Saturday, January 7, 2012

RAI YA JENERALI

MWAKA MWINGINE WA UHUNI NA VURUGU CHAMA TAWALA
Ni mwendelezo ununuzi nafasi za ‘uongozi’

HAUHITAJI kuwa nabii kugundua kwamba mwaka huu utakuwa na mivutano na misuguano mingi ya kisiasa. Hili ni jambo linaloeleweka hata kwa wale tunaoweza kuwaita mbumbumbu-mzungu-wa-reli katika masuala ya kisiasa.

Mwaka huu zitafanyika chaguzi nyingi na za ngazi mbali mbali ndani ya CCM, chama-tawala, kuanzia ngazi za mashina hadi kileleni, ngazi ya uongozi wa taifa, hatima yake ikiwa ni uchaguzi wa halmashauri kuu na mwenyekiti wa chama hicho.

Chaguzi zote hizi zinaingia katika mantiki ya kawaida ya kukihuisha chama, kukipa uhai mpya kwa kukipa uongozi mpya na kukiwekea malengo mapya au kushadidia yale ya zamani kwa mwamko mpya.

Chama chochote, hata chama cha wacheza ngoma, hakina budi kufanya kazi ya kujikagua kila mara, kwa vipindi vilivyokubaliwa ndani ya chama husika. Kwa sababu hili ni jambo la kawaida, halitakiwi kuzua mijadala yoyote mizito.

Lakini hali tuliyo nayo si ya kawaida, na hali tunayoishuhudia ndani ya chama-tawala si ya kawaida hata kidogo. Vurugu zilizomo ndani ya chama hicho zinatisha. Matamko yanayotolewa na wakuu wa chama hicho ni ya kustaajabisha. Mambo yanayofanywa na viongozi wa chama hicho ni ya kutia hofu.

Katibu mkuu wa zamani wa chama hicho aliwahi kusema, baada ya kuwa si katibu mkuu tena, kwamba chama hicho kilikuwa kimepoteza dira na hakikuwa na mwelekeo tena. Bila shaka hayo ni maneno yanaweza kuelezwa kuwa ni sawa na yela ya “sizitaki, ni mbichi” ya yule sungura aliyebeza zabibu alizoshindwa kuzifikia, na tungeweza kumsaili juu ya kile alichofanya kurekebisha hali hiyo wakati akiwa katibu mkuu.

Kwa vyovyote vile, jambo lisiloepukika leo ni ukweli kwamba chama hicho kimekwisha kama chama cha siasa, kimebakia kuwa chama-tawala kweli kweli kwa maana kinachofanya ni kutawala tu, basi, na katika kutawala kwenyewe kinatawala vibaya. Tukiirejea kauli ile ya katibu mkuu wa zamani wa chama-tawala tunakumbushwa kwamba matatizo ya chama hiki yameanza kitambo; si ya juzi wala jana. Katika misemo ya ki-msiba, leo tusingezungumzia kifo cha marehemu, wala tusingezungumzia matanga, na wala isingekuwa arobaini. Tungezungumzia kumbukumbu ya miaka kadhaa tangu marehemu atutoke.

Hii ina maana kwamba kilichobaki ni mipangilio ya kuendeleza utaratibu wa ki-dola kwa kutumia jina la chama ambacho hakipo tena isipokuwa mabaki yake (residual essence) yanayoruhusu misemo, kauli-mbiu na vibwagizo, lakini si matendo halisi yaliyosimikwa juu ya misingi ya falsafa na itikadi. Kimebaki ni chama-bua, ndani yake hamna kitu hata kama kwa nje kinaonekana kimejaza.

Sasa hicho ndicho chama kinachoingia katika mchakato mrefu wa uchaguzi mwaka huu wote, na nchi nzima itakokotwa na mkumbo huo, itake, isitake, kwa sababu hiki ni chama-tawala, na kinaweza kutoa maagizo na yakatekelezwa, kwa sababu kina dola.

Kwa hiyo, nchi itaburuzwa katika uchaguzi huu ambao utakuwa si jambo jingine isipokuwa muendelezo wa mipangilio ya ki-dola, hususan mipangilio itakayolenga uchaguzi mwingine. Huu ni uchaguzi wa mwaka 2015, ndani ya chama-tawala chenyewe, na baadaye nchini kwa ujumla.

Kitakachofanyika mwaka huu ndani ya chama-tawala ni kwa kila kikundi ndani yake kuweka utaratibu utakaokiwezesha kikundi hicho kukusanya kura nyingi ndani ya chama-tawala kukiwezesha kikundi hicho kukamata dola baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kukamata dola kwa kikundi kimoja maana yake ni kuvishinda vikundi vingine vinavyoiwania dola. Kukamata dola maana yake ni kujihakikishia fursa ya kukusanya utajiri haramu unaotokana na kikundi fulani kuhodhi madaraka ya dola.

Ndiyo maana katika vikumbo tutakavyoshuhudia mwaka huu hadi mwaka 2015 hatutasikia hata kidogo mabishano ya kifalsafa wala ya kiitikadi, hata ya ki-sera; tutakachosikia ni minada ya majina ya watu na majina ya vikundi, ikiandamana na kauli-mbiu zilizotungwa na ma-MC.

Hali hii inanifanya niwe na hofu kuhusu chama-tawala hiki na jinsi kinavyojipeleka kuelekea kwenye vurugu. Kwa chama kinachojinasibu kuwa bingwa wa kujenga nchi ya “amani na utulivu” nchini, chama hiki kimekuwa ni kama genge la vurugu lililojaa chuki, ugomvi, inda, fitna, hiyana na kila aina ya uovu.

Ndani ya chama kimoja yamo makundi yanayoombeana kifo na yanaweza yakasababishiana kifo huko tuendako. Uhasama uliomo ndani ya chama tawala haupo kati ya chama hicho na vyama vya upinzani. Kwa nini?

Kuna mgando wa hisia. Hadi sasa wana-mipangilio wanaojiona ni wanasiasa wanahisi kwamba rais ajaye lazima atoke katika chama-tawala. Sababu ya hisia hiyo ni kwamba tangu mwaka 1961 rais amekuwa akitoka chama hicho hicho. Mgando huo wa hisia hauruhusu kufikiri kwamba inawezekana safari hii rais asitoke katika chama hicho, hata kidogo. Kwani nini kimebadilika hadi tufikie huko? Nchi hii ije kutawaliwa na hawa wahuni?

Hisia zilizoganda haziruhusu kutambua kwamba nchi imebadilika kiasi kwamba sisi tuliokuwapo mwaka 1961 ndio wachache tukilinganishwa na wale waliokuja baada ya Uhuru.

Hisia mgando hazioni kwamba wahuni wamejenga makao ya kudumu ndani ya chama-tawala na wanafanya mambo ya kihuni kama kugawiana nyumba za serikali, kupora Benki Kuu na kujizawadia migodi ya taifa. Kama kuna uhuni zaidi ya huo itabidi tuwajaribu na wengine nao watuonyeshe viwango vya uhuni wao.

Lakini mgando wa ubongo unawatia hamasa wanamakundi ndani ya chama-tawala kuchimbana, kushutumiana, kutukanana, kuwindana, kuhujumiana, na wataendeleza kasi ya mapambano yao hayo hadi mwaka 2015, kabla hawajagundua kwamba ‘wahuni’ wenzao ndani ya vyama vya upinzani wamekwisha kuiteka nchi.

Hata hivyo, ziko mbinu nyingi za kuhakikisha kwamba “kuiteka nchi” ni tofauti na kuchukua dola, kama ‘wahuni’ wengine wa Kenya walivyotufundisha miaka mitano iliyopita. Hawatajali kwamba uhuni wao unaweza kusababisha maafa kwa taifa. Kwani ni lini wahuni walijali mambo madogo madogo kama hayo?

Nimekwisha kuonyesha katika safu hii ni jinsi gani wana-mipangilio wanavyotumia fedha kununua nafasi za utawala ili waweze kutengeneza (kuiba) fedha zaidi. Nimekwisha kuonyesha vile vile jinsi ambavyo bei ya kuinunua nchi nzima inaweza kupangwa. Sasa ninajaribu sana kujishawishi kwamba nilichokuwa nikikieleza ni uwezekano wa kimantiki kutokana na jinsi tunavyoenenda, na si kwamba ni kweli bei imekwisha kupangwa! Sijui.

Viwango vya fedha vinavyoendelea kutumika katika chaguzi zetu tunavijua? Fedha hizo zinatoka wapi? Tukiacha zile zilizochotwa na Mkapa na wenzake kutoka Benki Kuu, vyanzo vingine ni vipi? Hivyo vyanzo vina maslahi gani katika nchi hii? Je, haiwezekani kwamba uamuzi mwingine wa Serikali yetu unakwamishwa na jeuri ya vyanzo hivyo? Wakuu wa Serikali wanashangaa nini, wakati wanajua? Na sisi tunashangaa nini kuhusu wafanyabiashara wa mafuta ya petroli, au wamiliki wa vitalu vya uwindaji?

Tujiandae kuona katika mwaka huu wakuu wa chama-tawala wakipigana vikumbo kwa ari kubwa zaidi, nguvu kubwa zaidi na kasi kubwa zaidi kukusanya fedha haramu kwa ajili ya kununua nafasi za kutengeneza fedha zaidi.

Sheria zipo zilizotungwa eti ili kuzuia fedha haramu zisiingizwe katika uchaguzi, lakini sheria hizo ni mwanasesere wa kuwinda ndege (scarecrow). Asasi za kuzuia rushwa zimeundwa, na hata kupewa majina mapya (PCB ikawa PCCB), lakini ni mwanasesere mwingine, na ndege wamekwisha kumng’amua.

Yote hii ni kwa sababu watungaji wa sheria hizo, na wasimamizi wa utekelezaji wake, hawakuwa na nia, na wala hawana nia, ya kuziruhusu zifanye kazi kwa sababu wao ndio wahalifu wakubwa dhidi ya sheria hizo. Kama wanabisha waseme.

Natoa changamoto kwa yeyote katika asasi za (eti) kupambana na kuzuia rushwa, udhibiti wa mienendo ya vyama vya siasa, ‘sekretareti’ za maadili, na asasi nyingine zinazoendeshwa kwa gharama kubwa za wananchi wa Tanzania wasimame wanisute kwa kusema uongo ninaposema kwamba wote hawa ni wanasesere, wao na asasi zao, na hawana sababu ya kuendelea kuwapo.

Asasi kama hizi zilianzishwa katika nchi nyingi zilizoendelea ili angalau kupunguza vitendo vya ufisadi katika michakato inayotakiwa kuwa mitakatifu, kama vile uchaguzi. Katika nchi hizo, kwa kiwango kikubwa asasi hizi na sheria zake zinafanya kazi, na mara kwa mara wahalifu hukamatwa na kuadhibiwa.

Nchini kwetu, najiuliza, tungetaka kuwakamata wahalifu kama hao, je, tungekuwa na Serikali, au tungekuwa na rais mstaafu, au waziri mkuu mstaafu, au waziri mstaafu asiyekuwa gerezani?

Haya ni masuala ya kutafakari wakati tukiuanza mwaka huu ambao bila shaka utakuwa na mikwaruzano mingi ndani ya chama-tawala, lakini pia utakuwa na mabishano yenye hamasa kuhusu mustakabali wa taifa letu na masuala muhimu yanayohusiana na hilo, kwa mfano uandishi wa Katiba mpya. Nitayajadili.


RAIA MWEMA


No comments: