Tuesday, March 20, 2012

POLISI, WATAWALA WAJIFUNZE KUTATUA MATATIZO , SI MATOKEO YA MATATIZO

KUMEKUWAPO na mijadala inayoongezeka kwa kipindi cha zaidi ya mwaka sasa juu ya namna polisi wa Tanzania wanavyoshughulikia maandamano ya raia. Maandamano haya yamegawanyika katika aina nne tofauti na yamekuwa yakiongezeka tangu miaka ya 2000, pale ambapo maandamano yasiyo na ‘ruksa’, ‘kibali’ na au ridhaa ya polisi na watawala yalianza kushika kasi.

Aina ya kwanza ya maandamano haya ni yanayoitishwa na watawala (au chama tawala) na washirika wake ili kuunga mkono hoja au uamuzi fulani wa serikali na viongozi wake. Aina nyingine ni yale ya ‘wapinzani’ wa serikali iliyopo madarakani; wengi kati ya hawa wapinzani ni wanasiasa kutoka vyama mbadala ambao huainisha hoja ya kuungwa mkono na jamii ili kudai au kupinga hoja au jambo fulani.

Maandamano haya ni nadra kupata ridhaa ya vyombo vya dola kufanyika na mara nyingi huishia kukatazwa, kutofanyika au kutumika kwa nguvu kuyadhibiti na hatimaye kuibua vurugu. Maandamano haya pia hufanana na yanayoitishwa na asasi za kiraia, vyama vya kijamii au wanaharakati wanaotumia haki yao ya kukusanyika na kueleza hisia zao juu ya jambo fulani.

Aina ya nne ya maandamano nchini ni ile ya dharura. Aina hii hujitokeza kwa misingi ya matukio. Jamii au kundi la wananchi huona au kusikia jambo na kuamua kuandamana kueleza hisia zao kwa watawala au kuwashinikiza kuchukua hatua fulani.

Maandamano ya aina hii hayana muandaaji au kiongozi, sehemu ya wananchi huungana na wengine wataojitokeza wakati wa maandamano.

Aina hii ya nne ndiyo iliyoonekana Songea Aprili, 2012 na polisi waliua raia wanne wakati wa maandamano hayo.

Wataalamu wa uendeshaji mamlaka za nchi wanaainisha vyombo vitatu muhimu kama vipimo vya hali ya mambo katika tawala za nchi yoyote duniani. Jambo la kwanza; utendaji wa vyombo vya usalama wa ndani ya nchi (polisi, askari magereza na askari wasaidizi wa mamlaka za ndani). Pili, utendaji wa serikali za mitaa na tatu, huduma za jamii (afya, maji, elimu).

Viashiria vya utendaji katika maeneo haya huashiria aina na ubora wa huduma za utawala uliopo kwa jamii husika. Utendaji wa vyombo vya usalama wa ndani ya nchi huashiria zaidi ya hali hii, yaani hali ya mawasiliano kati ya watawala na wananchi na namna vyombo vya sheria vinavyotekeleza haki kwa raia.

Kwa hoja hizi basi utendaji wa polisi ni jambo la msingi sana kuliangalia wakati nchi inapojikita katika mchakato wa kujenga na kuimarisha demokrasia yake. Hata hivyo, polisi wa Tanzania wamejikuta katika misuguano na raia huku shutuma dhidi ya chombo hiki muhimu zikiongezeka juu ya ukiukaji haki za binadamu na askari wake kuhusika katika matukio ya uvunjaji sheria.

Tumeshuhudia matukio mengi ya ukiukwaji wa hjaki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji, raia kujeruhiwa, uharibifu wa mali na vitendo vya udhalilishaji vikifanywa na vyombo vya usalama, hasa polisi.

Pia tumeshuhudia tume zikiundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza mauaji na ukatili huu unaofanywa na baadhi ya askari wake bila kuwapo kwa taarifa au hatua dhahiri kudhibiti matukio haya.

Taarifa kupitia vyombo vya habari na taarifa ya haki za binadamu Tanzania ya mwaka 2010, iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), zimejaa takwimu na matukio ya kutisha, hususan kuanzia mwaka 2008.

Katika mtiririko wa taarifa za namna hiyo, taarifa za matukio ya 2011 zinatisha zaidi. Baadhi ya matukio haya ni pamoja na lile la Januari 5, 2011 watu watatu ambao ni Denis Michael, Ismail Omary na Paul Njuguna Kaiyele waliuawa na wengine 21 kuumizwa vibaya wakati wa maandamano ya amani ya raia mjini Arusha.

Mei 16, 2011 polisi waliwaua watu watano katika eneo la Mgodi wa North Mara, wilayani Tarime, unaomilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold Mine na kufanya idadi ya watu waliouawa katika eneo hilo tangu mwaka 2009 hadi Juni, 2011 kufikia 34.

Kama hiyo haitoshi, Juni 9, 2011 kijana Nyaitore, mkazi wa kijiji cha Nyangoto wilayani Tarime alipigwa risasi ya bega na polisi wa mgodi na kulazwa Hospitali ya Sungusungu.

Mei, 2011 katika kijiji cha Namanga wilayani Nachingwea, askari wa wanyama pori walimpiga risasi kwenye miguu yote, Juma James (27) ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea.

Oktoba 31, 2010 vijana 11 wa kijiji cha Gibaso waliodaiwa kuingia kwenye hifadhi ya Serengeti kwa ajili ya kuwinda walikurupushwa na askari wa hifadhi ya Serengeti kambi ya Ramai.

Hadi leo hatma ya watu sita miongoni mwao haijajulikana huku kukiwa na taarifa kuwa walipigwa risasi wakivuka mto Mara katika kujisalimisha.

Kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, watu wanne wanaripotiwa kufia mikononi mwa Jeshi la Polisi wilayani Serengeti, kati ya Septemba 2010 hadi Juni 2011, hii ni pamoja na tukio la Juni 7, 2011 ambapo askari polisi wa kituo cha Mugumu wilayani Serengeti wanadaiwa kumuua kwa kumpiga risasi mkazi wa kijiji cha Nyiboko, kata ya Kisaka, Nyitamboka Mwita (28) nyumbani kwake wakidai ni jambazi.

Sambamba na hayo Daudi Makabara (40) alipigwa risasi na Askari Magereza wa Serengeti tarehe 29/3/2010 akiwa anapita na mifugo yake karibu na shamba la gereza la Mugumu.

Wimbi la ukatili na mauaji ya raia unaofanywa na baadhi ya polisi umeendelea hadi Tabora wilayani Urambo na Mei 28, mwaka jana askari polisi walimuua Juma Saidi na kujeruhi wengine kadhaa katika kijiji cha Usinge.

Picha za video za tukio hili zinaonesha wazi kuwa askari polisi aliyeua aliamua kwa makusudi kumlenga kijana aliye mbali na eneo la tukio na bila tahadhari akampiga risasi kwenye mbavu upande wa kulia kwa nyuma. Tukio hilo lilitanguliwa na kipigo kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Shela na wenzake, Mei 26, 2011. Vitendo hivi vilifanywa na askari waliokuwa wakikamata mifugo.

Aprili 2, 2011, mkazi wa Kijiji cha Mwanza Buriga, kata ya Kukirango Wilaya ya Musoma Vijijini, Mwabia Zome (40) aliuawa kwa kupigwa risasi chini ya titi la kushoto na askari magereza wa gereza la Kiabakari.

Watu wengine wa umri kati ya miaka 25 - 30 walipigwa risasi Machi 7, 2011 ambapo Sese Kabanzi, alifia njiani akipelekwa hospitali na July Hamisi alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi kifuani.

Februari 5, 2011 askari wa wanyama pori katika Hifadhi ya Selou waliripotiwa kuua watu wawili na kumjeruhi mmoja wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani. Waliokufa ni Hamisi Boy na Mohamed Suta na anayeuguza majeraha ni Mohamed Kigwiso.

Kuna ushahidi kuwa askari hawa wanashutumiwa kwa kuendeleza matukio ya ukatili dhidi ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kwa makusudi huku Jeshi la Polisi likishindwa kuwasaidia raia kulinda usalama wao.

Huko huko Kisarawe askari hawa wanadaiwa kuua na kuwatupa mtoni na walikoliwa na mamba; Ndugu Majengo, Mohamed Kibavu, Adamu Feruzi, Semeni Abdala Kube, Hemed Kassim, Mzee Hussein, Ramadhani Mgeto na Bwana Mkala.

Aprili 2010, askari walimuuwa Octavian Kashita jirani na nyumba ya Waziri Celina Kombani, eneo la Victoria Dar es Salaam. Pia polisi wa Kituo cha Chag’ombe Dar es Salaam walimkamata dereva teksi, Juma Musa na kumtesa hadi kufa.

Katika tukio jingine; Januari 18, 2010, polisi wa Kituo cha Kilwa jijini Dar es Salam walimkamata John Elias, mkazi wa Kigamboni Vijibweni na kumchoma sindano machoni. Sindano hiyo inadaiwa kuwa na maji yenye tindikali na walisababisha macho yake yote kutolewa na hatimaye kupata upofu wa kudumu.

Matukio haya na madai ya wananchi dhidi ya vyombo vya dola ni mengi ikiwa ni pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mavota, wilayani Biharamulo wanaowatuhumu polisi wa Kituo cha Mavota kwa kupiga, kunyang’anya fedha na mali na kuua raia katika eneo la mgodi wa dhahabu wa Tulawaka.

Kana kwamba hii haitoshi mwaka 2010 askari wa TANAPA walimuuwa mzee wa makamo na asiyekuwa na hatia, Ndekilwa Palangyo, huko Arumeru wakimdhania ndiye mtuhumiwa waliyekuwa wanamtafuta.

Matukio haya ya ukatili, unyanyasaji, vitisho na udhalilishaji unaofanywa na jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola si mageni sana na inatosha kusema hapa kuwa wananchi wanaendelea kujifunza mengi mabaya toka kwenye mlolongo huu.

Tukio la kufukiwa wananchi katika mgodi wa Bulyanhulu wakati ukibinafsishwa halijafanyiwa kazi hadi leo. Ushahidi wa mkanda wa video upo ambao unaonesha namna wananchi walivyofukiwa wakiwa hai, mali zao kuharibiwa na kudhalilishwa utu wao mbele ya viongozi wa serikali kwa kutumia vyombo vya dola.

Cha kusikitisha zaidi kuna matukio mengi ambapo ndugu za waathirika hayo ya ukatili wanaendelea kunyanyaswa pale wanapofuatilia haki au uwajibikaji katika vyombo vya usalama.

Matukio ya uchomaji moto miili ya marehemu, kulishwa mamba na kutupwa na kutelekezwa barabarani maiti ni matukio yanayotuingiza katika historia mpya ya kutojali haki za binadamu. Achilia mbali tukio la hivi karibuni la kule Songea ambako askari polisi waliwaua kwa risasi raia wanne waliokuwa miongoni mwa waandamanaji, wakishinikiza serikali mkoani hapa kuchukua hatua madhubuti kukomesha mauaji ya kiholela yanayosadikiwa kuhusika na ushirikina.

Pamoja na kwamba waandamanaji walitaka kuonana na kupata majibu kutoka kwa mkuu wa mkoa, askari waliwazuia na hatimaye kuua na kujeruhi waandamanaji bila hata mkuu wa mkoa kujitokeza kuonana nao.

Kwa upande mwingine viongozi wa jeshi hilo hawakuwa na hata muda wa kutafakari majibu kwa mauaji haya zaidi ya kutamka kwa sauti kubwa waliokuwa wakiandamana ni wahuni.

Jambo hili linajirudia mara kwa mara; kule Arusha, kamanda wa polisi wa wilaya anadaiwa kuwaita waandamanaji kuwa ni panya na hata kwenye vyombo vya habari baadhi ya viongozi wa jeshi hili huwaainisha waandamanaji kuwa ni wahalifu.

Hii inafanyika huku polisi na viongozi wake wakijua kwamba kuandamana ni haki ya msingi ya binadamu iliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na hata pale wanaharakati walipoingilia na kuhamasisha heshima kwa haki za binadamu na kulindwa haki ya kuishi, vyombo vya dola vimekuwa vikikebehi na hata kuwatishia kwa namna moja au nyingine. Hivi karibuni tumeshuhudia wanaharakati wakikamatwa kwa kuishinikiza serikali kumaliza mgogoro wake na madaktari ulioleta maafa na vifo kwa zaidi ya wiki tatu.

Wakati hali ikiwa hivyo hapa Tanzania, mahali kwingine duniani ambako maandamano yamekuwa yakifanyika kumetufundisha mambo tofauti yanayofanana; kwamba mahali waandamanaji walipopewa nafasi ya kueleza hisia zao na au kusikilizwa migogoro na maandamano haya huisha kwa amani na wakati mwingine suluhu hupatikana bila maafa, na pia pale waandamanaji walipozuiwa kwa matumizi ya nguvu zaidi ya kawaida madhara makubwa yamejitokeza ikiwemo machafuko.

Mifano ni mingi, yafaa kuitaja michache tu ya Tunisia, Libya, Misri, Ukraine na ule wa Ocupy Wall Street. Mara zote katika haya wanaharakati wamekuwa mstari wa mbele kueleza na kushinikiza hatua zichukuliwe kutatua matatizo bila mafanikio na mwishowe, wananchi wanaochoshwa na hali iliyopo huchukua hatua kali za kupambana na serikali zao na hata kuwaondoa kwa nguvu viongozi wake.

Somo tunalopata hapa ni kuwa iwapo tunapenda nchi yetu kwa dhati ni vema tutafakari juu ya sababu za maandamano na mbinu za kutatua tatizo halisi baadala ya njia zinazotumika sasa kutatua matokeo ya tatizo tu.

Bila mabadiliko ya kifikra miongoni mwa polisi na watawala, na tafakari ya kina juu ya maoni ya rai na yale yanayoibua maandamano, tutakuwa na wakati mgumu huko mbele ya safari bila kujali kama tutafika au la.


RAIA MWEMA

No comments: