Saturday, February 18, 2012

KUFELI HUKU NI JANGA LA TAIFA SI SUALA LA WAKRISTU VS WAISLAMUWAKATI mwingine natamani ningekuwa na uwezo wa kuwatia bakora baadhi ya watu wanaozungumzia suala la maelfu ya wanafunzi kufeli vibaya katika mtihani wa kidato cha nne.

Watu wanaoniudhi na kunikera ni wale ambao wanayaangalia matokeo haya ya mtihani kama ni suala la ubora wa shule za “Kikristu” kulinganisha na shule za “Kiislamu” au wale wanaoona “kupendelewa kwa Wakristu” na “mfumo Kristu”.

Mwitikio wa baadhi ya watu kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha nne kwa kweli unanifanya nijiulize kama udini umezama kati yetu kiasi kwamba hatuoni kilichotokea na kinachotokea katika elimu ni nini.

Ndugu zangu, kuna janga katika sekta ya elimu ambalo linasababisha maelfu ya watoto wetu, wadogo zetu, ndugu zetu kuachwa nje ya elimu! Jamani, hawa maelfu wanaofanya vibaya si Waislamu, si Wakristu, si Wapagani hawa ni Watanzania!

Kwa upande wa Wakristu

Kuna baadhi ya Wakristu ambao wanapoangalia matokeo ya mitihani wanajisikia vizuri kwamba watoto wenye majina ya Kikristu wanaonekana kuwa wamefanya vizuri.

Tena wengine wanajisikia vizuri wanapoona majina ya shule zilizofanya vizuri mengi yanahusiana na Wakristu na hivyo kuthibitisha ile imani kwamba shule za Kikristu ni bora. Sasa, jambo moja liko wazi sana kwamba shule za Kikatoliki – si shule za majina ya Kikristu tu -karibu sehemu zote duniani zinatoa elimu ya kipekee na bora zaidi.

Hilo ni kweli India, China, Pakistani, Uingereza, Marekani na hata Indonesia. Kuna sababu ya hilo na si kusudio langu kuingia kwa undani kwenye sababu hizo. Sasa huu ni ubora unaotokana na mfumo wa elimu ya Kikatoliki pote duniani na hili halikuanza jana au juzi. Kanisa Katoliki lina historia ya muda mrefu katika masuala ya elimu mbalimbali huko Ulaya na baadaye katika makoloni ambayo yalichukuliwa na nchi za Ulaya.

Nimesema hili ili kusiwe na hisia kuwa ni shule za Kikatoliki za Tanzania ndizo zinafanya vizuri zaidi. Wale wanaowaaminisha watu kuwa shule za Kikatoliki za Tanzania zinafanya vizuri zaidi kwa sababu “zinapendelewa” hawawatendei haki wasikilizaji wao.

Mtu anaweza kwenda Kenya, Zambia, Uganda, Nigeria au nchi yoyote ambayo ina mfumo wa shule za Kikatoliki na ataona kuwa shule hizi zinafanya vizuri zaidi na mara nyingi kuliko shule nyingine binafsi au za serikali.

Lakini si watoto wote wa Kikristu wanasoma shule za Kikristu! Si Wakatoliki wote hupeleka watoto wao kwenye shule za Wakatoliki kwanza kwa sababu zina gharama ya juu na vile vile kwa sababu ni chache na zina uchaguzi wa hali ya juu sana.

Hii ina maana ya kwamba bado kuna Wakristu (Wakatoliki na wengine) ambao wanapeleka watoto wao kwenye shule hizi hizi za umma. Maelfu ya hao waliofeli kwa mara nyingine ni Wakristu vile vile na hivyo huku si kufeli kwa watoto wa Kiislamu peke yake kama watu wengine wanavyochukulia.

Kwa Waislamu

Wale Waislamu ambao wanaangalia suala hili kama ni mashindano ya “sisi dhidi ya nyinyi” hawawatendei haki watoto wa Kiislamu nchini. Kuwaambia au kuwafanya watoto waamini kuwa wamefeli kwa sababu ni Waislamu ni kuwaonea, kwani hao watoto wanajua – kama wanatazama vizuri – kwenye shule hiyo hiyo waliyofeli wao watoto wengine mamia wa Kikristu nao walifeli!

Hawa Waislamu wanaofikiria kuwa Wakristu wote nchini wanapata elimu nzuri, wanapata kazi nzuri na wanaishi maisha yenye utu na kuwa Waislamu wote hawajasoma na hawana nafasi yoyote ya maana na kuwa hakuna Waislamu wengine wanaofanya vizuri kwenye mitihani, hawautendei haki ukweli.

Sote tunajua wapo Waislamu ambao wamefanikia na wanaendelea kufanikiwa kwa kila kipimo; wapo wafanyabiashara, wasomi, walimu, madaktari n.k ambao ni Waislamu ambao wamesoma kwenye elimu hii ambayo Wakristu wengine wanapata. Sasa kufeli kwa baadhi ya shule za Kiislamu ni lazima kutafutiwe maelezo ya kisayansi kama vile kufeli kwa shule za Kata au shule nyingine binafsi kunavyohitaji maelezo.

Nitoe mifano kidogo

St. Mary ya Mbalizi huko Mbeya ni shule inayoonekana ina jina la Kikristu na sijui kama ni ya kanisa au mtu binafsi. Mtu mwingine anaweza kufikiria labda shule hiyo imefanya vizuri. Matokeo ya mtihani shule hiyo yanaonyesha kuwa waliopata daraja la 1 ni 0 waliopata daraja la 2 ni 0 waliopata daraja la tatu ni 1 na waliopata daraja la nne ni 38 huku 34 wakifeli. Huo mfumo Kristu umeshindwa vipi kuwasaidia hawa?

Shule nyingine inaitwa St. Margareti ya wasichana. Sasa kwa jina na kwa vile ni ya wasichana tena wengi wana majina ya Kikristu watetezi wa hoja ya “mfumo Kristu” wangeweza kutuonyesha kuwa shule hiyo wanafunzi wake wameshinda kwa kiwango cha seminari za kiume. Hakukuwa na mtoto yeyote aliyepata daraja la kwanza, la pili wala la tatu! Walikuwepo 27 wa daraja la nne na 28 wakifeli kabisa!

Shule nyingine ni St. Paul ambayo nayo kwa kuangalia haraka haraka tunaweza kuamini kuwa ni shule ya Kikristu na hivyo ingependelewa na mfumo “Kristu”. Wanafunzi wengi wana majina ya Kikristu lakini katika shule hiyo hakuna hata mmoja aliyepata daraja la kwanza, la pili au la tatu!

Sasa hii ni mifano michache tena ya haraka haraka tu kuonyesha kuwa wanaofeli si watoto wa Kiislamu tu na si katika shule zenye majina ya Kiislamu tu! Wanaojaribu kuelezea kufeli huku kwa misingi ya kidini hutawasikia wakiwapigania watoto hawa wa Kitanzania! Wao wameng’ang’ania “mfumo Kristu, mfumo Kristu” na hawa watoto walilie nini? Rais Muislamu? Makamu Muislamu? Ndipo maelezo ya kufeli kwao yatapatikana?

Tuvuke mpaka wa udini na kuliangalia tatizo letu kama letu sote

Ndugu zangu, muda wa kubebesha lawama za kidini tena za kijinga umepita. Watoto wetu wanafeli kila mwaka na sisi watu wazima tumekaa kama washirikina kukwepa kuelezea mambo yanayoelezeka kisayansi na badala yake tunatafuta maelezo mepesi yasiyoweza hata kushawishi akili za mtoto mdogo.

Wazazi wa Tanzania ni lazima wakasirike kuwa watoto wao wengi wanafeli na wanapoteza nafasi. Hivi tumewahi kujiuliza hawa watoto wote wanaofeli kila mwaka na wakakosa nafasi ya kuendelea mbele huwa wanaenda wapi? Hivi, tunafikiria wote wanaenda kwenye shughuli gani hasa? Hawa watoto wa kike ambao walijizuia na majaribu mbalimbali ili angalau wapate elimu ya sekondari wanapofeli nani anajali!?

Binafsi naomba niwe wa kwanza kutaka uongozi wote wa Baraza la Mitihani kujiuzulu na pamoja nao kufumuliwa kwa uongozi wa Wizara ya Elimu. Hizi sera za CCM zimekuwa janga la kudumu sasa na watu wetu hawachoki na hawakomi! Leo hii vile ambavyo vimekuwa aibu na fedheha kwa familia nyingi vimekuwa navyo ni aibu hadi Ikulu! Nani atatusadia?

Makundi ya Waislamu wanadai Wakristu wanapendelewa; Wakristu wanasema Waislamu hawapendi elimu. Lakini ukweli unabakia kuwa wanaofeli na kupoteza nafasi nyingi ni watoto wa Kitanzania, Waislamu, Wakristu, Wapagani na wasioamini kabisa!

Tufanye nini? Well, wapo wanaoangalia CCM na serikali yake kutafuta majibu. Hatuamini kuwa tunavuna tulichopanda; hatutaki kukubali kuwa haya ni matokeo ya kushindwa kwa sera za elimu pamoja na mipango yake yote!

Tunatumia mabilioni ya shilingi kila mwaka lakini tunazidi kufelisha kama tuna wazimu au tunashindana. Hadi inafika wakati watoto wanaandika mashairi ya bongo flava kwenye mitihani na watu bado wako na ofisi zao wakisubiri mwaka mwingine, hakuna hasira, hakuna kukerwa, hakuna kuchukizwa, inashangaza!

Hivi walimu na wenyewe kwa nini wasigome hadi mabadiliko ya kweli yaanze? Walimu wanaweza na wanapata wapi ujasiri wa kwenda darasani na kukuta shule isiyo na milango, madawati, vitabu na watoto ambao wamekosa chakula? Mwalimu anaweza kufundisha vipi mahali ambapo mtoto akirudi nyumbani hana cha kufanya zaidi ya kujipanga kucheza “Hakunaga”?

Hawa wazazi wanaoshabikia mtoto “anavyojua kucheza sana” wanafikiria watoto watafaulu kwa kuombea au kwa kuonea? Wazazi wangapi wanauliza kama mtoto kamaliza kazi na kufuatilia kuona amefanya kazi yake vizuri? Wazazi wenyewe ni nani anawasaidia kuweza kuwasaidia watoto maana si wazazi wote nao wana uwezo wa kusaidia watoto wao linapokuja suala la shule. Kama mzazi hakupata elimu yeye mwenyewe anaweza vipi kufuatilia elimu ya mtoto wake?

Labda sasa inabidi tufikirie kitu kingine nje ya CCM, nje ya sera hizi zilizoshindwa na nje ya watu hawa hawa. Tufanye nini? Tusaidie vipi? Au tukubali tu na kuombea labda mwaka ujao tutafaulisha zaidi kidogo. Twende tukaombee na kwenda kwa waganga tuone ni nani anatuloga! Maana kama hatutaki kutumia vichwa vyetu na uwezo wetu tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu kubadilisha maisha yetu hivyo ni bora tuanze kutumia uganga wa kienyeji!?

Vinginevyo, kuna kitu cha haraka, cha makusudi na kikali kinahitajika kufanyika ili kuokoa elimu ya watoto wetu. Lakini ili tuweze kufika ni lazima kwanza tukasirike. Mimi nimekasirika na nimekerwa. Sijui wewe mwenzangu unajisikiaje? Kama hujisikii hasira yoyote au kukerwa kwa namna yoyote, nina uhakika wewe ni sehemu ya tatizo!


RAIA MWEMA

No comments: