Tuesday, January 10, 2012

WANAFUNZI UDSM WAPIGA "KUNJI" (KUGOMA) WAKISHINIKIZA WENZAO WARUDISHWE CHUO.

Ellen Manyangu na Keneth Goliama,

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani (UDSM) jana walianza mgomo ili kushinikiza uongozi wa chuo hicho kuwarudisha wenzao 48 waliofukuzwa na kufutiwa usaili katika vyuo vyote vya serikali nchini.

Uamuzi huo ulichukuliwa kwa madai ya kuwasiliana na uongozi wa chuo hicho bila mafanikio wakati wakiangalia uwezekano wa kumaliza tatizo hilo kwa njia ya mazungumzo.

Wanafunzi hao walifukuzwa Desemba 13, mwaka baada ya kubainika kuwa walihusika katika matukio mbalimbali ya vurugu na uhalifu chuoni hapo.

Hata hivyo, mgomo na maandamano hayo yalifanyika katika mazingira mvutano huku baadhi wakipinge kwa maelezo uongozi wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso) umeshindwa kutoa muongozo unaotosheleza.

Wanafunzi wanaopinga mgomo walikuwa wakizomea na kuwataka viongozi wa Daruso kutoa muongozo jambo lililoonekana kuwa gumu ingawa kulikuwepo na kundi jingine lililokuwa linashawishi ufanyike.

Waliokubali kufanya mgomo walizunguka katika maeneo mbalimbali ya chuo hicho wakiimba nyimbo mablimbali huku wengine wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe wa kuwataka wenzao warudishwe na haki na sheria zizingatiwe.

Akizungumzia juu ya uhamuzi wa kuitisha mgomo huo, Waziri wa Mikopo Serikali ya Wanafunzi (Daruso), Daniel Naftali alisema huu ni wakati wa wanafunzi kuonyesha ushirikiano na kuona thamani ya wenzao waliofukuzwa kwani haki haikutendeka dhidi yao.

Alisema katika kikao cha Bunge cha Daruso kilichofanyika Jumamosi iliyopita kiliazimia kupitisha mgomo kwa kura 56 za ndio na 5 za hapana na azimio hilo liliafikiwa kwa dhumuni la kudai wanafunzi waliofukuzwa warudishwe kuendelea na masomo.

Alisema huu ni wakati wa kuungana na kujiita sisi sio mimi,kwani inafahamika kabisa kuwa baadhi ya wanafunzi waliofukuzwa walikuwa hawana mbio za kuwakimbia polisi na wengine walikuwa wakipita maeneo ya chuoni.
“Ni kweli vioo na vitu vingine viliharibiwa chuoni hapa lakini ni nani ana uhakika kama wanafunzi ndio wanaohusika na uharibifu huo kwani,katika zoezi la kukamata wapo watu wasio wanafunzi walikamatwa katiak eneo hili la chuo”alisema Naftal

Aliongeza kuwa lengo lao sio kuleta fujo wala madhara chuoni hapo bali ni wajibu wao kuhakikisha kila mmoja anapata haki ya kusoma kama zilivyo ainisha sheria za nchi.

“Tulifungua nafasi ya majadiliano kwa uongozi wa chuo kwa kipindi chote hicho lakini badala ya kuelewana na kufikia muafaka wa nini kifanywe juu ya wenzetu tumeambulia vitisho ambavyo haviana jibu lolote la wenzetu kurudishwa chuoni”alisema Naftal.

Naye naibu spika wa Bunge la Daruso Peter Arnold alisema taratibu zote za kisheria kufanikisha azimio hilo zifuatwe ili kuweza kufanikisha lengo.


MWANANCHI

No comments: