mohoro, Chumbi A na B ambavyo wananchi wanalalamika na wananchi wenyewe wamekiri hadharani kuwa rushwa imetolewa,” alisema.

Msae alisema kuwa amefarijika kuona watu hao wakisema bila hofu kuwa wamepokea rushwa ili kuruhusu ardhi hiyo itolewe kwa watu hao hivyo kuirahisishia taasisi hiyo kufanya kazi ya kuchunguza zaidi na kuwafikisha mahakamani wale wote waliohusika na tuhuma hizo.

Alishangaa kijiji kutoa ardhi bila kuwa na barua za maombi ya watu hao, barua za watendaji wa mtaa wanakotoka, picha zao na mikataba ya namna ya watakavyofaidika na ardhi hiyo na kuhoji inakuwaje watu 94 waweze kutoa ardhi wakati kijiji kina watu karibu 5,000?

Msae alisema kuwa Serikali ya Kijiji haikufanya busara kupuuza malalamiko ya wananchi wanaopinga ardhi hiyo kuchukuliwa bila wao kushirikishwa na kuomba mchakato mzima wa kurudisha ardhi hiyo ufanyike upya kwa kuwa uligubikwa na rushwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Nassoro Mwingira alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kuwa hajapata taarifa hizo. “Sijapokea taarifa zozote kuhusu malalamiko hayo, sijasikia kabisa.”

Chacha: Taratibu zilifuatwa
Kwa upande wake, Chacha alisema anachojua ni kwamba uongozi wa Serikali ya kijiji hicho ulitaka kutoa ardhi kwa ajili ya Kilimo Kwanza na taratibu zilifuatwa.

“Lakini baadaye ukazuka mgogoro kuhusu mchakato huo na kuona hivyo, mimi nikaamua kujitoa,” alisema Chacha na kuongeza:

“Ni kweli ardhi ilikuwa itolewe kwa watu 30 na mkutano uliopitisha ulikuwa halali ila kuna mtu mmoja ambaye anataka kutuchafulia majina. Mimi baada ya kuona kuna mgogoro, sikurudi tena maana siwezi kujiingiza sehemu yenye matatizo,” alisema Chacha.

Alisema alikuwa amehamasika kutokana na mpango uliokuwepo wa kutaka kuanzisha kiwanda cha kusindika mihogo na ardhi ilikuwa itolewe kwa ajili ya kilimo cha mihogo.

Simba: Sijawahi kufika huko
Waziri Simba alisema hajawahi kufika Rufiji ila alisikia mtu akisema kwamba kuna ardhi Rufiji: “Ni kweli nilipata taarifa kwamba kuna ardhi Rufiji na mimi kama mkulima nahitaji sana ardhi. Kwa hiyo niliagiza ikipatikana waniambie, lakini yule mtu niliyemwagiza hajaniletea majibu. Mimi pia nina haki ya kupata ardhi kwa ajili ya kilimo si ndiyo jamani?”

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mohamed Msango alinukuliwa katika kikao hicho na Takukuru akisema alifuata taratibu zote... “Tulianza kuwashirikisha Serikali ya kijiji na baadaye tukawa na mkutano mkuu wa kijiji.” Lakini alipokumbushwa sheria zinasemaje, alikiri kuwa mchakato huo ulikuwa na kasoro.

Mmoja wa wanasheria kutoka Taasisi ya Hakiardhi yaDar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kila mtu anayo haki ya kuomba na kupewa ardhi, lakini kwa kufuata sheria.

Diwani wa Kata hiyo, Ramadhani Mikole alisema hajaridhishwa na utaratibu uliotumika kutoa ardhi hiyo na kusema kuwa amewasiliana na viongozi wa vijiji hivyo wakutane ili kujadili upya suala hilo.

Kondoa nao wadai kuporwa ekari 1,494

Huko Kondoa, mgogoro wa ardhi umeibuka katika Kijiji cha Atta kilichoko katika Kata ya Itaswi ambako wanakijiji wanamtuhumu mwekezaji Mick Dennis kuwapora ekari 1,494 na kuharibu mazao ya wanakijiji kwa kuyamwagia sumu ya kuulia magugu.

Inadaiwa kuwa mwekezaji huyo amekuwa akifanya hivyo kutokana na kukingiwa kifua na baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo, akiwamo aliyekuwa Mkuu Wilaya, Said Bwanamdogo.

“Kabla mwekezaji huyo hajafika, mipaka iliyokuwa imewekwa kuvigawa Vijiji vya Chubi na Atta ni korongo na bikoni lakini baada ya kufika mwekezaji huyo, mipaka ilisogezwa kama kilometa tano hivi,” alisema Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Atta, Bakari Goronya na kuongeza:

“Hata wanakijiji hao walipokuwa wanalima kwenye mashamba hayo walikamatwa na kupigwa wakielezwa kuwa wamemvamia mwekezaji huyo.”

Kwa nyakati tofauti, wanakijiji hao waliiomba Serikali iwasaidie kuondokana na tatizo hilo lililokuwa likiwabughudhi tangu mwaka 2009 na kulazimika kuishi kama wahamiaji kwenye maeneo yao.

Diwani wa Kata ya Itaswi, Said Chobu alisema mgogoro huo tayari umefika Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ameagiza mashamba hayo yarudishwe kwa wanakijiji lakini hadi leo, agizo hilo halijatekelezwa.

Akizungumzia mgogoro huo Dennis alisema: “Nimekubaliana na wanakijiji wa Chubi kulima katika eneo hili. Niliomba kupewa ekari 5,000, lakini nimepewa ekari 1,764.96 tu. Makubaliano ya mkataba ilikuwa nijenge zahanati ya kijiji, nyumba ya mwalimu, kuchimba kisima cha maji na ofisi ya kijiji.”

Mick alisema kuwa amekuwa akiendesha shughuli zake kijijini hapo miaka miwili sasa lakini amechoshwa na mambo yanayojitokeza katika eneo hilo na maneno kwamba amepora mashamba ya wanakijiji na kuombwa fedha na baadhi ya viongozi wa wilaya.

“Nilikubaliana malipo kwa wale walioharibiwa mazao yao, lakini tathmini iliyoletwa ni kubwa na mimi siwezi kulipa kwa kuwa ni mbinu zimefanywa ili nitoe fedh,” alisema.

Kwa upande wake, Bwanamdogo alisema jana kwamba asingependa kuzungumzia suala hilo siku za mwishoni mwa wiki na badala yake akataka atafutwe siku za kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kondoa, Isdory Mwalongo alisema kero hiyo imekuwa ni ya muda mrefu na imefika wakati wa kuishughulikia kwa haraka ili kunusuru maisha ya wanakijiji hao.

“Tatizo hilo limekuwa likiongelewa lakini halipatiwi ufumbuzi. Ikiwezekana iundwe tume ya uchunguzi na watakaobainika kuhusika na uchochezi huo wakamatwe na washtakiwe kwa mujibu wa sheria,” alisema.


MWANANCHI

No comments: