Friday, March 9, 2012

KUJARIBIWA KWA KIONGOZI

Pichani Rais Kikwete akiwakoromea wafanyakazi "mbayuwayu" mwaka 2010 na kuzuia mgomo wao
Na M.M Mwanakijiji,


Leo tutashuhudia kujaribiwa kwa Rais Kikwete kama kiongozi. Naamini hakuna kipimo kizuri cha uwezo wake wa kuongoza na kulishawishi taifa kama atakavyojaribu kuonesha njia ya kushughulikia tatizo la mgomo wa madaktari nchini. Uchaguzi kwake ni mwepesi sana; kuwafanya madaktari waonekane maadui na kuwapa jina baya (demonize) ili kuhalalisha maamuzi dhidi yao ama yeye mwenyewe kuonesha kuwa anawajibika kwa serikali yake kushindwa kushughulikia matatizo ya mgogoro huu uliodumu kwa wiki kadhaa sasa.


Kuwa-demonize madaktari


Njia rahisi na uamuzi mwepesi kwa Rais Kikwete – na yawezekana maarufu kwa baadhi ya watu – ni kuamua kuwabebesha lawama madaktari. Kama tukitumia mfano wa jinsi alivyotumia kikao kama hicho Mei 2010 tunaweza kusema kwa uhakika mkubwa tu kuwa Rais Kikwete anaweza akawafanya duni madaktari na kuwatisha. Katika mkutano uliofanyika Diamond Jubilee wakati ule Rais Kikwete aliwaambia wafanyakazi waliokuwa wanajiandaa kugoma “Mie ndiye muajiri mkuu nisikilizeni mimi, msimsikilize Mgaya (Kaimu Katibu Mkuu TUCTA) mtafukuzwa kazi wala Mgaya hamtamuona! Mtapoteza haki zenu…akili ni nywele kila mtu ana zake mtu mzima dawa”


Akiamua kuchagua njia hii ya kuwa-demonize madaktari ili kujenga hoja ya kuwafukuza kazi atakuwa amechagua njia aliyoizoea –yaani njia ya kutokujaribu kushawishi. Njia hii hata hivyo inadhania (presume) kuwa serikali iko sahihi na haijakosea. Na ninaamini hapa ndipo mgongano ulipo – je serikali imekosea katika kushughulikia suala la madaktari toka mwanzo? Akichagua njia hii manake ni kuwa haamini serikali imekosea na hivyo lawama zote ziwaendee madaktari.

Kwa hiyo, kwa njia hii kuna uwezekano mkubwa wa kutumia muda mrefu kuelezea historia ya “mazungumzo” kama alivyofanya kwa wafanyakazi.

Kwenye kikao kile cha karibu miaka miwili iliyopita Rais Kikwete alisema kati ya mengi “Nimesikia wakiwashawishi kugoma wakitutuhumu sisi kuwa ni serikali isiyoambilika, huo ni uongo na hawa viongozi wa TUCTA ni waongo, wanafiki…nilieleza katika hotuba yangu ya mwezi Machi jinsi serikali ilivyochukua hatua kuboresha maslahi ya wafanyakazi, na dhamira ya kuendelea kuwajali.” Akaongezea na kusema “Nikasema hata katika bajeti ijayo tumejiandaa kuongeza kima cha chini toka sh 60, 000 hadi kufikia 105,000…nikaeleza mambo mazuri toka katika sekta binafsi na umma lakini yote haya wenzetu hawayaoni hata walidiriki kusema kuwa Kikwete kaongeza shilingi 4,000 tu, ama kweli akutukanae hakuchaguli”


Kama huo ni mfano basi tutarajie Rais Kikwete kuwaita majina ya ajabu madaktari. Bado tunakumbuka jinsi Waziri Mkuu mara ya kwanza alipoamua kumuita jina baya (demonize) Dr. Ulimboka na kumdunisha mbele ya jamii. Safari hii kuna uwezekano wa madaktari wote kujaribiwa kufanywa duni na kuitwa “waongo, wanafiki” na kama tumesikia maneno ya karibuni basi “hawana utu, siyo wazalendo, na hawajali viapo vyao”. Yote haya yatafanyika katika kuhalalisha hoja kuwa serikali haijafanya makosa na haipaswi kulaumiwa kwa yanayotokea.


Akichagua njia hiyo manake ni kuwa madaktari watatakiwa kurudi kazini “mara moja” na vitisho vingi – baada ya historia ndefu itakayokuwa inashangiliwa na wazee walioalikwa. Hapa atapata ushujaa wa muda na sifa za kitambo; tatizo la msingi litakuwa halijatatuliwa.


Yeye mwenyewe kukubali kuwajibika


Mojawapo ya vitu ambavyo tumevikosa kwa muda mrefu ni Rais Kikwete kukubali makosa na udhaifu wa serikali yake. Mojawapo ya vitu ambavyo tumejifunza katika historia ya taifa letu hasa wakati wa Mwalimu ni uwezo wa Baba wa Taifa kukubali makosa na kujaribu kusahihisha makosa. Kwa wanaokumbuka mojawapo ya nyaraka muhimu sana katika historia ya mwanzo ya taifa letu ni ile ya “TUJISAHIHISHE” kwani ilikuwa ni katika nyaraka ile ambapo Nyerere alijaribu kuangalia miaka kumi ya mwanzo ya uhuru na makosa yaliyofanyika na kuweka mkakati wa kuyasahihisha makosa. Kinyume na porojo nyingi kuwa Nyerere “hakuwahi kukubali kukosolewa” ukweli wa kihistoria ni kuwa alifanya hivyo mara nyingi. Siyo kwenye serikali tu hata kwenye chama chake. Kwa wana CCM wanaweza kufanya vizuri kujisomea “MWONGOZO WA 1981” ambao kwa kiwango kikubwa ilikuwa ni jitihada pia ya kujichunguza.


Kwa miaka hii mitano iliyopita ya utawala wa Rais Kikwete hakuna wakati wowote ambapo yeye kama Rais amewahi kukaa chini na kuonesha makosa ya serikali yake au hata kuanzisha program ya kujisafisha. Yawezekana Rais Kikwete hataki kuonekana dhaifu; kwa kukubali kuwa kuna makosa atakuwa anawapa maadui zake silaha ya kutumia dhidi yake.


Hata hivyo hapa ndio kipimo hasa cha uongozi. Suala la mgogoro wa madaktari katika nchi nzima lilipaswa kuingiliwa na kuangaliwa na Rais mara moja. Nilipoandika juu ya “tepidity” ya mwitikio wa Rais Kikwete nilimaanisha hili hasa. Kwamba, mgomo wa madaktari ulikuwa jambo kubwa sana kiasi kwamba Waziri Mkuu halimtisho. Walipokubali kurudi kazini na kutoa wiki tatu nilitarajia kuwa labda wakati huo Rais Kikwete angeonesha uongozi yeye mwenyewe kwa kujaribu kuingilia kati na kusikiliza uzito wa madai ya madaktari kutaka Waziri na Naibu wake wawajibishwe. Hakufanya hivyo.


Matokeo yake ni kuwa njia pekee iliyobakia – na sahihi- ni kwa rais Kikwete kukubali moja kwa moja kuwa anawajibika kwa makosa ya mawaziri wake na wale aliowateua na kuwa angepaswa kuingilia kati mapema zaidi. Wamarekani wanamsemo kuwa “the buck stops with the president” wakimaanisha kwamba mwisho wa siku ni Rais anayewajibika. Nitatumia mfano wa Rais Obama mwaka 2010. Kufuatia kumwagika kwa mafuta kwenye Ghuba ya Mexico watu wengi walilalamikia jinsi serikali ilivyoitikia hasa kwa kuacha kwa muda mrefu kampuni ya BP kuamua nini kinafanyika. Hatimaye Rais Obama akizungumza na waandishi wa habari alisimama na kusema kuwa kulikuwa na udhaifu wa mwitiko wa serikali yake – japo ilikuwa inafuatilia – na kuwa kama kulikuwa na mtu anataka kujua nani anawajibika Obama alisema kwa Kiingereza “In case you were wondering who’s responsible, I take responsibility” yaani “kama mlikuwa mnajiuliza nani anawajibika kwa hili, mimi ndio nawajibika”.


Obama hakuishia kukubali tu makosa na kukiri udhaifu wa vyombo mbalimbali vya serikali alienda mbali zaidi na kuongeza muda wa kuzuia utafutwaji mafuta kwa miezi sita na kuzuia makampuni 33 kufanya uchimbaji wowote kule; pamoja na hilo mkuu wa kitendo cha utawala wa mambo ya majini alikuwa amejiuzulu siku ile ile Obama alipozungumza na waandishi wa habari. Kwa ufupi, huu ni mfano wa mwitikio sahihi unaopaswa kuoneshwa na Rais Kikwete leo. Kwamba, suala la mgomo wa madaktari ni suala ambalo yeye alitumaini kuwa lingeweza kumalizwa mara moja na bila kuhatarisha maisha ya Watanzania lakini alikosea kufanya hivyo na anawajibika kwa yote yaliyotokea; siyo Mponda, siyo Nkya, siyo madaktari wala siyo Waziri Mkuu bali yeye.


Halafu Mponda na Nkya wajiuzulu?


Sasa hawezi kuwajibika na kuacha vitu vibakie vilivyo – itakuwa haina maana. Kuwajibika kwa Rais ni lazima kuwe na matokeo. Nyerere alipokuwa anazungumzia suala la kuwajibika kwa Waziri Mkuu Malecela kwenye sakata la “Hoja ya Tanganyika” alisema kanuni muhimu tu kuwa haiwezekani kila wakati kuna makosa basi Rais anawajibika lakini Rais anapowajibishwa Waziri wake lazima awajibike. Nyerere hakutaka Mwinyi aondolewe kwa udhaifu aliouonesha lakini Waziri Mkuu wake ilimpasa awajibike – hata kama ni kwa sababu ya udhaifu wa Rais. Katika hili linaloendelea ni lazima viongozi kadhaa wa serikali wawajibishwe permanently!Hii ina maana – na nimatumaini yangu – kabla Rais Kikwete hajazungumza na wazee wa CCM jijini Dar na kupitia kwao kuzungumza na taifa Waziri Mponda na Naibu wake Nkya watakuwa wamekubaliwa kujiuzulu. Hili ni jambo muhimu sana kwa sababu hatua yoyote yenye kudhania kuwa wanaweza kuendelea madarakani baada ya madhara yote haya ya sifa, hadhi na heshima yao ni kuwadharau Watanzania.


Hoja ya “kubingirika” hawa wakiondolewa haina msingi


Kwa siku hizi chache nimewasoma wengi ambao wamekuwa wakirudia mojawapo ya makosa (fallacies) kubwa za hoja yaani ile ya kudai “kama tukikubali kwa huyo itakuwa ni mwanzo wa kukubali kwa wengine”. Wenye kutoa hoja hoja hii wanataka watu waogope Rais kushinikizwa hadi kuwaondoa mawaziri kwani akifanya hivyo basi makundi mengine nayo yanaweza kuja na mashanikizo kama haya! Wanaotoa hoja hii wanafikiria wanasema kitu kizito kweli – wanaamini Mponda na Nkya wasiondolewa kwa shinikizo kwani kwa kufanya hivyo mawaziri na viongozi wengine wataondolewa kwa shinikizo! Ni hoja dhaifu sana kiakili.


Kwanza, kwa sababu hadi hivi sasa madai ya kuondolewa kwa Mponda na Nkya hayatolewa kiholela bali yanahusiana na utendaji wao na maamuzi yao kwenye wizara hii na si kwingine. Mawaziri na viongozi wengine watawajibika kwa mambo yao kwenye ofisi zao. Hakuna uhusiano wowote wa kuwashinikiza hawa na kuwashinikiza wengine. Uwezekano wa kutokea hili ni sifuri. Katika elimu ya ujengaji hoja ulaghai huu unafanana sana na kile kinachoitwa “fallacy of conjunction” yaani kama Wikipedia inavyotafsiri kuwa ni “logical fallacy that occurs when it is assumed that specific conditions are more probable than a single general one.


Pili, kama kutakuwepo na viongozi wengine wabovu au wasiotenda inavyopaswa wananchi wanayo haki ya kulalamika na kama wanaopaswa kuwawajibisha wakisuasua basi wananchi wanaweza kuweka shinikizo jingine. Kwa ufupi ni kuwa hakuna kosa kwa wananchi kushinikiza viongozi wabovu kuondolewa; kubwa linalotakiwa ni viongozi kuonesha uadilifu na weledi ili wananchi wasisukumize kuondolewa kwao.


Hivyo, leo ni siku ya majaribio; ni majaribio kwa mtu mmoja tu naye ni Kikwete. Leo ana uamuzi wa kulionesha taifa uongozi au anauamuzi wa kuonesha taifa kuwa bado hajabadilika na hajaelewa uzito wa kuwa Rais! Leo tutashuhudia Kikwete ni kiongozi wa namna gani; je anapenda kutumia ofisi yake kulazimisha mambo au anaweza kutumia nafasi yake kushawishi mazuri kufanyika? Leo tutashuhudia kama Kikwete kama kiongozi anaweza kuwajibika yeye mwenyewe – bila kisingizio – kwa yote yaliyotokea au leo atajitahidi kwa nguvu zake zote – kama alivyofanya mwaka 2010 – kuwademonize madaktari ili tu kutetea viongozi wabovu?


Leo tutapata jibu – je Kikwete anaweza kuonesha njia au kuongeza giza? Kwani kama baada ya kikao chake cha wazee wa CCM kutakuwepo na mgomo mkubwa zaidi basi jibu litakuwa wazi zaidi kwa kila Mtanzania kuwa Kikwete ameshindwa kuongoza. Kwani, endapo mgomo mkubwa zaidi utatokea nchini kwa sababu ya kutoamua sahihi leo hii basi tusije kushangaa tutakachoshuhudia leo hii itakuwa ni kwa Rais Kikwete kuanza kujichimbia shimo la kisiasa ambalo yeye mwenyewe atashindwa kujitoa. Asipofanya sahihi leo – Kikwete atawajibika kweli kweli yeye mwenyewe.
Kwa kujiuzulu.


JAMII FORUMS


Update
Kikao cha wazee wa Dar es salaam na mheshimiwa Rais kimesogezwa mbele ili kupisha mazungumzo baina ya madaktari na Serikali

No comments: