Wednesday, January 11, 2012

VIGOGO WAHOJIWA KASHFA YA UDAWAMO KIMBISA, DK MASABURI NA IDD SIMBA, RIPOTI YAKE KUTOKA KARIBUNIPatricia Kimelemeta,

SAKATA la uuzaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), limezidi kupamba moto baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Utouh, kuwataja vigogo wapya waliohojiwa na shirika lake kutokana na kutajwa kwamba walishiriki katika mchakato wa uuzaji wa hisa za shirika hilo.Akizungumza na Mwananchi jana, Utouh aliwataja vigogo hao ambao alisema baadhi wameshahojiwa kuwa ni Mwenyekiti wa Bodi, Idd Simba na Mkurugenzi wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena.

Vigogo wengine ambao Utouh alisema wanatarajiwa kuhojiwa wakati wowote ni Meya wa jiji la Dar es Salaam Dk Didas Masaburi na mtangulizi wake, Adam Kimbisa pamoja na Meneja Mkuu wa UDA, Victor Milanzi.

“Sisi hatufanyi kazi kisiasa, tunafuata sheria na taratibu zote zinazotakiwa katika kufuatilia suala hilo. Hivyo basi, lazima tuwe makini kwa kujiridhisha na taarifa inayotolewa," alisema CAG.

Utouh alisema ili ripoti hiyo iweze kukamilika na kuondoa hofu ya kumwonea mtu, wahusika wote waliotajwa kwenye sakata hilo wanapaswa kuhojiwa.

Agosti 13 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Keptein mstaafu George Mkuchika, alitekeleza agizo la waziri mkuu na kumpa CAG barua ya kufanya ukaguzi wa UDA ndani ya mwezi, lakini sasa ni zaidi ya miezi minne matokeo hayajatoka.

Hata hivyo, CAG Utouh akizungumzia sababu za kuchelewa kwa uchunguzi huo aliema; “Tulitaka kutoa nafasi kwa watuhumiwa kupata fursa ya kujitetea."

Utouh alifafanua kwamba, lengo hilo la kutenda haki ndilo lililofanya ofisi yake kuwahoji wahusika wote waliotajwa kushiriki kwenye mchakato huo ili ripoti itakayotoka isiwe ya kumwonea mtu.

Aliongeza kwamba kutokana na hali hiyo, wanaamini kuwa kukamilika kwa ripoti hiyo, kutaisaidia serikali kutoa uamuzi sahihi kuhusu sakata hilo na kuwaachia wale ambao wanaweza kuingizwa kwa makusudi kutokana na tofauti zao za kisiasa.

Utouh alifafanua kwamba, hadi jana Kampuni ya KPMG iliyopewa jukumu la kufanya ukaguzi huo, ilikuwa ikikamilisha ripoti yake ambayo, wanaamini inaweza kutolewa mwishoni mwa mwezi huu na kuikabidhi serikalini kwa ajili ya hatua zaidi.

Sakata lilivyokuwa
Serikali ilibaini kuwepo kwa ukiukwaji wa kisheria katika uuzaji wa UDA Agosti mwaka jana, jambo ambalo lilisababisha kuundwa kwa tume ya uchunguzi.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliagiza kuunda tume ya kuchunguza sakata hilo huku akizitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na CAG, kuchunguza mchakato mzima wa uuzaji wa hisa za shirika hilo kwa kampuni hiyo ya Simon Group Limited.

Habari ambazo Mwananchi limezipata zinadai kuwa tayari Takukuru pia walishawahoji baadhi ya watu kuhusu suala hilo.

UDA lilikuwa linamilikiwa kwa pamoja kati ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali Kuu, kupitia Hazina, wakiwa na jumla ya hisa milioni 15, kila hisa moja ikiwa na thamani ya Sh 100. Mchanganuo wa hisa za UDA unaonyesha kuwa, halmashauri ya jiji la Dares Salaam ilikuwa inamiliki asilimia 51 na Hazina asilimia 49 za hisa hizo. Hata hivyo, Februari 11 mwaka jana, bodi ya wakurugenzi ya UDA, chini ya Idd Simba, ilikutana na uongozi wa Simon Group ikiongozwa na Kisena na kusaini mkataba, ambao ulithibitisha kwamba UDA ilikuwa imeiuzia Simon hisa milioni 7.8 sawa na asilimia 52.6 ya hisa zote kwa thamani ya Sh bilioni 1.142.

Kwa mkataba huo, Simon Group ingekuwa mwanahisa mkubwa katika umiliki wa UDA kwa vile Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Hazina, wangebaki na hisa milioni 7.7, ambazo ni sawa na asilimia 47.4.


Baada ya mkataba kusainiwa, kipengele cha kwanza kiliitaka Simon Group kulipa asilimia 25 ya fedha za ununuzi wa hisa za UDA , ambazo kati ya fedha jumla Sh bilioni 1.142, ni sawa na kutanguliza Sh 285.6milioni.

Fedha hizo zilipaswa kulipwa ndani ya siku 14, tangu kusainiwa mkataba huo ili kuufanya utambulike kisheria na ndipo, Simon Group ililipa fedha hizo siku hiyo hiyo.

Ndani ya Bunge

Uuzwaji wa UDA ulitikisa Mkutano wa nne wa bunge baada ya wabunge kutaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika, huku wabunge wa mkoa wa Dares Salaam wakijikuta katika malumbano na Dk Masaburi.

Wakati mvutano huo ukiendelea, wamiliki wa Simon Group Ltd, walijitokeza hadharani na kuwaambia waandishi wa habari kwamba umiliki wake umekidhi vigezo vyote katika kumiliki Hisa ndani ya UDA.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Simon Group, Robert Kisena alisema kampuni yake ilifuata vigezo vyote vilivyotakiwa na kwamba imejizatiti kuliendesha Uda bila wasiwasi na kwamba hadi wakati huo walikwishawekeza kiasi cha Sh760 milioni.

Hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe nayo ilisema kuwa mkataba huo ni batili kutokana na fedha zilizonunua hisa husika kuwekwa kwenye akaunti ya kada wa Chama Cha Mapinduzi na mwanasiasa wa siku nyingi, Iddi Simba.

“Taratibu hazikufuatwa,na uamuzi wowote utakaofanyika ni batili kwa kuwa tayari sisi tumeshaanza mchakato wa kubaini kilichopo ndani ya mkataba huo ikiwa ni pamoja kumuagiza CAG na tayari Spika ana taarifa hizo,’’alisema Zitto.MWANANCHI

No comments: