Wednesday, March 21, 2012

POLISI, CCM MTAIINGIZA NCHI KATIKA MACHAFUKO

  • Ni mwendelezo wa kuchagua Azimio la Rushwa badala ya Azimio la Arusha

  • Tanzania si Mbingu, ikibidi ya Bukinafaso yanaweza kujitokeza nchiniKenya

MATUKIO ya polisi kuendelea kuua raia wasio na hatia kwa kutumia risasi za moto sehemu mbalimbali nchini ni ishara kwamba Serikali ya CCM imeshindwa kazi. Ni kwamba Serikali ya CCM haiheshimu utawala bora na wa sheria kama inavyojigamba katika medani za utawala wa kidemokrasia.

Hili nataka kuliweka wazi katika mada hii. Watanzania sasa tuwe wa kweli, tuache kubabaishwa na kutishiwa kwamba eti kila tunaposema yaliyo moyoni na kuitakia nchi yetu mema Waswahili hatua hiyo inatafsiriwa kuwa ni uchochezi. Lazima tuwe wa kweli na waswahili husema ; ‘‘Usipoziba ufa, utajenga ukuta.’’ Sasa hivi Tanzania imejionyesha kuwa na nyufa nyingi sana tena za hatari hasa katika suala la usalama wa raia wanaoeleza hasia zao kwa njia ya maandamao.

Tukio la hivi karibuni la kuuawa kwa raia wanne nyumbani kwetu Songea (mimi ni mwenyeji wa songea) limenisikitisha sana. Hawa waliouawa ni ndugu zetu, ni Watanzania wenzetu. Kwa nini wauawe bila sababu ya msingi, isipokuwa za kutunga tu? Huu mtindo wa kuua raia kwa visingizio vya kuhatarisha amani, visingizio vya kuvamia polisi vitaisha lini?

Kuendelea kutunga tunga tume zisizo na maana ni kuendelea kujidanganya machoni pa Mwenyezi Mungu anayejua na kuona yote na Watanzania wenye haki ya kuishi. Naomba tusiyapuuzie matukio yanayoonyesha hatari eti kwa sababu Watanzania ni wapole kwani wahenga husema tena ‘‘aliyelala usimwamshe... ukimwamsha utalala wewe.’’ Na Mwalimu Julius Nyerere alisema kwamba ; ‘‘kimya kimya usidhani ni ishara ya amani.’’ Maneno haya ya kinabii kama yanapuuzwa basi sitashangaa kwamba Tanzania inaelekea kule ambako Kenya ilikuwepo, yaani vita na mauaji.

Ninaona wazi kwamba mazingira haya haya ndiyo yaliyokuwapo hapa Kenya kabla ya kutokea kwa machafuko ya mwaka 2007, wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita. Sasa kama hatuwezi kujifunza kwa wenzetu basi sisi ni vipofu.

Nimekuwa nikifuatilia matukio ya mauaji ya raia wema kwa risasi za moto bila sababu ya msingi. Je, askari polisi wetu kazi yao ni kuua raia wasio na hatia au kulinda usalama wao na mali zao? Ukweli ni kwamba wakati miongoni mwetu tukiwa katika kipindi cha kwaresima, kipindi cha kuwa wa kweli ni vema tukakubali kwamba nchi yetu imetumbukia mahali pabaya sana.

Kuanzia Februari, mwaka 2002 pale Manzese kanisani (Kanisa Katoliki) nilihubiri siku ya Ijumaa Kuu kwamba ; "Tanzania imetumbukia mahali pabaya." Na ninaendelea kushikilia msimamo huo huo kwamba tumefika pabaya.

Propaganda za kisiasa zimeifikisha nchi katika mahali pabaya sana kwa sababu serikali na vyombo vyake inashindwa kusimamia haki ya raia wake kwa unyoofu. Inapojitokeza polisi kuonyesha upendeleo wa wazi kwa CCM na viongozi wa Serikali bila kujali maslahi ya raia bali ya kisiasa tu, lazima sisi wenye akili tujiulize maana yake nini?

Huu mtindo wa polisi kutumiwa na Serikali ili kunyamazisha haki za wananchi wawe wapinzani au raia wa kawaida ni kupoteza muda. Huku ni kuhairisha kutafuta dawa ya matatizo. Mwaka jana dunia ilishuhudia viongozi wengi waliokuwa wanatumia mabavu kutawala nchi waking’olewa, mfano dhahiri ni Gadaffi (Muammari Gaddafi wa Libya), aliyekuwa Rais wa Misri (Hosn Mubarak) na wengineo.

Kwa upande wa nchi yetu, polisi kujaribu kuibeba CCM ni kupoteza muda kwa sababu nguvu ya umma ikiamua kuleta mabadiliko hakuna atakayeweza kuzuia. Hakutakuwa na suala la risasi za moto, bunduki, hakuna cha mizinga hakuna chochote kinachoweza kuzuia.

Hapa Kenya kati ya vyombo vilivyosababisha vurugu na baadaye mauaji ni polisi, kwa kushabikia chama tawala. Kwa hiyo, nashauri jeshi la polisi nchini Tanzania litende haki sawa kwa wananchi wake na vyama vyote vya kisiasa. CCM ikikosea iadhibiwe kama chama chochote kile cha kisiasa na sheria ichukue mkondo wake bila kupendelea.

Tukumbuke kwamba Mungu wetu si Mungu wa upendeleo, bali ni Mungu wa haki. Mara kadhaa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa amewahi kusema ; "Jk (Rais Jakaya Kikwete), Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba wajiandae kwa lolote lile litakalotokea kwa upande wa uchaguzi.’’

Wiki hii, Dk. Slaa amerudia maneno hayo hayo kuhusiana na mauaji ya raia wema huko Songea. Hivi serikali na jeshi letu la polisi wanataka waambiwe na Marekani, Uingereza na Ufaransa ndipo wasikie?

Matukio ya mauaji katika mikoa mbalimbali ya Mbeya, Mara, Mwanza, Dar es Salaam na sasa mkoani Ruvuma wakati wa maandamano ni alama ya wazi kwamba wananchi wamechoshwa na serikali yao.

Wananchi wanataka haki yao ya msingi, pale wanaposhindwa kuipata, wanaamua kuandamana kitu ambacho ni haki yao ya msingi. Kuandamana ni haki ya msingi ambayo inatambuliwa na sheria za Umoja wa Mataifa.

Je, polisi wetu wanalifahamu hilo au hawalijui? Kusingizia kila wakati kwamba maandamano yanakuwa na ishara ya kuvunja amani ni kuendelea kujidanganya na kukosa elimu ya maana kuhusu umuhimu wa maandamano.

Mauaji ya Songea yametia doa kubwa sana mkoani Ruvuma na sisi Wana-Ruvuma hatuwezi kukaa kimya kana kwamba hatutambui haki za wananchi. Ndiyo kwa maana mimi kama Mwanaruvuma nimeamua kuchukua kalamu na kutoa hisia zangu za moyoni kuhusiana na mauaji haya ya kinyama ya ndugu zangu huko Songea.

Hii tabia ikiachwa iendelee itazoeleka na mwisho wake tutakuwa tunaishi katika uadui kama Waisraeli na Wapalestina. Polisi wanaoua raia wema ni ndugu zetu na tunaishi wote mitaani, hivi inaiingia akilini kweli wao kuanza kutuua sisi raia?

Je, raia wakiungana pamoja na kuamua kupambana na kila polisi anayeonekana mitaani hapa kutakuwa na usalama gani? Hili lilishatokea katika nchi ya Bukinafaso ambapo polisi walipiga mwanafunzi hadi kufa na baadaye wanafunzi waliamua nchi nzima kupambana na kila polisi aliyeonekana, na baadaye wazazi nao waliungana na watoto wao.

Je, hali kama hii ikitokea nchini Tanzania polisi mtakuwa na usalama gani? Mtasema tunachochea, la hasha, bali tunaeleza yale yaliyokea katika nchi nyingine, Tanzania si mbingu, ni sehemu ya dunia ambayo chochote kile kinaweza kutokea.

Ninawaomba wanaruvuma kuhakikisha tume iliyoundwa inatoa haki kwa wananchi na siyo kuikingia kifua Serikali.

Ukiangalia jinsi kampeni zinavyofanyika nchini Tanzania, kuna matukio ya maovu mengi sana ambayo yanaashiria kwamba huko tuendako kuna machafuko makubwa yatatokea tu. Viongozi wa dini wamejaribu kuonya lakini inaonekana nao wanaingizwa katika masuala ya kejeli, udini na kushabikia siasa kitu ambacho ni hatari sana.

Mtu kama mimi nianze kushabikia siasa itanisaidia nini? Kazi yangu kama padre au kiongozi wa dini ni kusema ukweli na kukemea bila kujali sura ya mtu au chama fulani kwa maslahi ya Watanzania.

Chaguzi zetu zote zinajaa mizengwe na hujuma kubwa sana hasa kwa vyama vya upinzani. Ni lini Tanzania itaendesha uchaguzi huru na wenye kutenda haki? Viongozi wengi wastaafu kama Jaji Joseph Warioba, akina Joseph Butiku wameshasema hadi kuchoka kwamba uchaguzi wa Tanzania ni biashara ya kununua na kuuza kura. Je, hilo nalo nikiliandika Serikali itasema tunaichukia au tunapandikiza chuki kati ya wananchi ya Serikali yao ?

Tukiangalia Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), wakati mwingine inatia shaka kubwa sana kwamba inapendelea na kukibeba Chama cha Mapinduzi. Inakuwaje kwamba ratiba inapangwa kwamba mikutano iishe saa 12.00 jioni lakini mgombea wa CCM anaruhusiwa kuendelea na mikutano? Hapa kuna sheria ngapi za kufanya kampeni?

Na akiwa kiongozi wa upinzani amepitisha huo muda, polisi haraka watakwenda kumtoa kwa nguvu na kumfungulia mashitaka? Watanzania wenzangu nchi yetu inakwenda wapi? Je, hii ndiyo ile nchi Tunayoiimbia " Tanzania, nakupenda kwa moyo wote" wimbo ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye sasa ni Mtumishi wa Mungu? Inanitia shaka kuamini hilo.

Mimi nasema Watanzania miongioni mwetu hatuko makini kiasi cha kutosha, tunafanya utani na amani ambayo ni zawadi ya Mungu. Tume ya uchaguzi fanyeni haki kuanzia sasa hivi kwa kudhibiti kila aina ya utovu wa nidhamu bila kupendelea chama.

Unajua bahati mbaya ni kwamba unapoamua ‘kuwazuga’ watu kwamba unatenda haki, na kumbe sivyo Watanzania wanafahamu ila kitu kimoja tu kwamba "hawana mahali huru na wazi pa kusemea" bila kufuatwa na vyombo vya dola.

Hili ndilo tatizo la demokrasia ya Tanzania. Demokrasia ya kweli inahitaji utendaji wa haki kuanzia siku ya kwanza ya kampeni, kinyume cha hapo hutaweza kutenda haki wakati wa kupiga kura, kuhesabu na hata kutangaza matokeo. Je, tume hii imejiandaa kiasi gani katika hayo, kusema na kutangaza ni rahisi sana kupitia vyombo vya habari lakini shida yangu kiutendaji ni kwa namna gani tume imejiandaa ?

Sasa macho karibu yote ya Watanzania ‘yamelekezwa’ Jimbo la Arumeru Mashariki, katika kinyang’anyiro ya uchaguzi wa ubunge jimboni humo. Awamu hii tunataka wananchi waachwe huru wachague mbunge wanayempenda, atakayeshindwa akae pembeni na atakayeshinda, basi aachwe aingie bungeni kwa amani. Na hii ndiyo maana ya demokrasia na utawala bora, ndiyo maana ya chaguo la umma, chaguo la Watanzania.

Hayo niliyoyasema hapa juu yanakwenda kwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo imepewa mamlaka makubwa katika uchaguzi huu. Swali langu ni moja ; Je, ofisi hii imepania vipi katika kutenda haki? Swali hili linaambatana na lawama zilizowahi kuelekezwa kwa ofisi hii ya msajili kwamba inakipendelea Chama cha Mapinduzi katika utendaji wake.

Masuala ya kutumia ubabe hayatatupeleka popote pale katika nchi yetu. Dawa ya Tanzania ni moja tu ambayo pia itasaidia kuleta amani na maendeleo kwa haraka. Dawa hiyo ni kutenda haki, hii ndiyo misingi ambayo Mwalimu Julius Nyerere aliijenga kupitia Azimio la Arusha ambalo liliuawa miaka michache iliyopita na likaletwa Azimio la Rushwa.

Narudia tena kwamba polisi na CCM mtatuingiza katika machafuko sasa hivi kama Serikali iliyopo madarakani haitatenda haki kwa raia wake. Lazima niseme wazi kwamba amani ya Tanzania ni muhimu kuliko chama chochote kumpata mbunge au kuliko kuficha makosa ya kiongozi yeyote.

Mwisho napenda kuwashauri viongozi wenzangu wa dini kwamba, haisaidii kukaa kimya wakati maovu yanajitokeza katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi mdogo Arumeru Mashariki na hasa wakati wa kampeni.

Mara chache nimesikia viongozi wa dini wakikemea maovu hayo kitu ambacho ni wajibu wao. Najiuliza hivi viongozi wa dini mnaogopa nini? Je, hamkupokea unabii kutoka kwa Bwana?

Machafuko yakiingia katika nchi mtakwepea wapi? Tukumbuke kwamba sisi tumepewa wajibu huu na Mungu siyo kutoka kwa chama au Serikali yoyote, na hivi tunawajibika kwa Mungu siyo kwa binadamu.

Najua viongozi wengi ni waoga kwa sababu wataambiwa umefanya siasa katika nyumba ya ibada. Mimi nauliza kufanya siasa katika nyumba ya ibada maana yake nini? Na nyumba ya imani ni nini? Na kiongozi wa dini ni nani? Mambo hayo yote lazima yaainishwe, namna nyingine hizi ni propaganda za Serikali za kudhoofisha, kuwatisha na kuwapotosha viongozi wa dini juu ya wajibu wao.

Msipokemea maovu hayo sasa hivi, mtakemea lini? Injili ya Yesu ina nguvu ya kubadiilisha mioyo ya watu hasa katika kipindi hiki cha kwaresima, kipindi cha kupata Neema, ukweli na uponyaji wa masuala mbalimbali yakiwamo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Utamaduni huu mchafu wa kuua raia kinyama ni lazima ukomeshwe haraka la sivyo nchi hii itageuka kuwa kisiwa cha mauaji na maovu.RAIA MWEMA

No comments: