Thursday, February 9, 2012

WANAPENDA KUPENDWA SI KUPONDWA HATA WAKIPONDA WENYEWE

Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.

Mpenzi Frank,

SAMAHANI mpenzi maana inawezekana nitashindwa kukuandikia vizuri wiki hii maana tangu mwenzie atupiwe mawe, Bosi amekuwa na hasirahasira za kila wakati.

Hivyo anapokuhitaji usipofika hata kabla hajamaliza kukuita anaamini umejiunga na wapinzani. Yaani ujinga mtupu lakini wanene ndivyo walivyo. Sheria zatuhusu sisi haziwagusi wao. Wanapenda kupendwa si kupondwa hata wakiponda wenyewe.

Lakini Binti Bosi kama kawaida hajali vimbunga na vimbwanga vya baba yake. Sijui amekula kiapo kwamba lazima amchokoze baba … au ndio ujana wenyewe … lakini ujue kabisa kwamba iwapo Bosi anaashiria kushoto, yeye ataenda kulia.

Kwa kweli nashangaa kidogo maana hata Bosi anavyosema, mbona watoto wengine wa waheshimiwa hawapingi madingi na badala yake wanataka kutumia jina la mshua wao kujineemesha wenyewe.

‘Huoni mwanangu wengine wanavyofanya? Kuna faida gani mimi nihangaike kukaa kwenye meza ya wenyewe kama wewe hauko tayari kutumia hiyo nafasi?’

‘Kwa nini nitumie baba? Kwanza nataka kujiendeleza kwa nguvu zangu mwenyewe kama wewe ulivyofanya ukiwa kijana. Na pili, unajua kama akili za mtu ziko kwenye kula tu haoni hatari iliyoko mbele. Hata kama maafa yanatokea kwa majirani, wanadhani haiwezi kutokea kwao.’

‘Ah, upuuzi mtupu!’

‘Siyo upuuzi baba. Nakuambia kila siku kwamba watu wamekasirika. Wamechoka. Wanaweza kuimba nyimbo za kukusifu huku kimoyomoyo wanakulaani.’

‘Sikiliza kapinzani kangu, hakuna serikali isiyochokwa duniani. Lakini sisi tunajua jinsi ya kujiimarisha hadi hakuna wa kutugusa.’

Siku ile BB aliamua kunyamaza maana nadhani aliona kujaribu kumwelewesha baba yake ni sawa na kuhutubia ukuta. Na kweli. Kila mahali watu wanalalamika, wanalaani, lakini walioko mbinguni hawaoni kabisa. Badala yake wanazidi kufanya mambo ya kuwakasirisha watu zaidi, eti wao si binadamu kama binadamu wengine.

Lakini baada ya mwenzie kutupiwa mawe, Bosi alikasirika sana. BB alimchokoza kama kawaida.

‘Si nilikuambia baba.’

‘Hawa ni wahuni tu. Kama vijana wengine chokoraa walioanza kuimba ‘POSHO … WIZI … POSHO … WIZI … POSHO … WIZI’ nilipopita.

Unajua mpenzi ilibidi mimi niiname haraka kuangalia vumbi chini ya zulia ili nisionekane nacheka lakini BB alishindwa kujizuia, na alivyopasuka kicheko, na Bosi alipasuka hasira.’

‘Unacheka nini pumbaf?’

‘Si nilikuambia baba. Wakati nyinyi mnazunguka kwenye maghorofa ya juu, hamjui mawazo ya watu walioko chini. Hata mkijitetea namna gani, hakuna watakaowaelewa. Kwa kweli nakumbuka somo letu la historia. Huko Wafaransa walipokasirika kukosa mkate kwa sababu bei ilikuwa juu, mke wa mfalme alisema …

Na hapo BB aliigiza sauti ya mwanamke

‘Kama wamekosa mkate si wanunue keki tu’. Watu waliposikia hivi walizidi kukasirika hadi mapinduzi yakatokea.’

‘Wewe na mifano yako. Watu hawajakosa mkate hapa. Tena tunawapatia mkate wa dezo kabisa …’

‘Katika sherehe zenu? Huku si kuwapa mkate bali takrima zilezile. Na nikishiba leo lakini sina uwezo wa kula kila siku haisaidii.’

‘Ah, wewe kweli una matatizo ya akili. Kila kitu kukosoa, kila kitu kukosoa. Hata tunapotaka kusherehekea na watu, unaiita hongo ….’

‘Hapana baba, sikusema miye. Umesema mwenyewe.’

Bosi akashtuka kidogo kana kwamba amejishtaki mwenyewe. Hivyo BB aliendelea.

‘Ni kama mnene mwenzio anavyoanika hadharani, kumbe mchezo wote wa gamba ni kuwasahaulisha watu. Mwisho wa siku mambo yataendelea kama kawaida. Yaani anasema hadharani kwamba mnatumia mbinu chafu za kuwadanganya watu.’

‘Si chafu. Ni mbinu ya kisiasa.’

‘Bado chafu. Na nashangaa kwamba mnapenda kuiga kwa wakoloni walewale mliowalaani kwa mbinu zao chafu wakati wanatutawala.’

‘Dunia imebadilika. Sisi tunajua hakuna chama ambacho kinaweza kuongoza vizuri kama sisi. Ndiyo maana watu wakielewa vibaya, lazima kutumia mbinu ili wahuni wengine wasitumie hii nafasi.’

‘Lakini baba, kama mnaamini kwamba hakuna chama kinachoweza kuongoza vizuri kama nyinyi, kwa nini mtumie mbinu chafu? Kwa nini mlazimishe? Waachie wananchi waamue.’

‘Nadharia tu. Wananchi hawana akili mara nyingine. Wanadanganyika kirahisi.’

BB alimwangalia baba yake mdomo wazi.

‘Umesemaje baba?’

‘Umesikia. Wananchi hawana akili! Wewe si unajidai msomi wa historia. Mara ngapi wananchi wameswagwa na mihemko kuwachagua wasiofaa kabisa.’

‘Nahisi elimu mbovu ni sababu mojawapo ya hiyo. Elimu yetu haitufundishi kutafakari. Ndiyo maana mnafanya mpendavyo. Sasa, kutupa mawe sijakubali lakini uniambie wale vijana walikosea kitu gani kukasirikia matumizi ya magari ya serikali?’

‘Wana mawazo mafupi kama birikumu. Gari ni gari. Serikali ni serikali yetu. Ni mke wetu lazima itutumikie. Itupikie na ituletee chakula maana sisi ni Bwana wa serikali.’

BB akakunja uso.

‘Baba wewe ni mzima kweli leo?’

‘Ndiyo mimi ni mzima kabisa. Ni hawa wazimu wasio wazima.’

‘Lakini hatuko katika enzi za chama kimoja. Lazima pawe na mpaka kati ya chama na serikali.’

‘Mpaka gani? Nakuambia, tutatumia serikali kuwasambaratisha vipinzani vyote. Ifikapo mwaka 2015 utaona! Ndiyo maana kama uliamua kuangalia sherehe yetu, uliona maSTK kibao. Hatuwezi kutishwa na vihunihuni vile. Pamoja na vijidaktari. Vyote vihuni tu.’

Kwa mara ya kwanza niliona BB ameduwaa hadi alishindwa hata kumjibu baba yake. Kweli hasira hasara maana Bosi alikuwa anamwaga sera yake ya kweli kabisa badala ya kutafuta maneno lainilaini ya kujifanya mpenda demokrasia. Bosi kuona ukimya huo alidhani BB hatimaye amesalimu amri hivyo akazidi kutamba.

‘Na hakuna wa kutuzuia. Sisi tumekuwa chama cha POKWA, yaani posho kwanza, hivyo wakiamua kutuudhi kuhusu posho zetu halali kabisa, hapiti mtu, haupiti muswada.’

‘Lakini baba …. Baba … mbona hivyo baba?’

‘Mbona nini? Tumechoka kuchafuliwa na viinzi. Tuna dawa kibao ya kuwaua wadudu na tutawaua. Mtu ajifikirie yeye mwenyewe kwanza si wengine. Wengine wanakula maisha ya mbinguni sisi tunahenya na viposho vya kijinga kabisa.’

BB alishindwa kuvumilia maana, ingawa anampinga baba yake kuhusu mambo mengi, bado anampenda. Sasa huu msimamo wa Bosi uliojaa hasira ulimwumiza hadi akajikuta anaangua kilio na kukimbilia chumbani. Bosi alishangaa.

‘Sasa huyu nini tena?’

Lakini Mama Bosi aliogopa hata kusema. Hivyo walimaliza kula kimyakimya kisha MB naye akaenda kulala na kumwacha Bosi akibugia wiski peke yeke. Mpaka akaanza kuongea peke yake.

‘Washenzi. Watanitambua. Eti posho ni wizi. Watakiona … watatambua nani ni watawala hapa na nani wa kuliwa.’

Unasikia hayo mpenzi. Sasa tufanye nini kama watu wanaotakiwa kuongoza kwa kusikiliza na kujirekebisha wanaendelea kufanya jambo baada ya jambo kujipendelea tu na kutuacha hoi? Kama hawatusikilizi na kuzidi kutukandamiza na hata kufanya vitendo vya uhalifu na vya kuvunja sheria hivihivi tu, sisi tufanye nini?

Sijui mpenzi wangu, sijui. Ila kichwa kinawanga kabisa. Watu wanapoonyesha ufisi wao ndani ya ngozi ya kondoo, kweli inashtua.

Akupendaye daima. Njoo unichukue mapema mume wangu mtarajiwa maana mwenzio nimebwagwa ndani ya kundi la mafisi.

Hidaya
RAIA MWEMA

No comments: