Tuesday, February 21, 2012

RUANGWA YAKOSA FEDHA ZA MAENDELEO

Abdallah Bakari, Lindi

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, imekosa ruzuku ya fedha za maendeleo ya sekta ya kilimo kwa mwaka wa fedha wa serikali 2011/12, ilifahamika.

Akiwasilisha taarifa ya kilimo katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Lindi, mshauri wa kilimo wa mkoa huo, John Likango alibainisha kuwa moja ya changamoto ya utekelezaji wa miradi ya kilimo katika mkoa huo ni pamoja na Wilaya ya Ruangwa kukosa fedha za kutekeleza miradi ya sekta ya kilimo (Dadps) kwa mwaka 2011/12.

Alisema hatua hiyo imefikiwa na Serikali kama adhabu, baada ya watendaji wilayani humo kushindwa kujibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali juu ya matumizi ya Sh45 milioni katika idara ya kilimo.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Issa Libaba alikiri halmashauri yake kutotekeleza mradi wowote wa kilimo kwa mwaka huu, kutokana na kukosa fedha za ruzuku za maendeleo katika idara hiyo nyeti kulikosababishwa na watendaji wake kushindwa kujibu hoja za ukaguzi.

“Tulitarajia tupate Sh429 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya kilimo wilayani kwangu, lakini kutokana na hoja hii hadi sasa hatujapata kiasi chochote cha fedha, tumeambiwa fedha hizo hatuwezi kupewa hadi hoja za ukaguzi zitakapojibiwa” alisema Libaba

Aliongeza kuwa “Sisi tunaendelea na utaratibu wa kuwachukulia hatua wale wote waliohusika, siku ukisikia mheshimiwa mwenyekiti (Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila) tunakuletea watendaji wako, wala usishangae, sisi hatuwezi kukaa nao tena”

Libabe huku akionekana mwenye kukerwa na tukio hilo alisema “Halmashauri yangu ilifukuzwa kwenye kikao cha Alat Taifa (kamati ya Bunge ya hesabu za Serikali za Mitaa), ni aibu tupu, wahusika watakapobainika basi hatutasita kuchukua hatua”
MWANANCHI.

No comments: