Monday, January 16, 2012

TAMKO LA CHAMA CHA MADAKTARI TANZANIA BAADA YA KIKAO CHA DHARURA

Kikao cha mkutano mkuu wa dharura wa chama cha madaktari Tanzania (MAT) kilichofanyika leo siku ya jumamosi, tarehe 14/01/2012 ukumbi wa JAFFARY COMPLEX kimejadili kwa kina yafuatayo:

1. Kwamba, chama cha madaktari Tanzania kimejadili na kuazimia kutoa masaa 72 kwa serikali kuwa “Intern doctors” wote waliohamishwa warudishwe Muhimbili mara moja wakamalizie muda wao. Na kwamba ifahamike kuwa interns huomba kwenda kufanya internship katika hospitali fulani kutegemeana na malengo ya baadaye waliojiwekea. Na pili kuna baadhi ya vifaa vipo mf. Muhimbili na huko kwingine haviko. Madaktari wemesikitishwa sana na uamuzi huu kwa vile haieleweki ni kwa nini “intern doctors” waadhibiwe wakati walidai walipwe mishahara yao tu na serikali ilikiri kosa hilo. Wanachama wangependa kuona waliofanya uzembe huo wanawajibishwa mara moja na sio kuachwa waendelee kuwaadhibu madaktari wasio na kosa.

2. Kwamba, kwa kuwa Intern doctors wamekuwa wakifanya kazi bila malipo kwa muda mrefu na hali hiyo ikapelekea kusitisha kazi ndipo serikali ikaamua kuwalipa mishahara yao. Kufuatia kuendelea kusababisha adha kwa madaktari na wataalamu wengine wa afya na hatimaye kusababisha huduma mbovu kwa wagonjwa, Chama cha madaktari kimeona kimshauri Mh. Rais atafute ajira nyingine kwa ajili ya maafisa waandamizi wafuatao:

a. Katibu Mkuu, wizara ya Afya , Ms. Blandina Nyoni b. Mganga Mkuu wa serikali, Dr. Deo Mtasiwa

3. Kwamba waziri wa afya Dr. Hadji Mponda (MB) afute kauli yake inayoashiria kwamba “intern doctors” ni wanafunzi wa udaktari wa mwaka wa 5. Ieleweke kwamba ni madaktari kamili, waliohitimu mafunzo yao na kula kiapo rasmi cha udaktari. Na chama cha madaktari kimesikitishwa sana na upotoshwaji huuu wa mara kwa mara. Kutokana na hayo hapo juu basi chama cha madaktari Tanzania kina msamehe kwani inaonekana hajui atendalo. Ijulikane kwamba mjadala wa hivi ulishawahi kuibushwa mwaka 2005 na waziri wa afya kipindi hicho alikiri bayana kwamba intern ni daktari kamili aliyefuzu.

4. Kwamba, chama cha madaktari Tanzania kimeamua kumsimamisha uanachama wa chama hiki Dkt. Deo Mtasiwa, ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Serikali (CMO), kwa kosa la kusaliti fani ya udaktari na pia kwa kushindwa kumshauri waziri wa afya vizuri kuhusiana na mambo yanayohusu fani ya udaktari Tanzania. Mkutano huu unamsimamisha rasmi Uanachama huo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Taratibu za kumrejesha zitajadiliwa kwenye Mkutano mkuu wa kawaida wa chama. Hii itakuwa fundisho kwa madaktari wengine wote nchini.

5. Kwamba chama cha madaktari Tanzania (MAT) kimeazimia kuitisha mkutano mwingine mkubwa wa wanachama wote siku ya jumatano tarehe 18/01/2012, kuanzia saa tatu asubuhi na kuendelea kwenye ukumbi utakaotangazwa. Agenda za mkutano huo, pamoja na mambo mengine, zitakuwa zifuatazo:

i. Hatma ya heshima ya fani ya udaktari na mustakabali wa huduma za afya kwa watanzania
ii. Kwa nini serikali haijaanza kulipa posho ya kazi muda wa ziada (on call allowance) kama ilivyopitishwa mwaka 1990 na kufanyiwa maboresho mwaka 2008.
iii. Mshahara mpya wa daktari unaoendana na elimu, ujuzi, umuhimu, hadhi, majukumu, na hali ya uchumi wa sasa na mfumuko wa bei.
iv. Maslahi mengine ya madaktari kama nyumba, posho ya mazingira magumu, ufadhili wa masomo ya elimu ya juu na posho ya kufanya kazi kwenye mazingira hatarishi( Risk allowance).
v. Kuhamishwa hovyo hovyo kwa madaktari bingwa 61
vi. Mengineyo (kwa idhini ya mwenyekiti)

IMETOLEWA NA

DR. NAMALA MKOPI
RAIS – CHAMA CHA MADAKTARI TANZANIA (MAT)

No comments: