Thursday, February 9, 2012

POLISI WALINISULUBISHA BILA HATIA SASA NI MLEMAVU MILELENa Salum Maige


SIKU ya Jumatano Agosti 12, mwaka 2010, haiwezi kusahaulika maishani mwa John Shauri (48)mkazi wa Mtaa wa Mission Kata ya Nyampulukano, jijini Mwanza. Pengine ni miongoni mwa siku mbaya kuliko zote katika maisha yake.

Siku hiyo ya balaa, ilimkuta Shauri, akiwa mwenye afya na akiendelea na shughuli zake za kujitafutia riziki. Lakini ilipofika saa 6:00 mchana, fundi baiskeli huyu alipatwa na ugeni usio wa kawaida.

Ugeni huo ulikuwa ni wa polisi, ambao walimpasha habari ngeni mno masikioni mwake.

“Polisi waliniita pembeni kama hatua 10 hivi kutoka sehemu yangu ya kazi, na ghafla polisi wengine nao walifika,” anasimulia Shauri

Polisi hao walimwomba aende nao kituoni akamwone Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Sengerema. Alipofika huko aliulizwa kama yeye ndiye John Shauri naye akakubali. Kisha wakamuuliza umri wake na kabila.

“Wakati huo nilimsikia mkuu wa kituo akiagiza kuwa mtu anayeitwa Haruna Yusuph, akakamatwe na mimi nifungwe pingu,” anasimulia.

Alipofika Haruna ambaye ni mtuhumiwa mwingine kwa pamoja walifungwa pingu na gari la polisi lilifika katika kituo hicho na wakapandishwa ndani ya gari na safari ya kuelekea nyumbani kwake ikaanza.

“Tulipofika kwangu, majirani zangu, Sued Mashauri na Daniel Best nao walikamatwa kama mashahidi wakati upekuzi unaendelea,” anasema Shauri.

Kabla ya kufanya upekuzi huo, polisi walimwambia Shauri kuwa, wamemkamata kwa kuwa wamehakikishiwa kuwa yeye(Shauri) anamiliki silaha.

Polisi hao walipoingia ndani walifanya upekuzi kila sehemu wakianzia kwenye chumba chake cha kulala wakachukua panga na kifaa cha muziki cha amplifire ambacho kilikuwa kibovu.

“Wakiendelea kusearch, (kupekua) waliingia hadi katika banda la mifugo ambako baada ya kuona unyevunyevu waliomba jembe wachimbe ingawa hawakuona kitu,” anasema.

Shauri anaeleza kuwa, baada ya kukosa walichokuwa wanahisi, wakaanza kumhoji kwa nini anamiliki jembe na ‘amplifier’ swali ambalo anadai, lilikuwa gumu kwake.

“Baada ya polisi hao kunihoji wanitaka kupanda tena kwenye gari, safari hii ahata mke wangu na kijana aliyekuwa anasimamia shughuli zangu..tulipelekwa hadi kituoni’’ anasimulia huku akiugulia maumivu,” anasema.

Shauri anasema alipofikishwa kituoni, Yusuph na mke wake walipelekwa mahabusu wakati Shauri alipelekwa moja kwa moja katika chumba cha mateso. Anaongeza kuwa, wakati huo ilikuwa ni saa 9:00 alasiiri.

Mkuu wa upelelezi alimwamuru akae chini huku akiwa amefungwa pingu mikononi, bomba la chuma likapitishwa chini ya miguu yake na kuanza kunyanyuliwa.

“Wakati huo nilikuwa naumia sana, lakini walikuwa wakilazimisha nitaje silaha ninazo miliki,” anasema na kuongeza:

‘’Nikiwa kwenye chumba hicho cha mateso chini ya polisi wawili na mkuu wa upelezi,kabla ya kuanza kunisulubu akaitwa kijana mmoja Joseph Masala aliyekuwa mahabusu….naye alikuwa amepigwa sana akaulizwa kama ananifahamu, alisema hanifahamu, lakini baada ya jibu hilo akapigwa kofi’’ anasema Shauri.

Anasema baada ya kijana Masala kupigwa kofi aliulizwa kwani ni nani tunayemtafuta akawa amewajibu ni John Michael, walimgeukia na kusema unajifanya mjanja na kisha wakamkamata Shauri na kumnyanyua juu kwa kumning’niza kichwa chini.

Baada ya kitendo hicho alianza kupigwa marungu bila huruma huku mtekelezaji wa kitendo hicho akiwa ni ofisa mwandamizi wa polisi.

Anasema polisi walimpiga kwa zaidi ya saa mbili, kisha alishushwa chini kutoka sehemu aliyokuwa amening’inizwa na kuambiwa asimame, ingawa hakuwa na uwezo kutokana na magoti kuvunjika.

“ Miguu yangu ilikuwa imevunjika damu nyingi zilinitoka sehemu za magoti na nilikuwa nahisi kufa kwa maumivu niliyokuwa nayo,’’anasema huku akibubujikwa na machozi.

Anaeleza kuwa aliposhindwa kusimama walimfungua pingu na kumpekua mfukoni, wakachukua Sh26, 000 na betri moja ya simu kabla ya kumburuza kama mzoga hadi mahabusu.

Hata hivyo, saa moja jioni walimpeleka katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema kwa matibabu huku polisi aliokuwa ameambatana nao wakitoa taarifa kwamba Shauri ni jambazi na majeraha yake wamempiga risasi miguuni.

‘’Nilipofikishwa Hospitali niliingizwa kwenye chumba cha upasuaji nikashonwa sehemu zilizokuwa zimeharibika nikalazwa wodini..siku ya pili nikapimwa X-Ray ikaonekana kuwa mifupa katika sehemu ya magoti imesagika na nikashauriwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi," anasema.

Disemba 3, mwaka jana siku ambayo mke wake na kijana wa kazi waliachiwa huru Shauri alipelekwa na polisi katika Hospitali ya Bugando kwa uchunguzi zaidi akiwa na hali mbaya kwani alikuwa amepoteza fahamu.

Akiwa Bugando Shauri alifanyiwa upasuaji na kuondoa vifundo vyote vya magoti kwa sababu zilikuwa zimeharibika vibaya na hazifai tena.

Baada ya kumsulubu kwa makosa yasiyo yake, polisi hao walimtelekeza na tangu wakati huo hawajawahi kumfuatilia tena.

Dk Vicent Rugereka Mganga, wa Hospitali ya Sengerema anasema vifundo vya magoti ya Shauri vimeharibika haviwezi kurejeshwa tena.

"Shauri hawezi kupona tena, kwa sababu yale majimaji ya kwenye magoti hayamo tena hiyo hali ndiyo inayosababisha apate maumivu na asiweze kukunja miguu kwa maana majimaji yale ndiyo yanayosaidia mguu kukunja na kunyosha, kwa hiyo huyu amekuwa mlemavu na anahitaji msaada mkubwa,’’anasema Dk Mganga.

Baada ya kuona hapati msaada kutoka jeshi la polisi Shauri aliandika barua ya malalamiko kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Mwanza,wakili wa serikali na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Hata hivyo, Ofisi ya Wakili wa Serikali na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora walimjibu huku mkuu wa upelelezi makosa ya jinai wa Mkoa akieleza kuwa anafanya uchunguzi wa tukio hilo ikiwamo kuagiza majina ya polisi waliohusika katika tukio hilo.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi la polisi Wilya ya Sengerema zinaeleza kuwa orodha ya majina ya watu waliohusika haikufanyiwa kazi na badala yake polisi hao walihamishiwa vituo vingine vya kazi.

Katika kuonyesha kuwa jeshi la polisi lilifanya makosa ya kumkamata Shauri, Jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza limeeleza kuwa kulifanyika makosa aliyekuwa anatafutwa na polisi ni John Michael na sio John Shauri.

Shauri anasema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliagiza uchunguzi ufanyike haraka na majina ya watuhumiwa, waliohusika yapelekwe kwenye tume hiyo ingawa hadi sasa hana taarifa hatua zilipofikia.

Kilio cha Shauri ni haki itendeke. Kwani hivi sasa yeye amepata ulemavu wa kudumu. Lakini pia, anahitahi msaada wa kiuchumi, matibabu na fedha za kuitunza familia yake.

Kutokana na ulemavu alionao Shauri anasema ameadhirika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa yeye ni tegemeo katika familia yake ya mke na watoto wawili Samweli John[19]na Magdalena John [27]ambao wote kwa pamoja wameshindwa kuendelea na masomo baada ya baba yao kuwa mlemavu.

Shauri anasema anahitaji msaada wa aina mbili, kwanza serikali itoe msaada wa kisheria ili waliohusika kumtendea unyama huo wachukuliwe hatua kwa kuwa alipigwa bila hatia na wala hachukuliwa maelezo ya kipolisi ya kumpeleka mahakamani.

‘’Msaada mwingine ni wa kujikimu kimaisha kutokana na kwamba sina uwezo tena wa kujishughulisha na kazi yoyote kwa kuwa hata kutembea natembea msaada wa magongo…hadi sasa nimeshindwa kuhudhuria klinki kwani nadaiwa shilingi 375,000 katika hospitali ya rufaa Bugando,’’.


MWANANCHI

No comments: