Thursday, January 19, 2012

PEMBA NA KUMBUKUMBU MUHIMU ZA KIHISTORIA

Na Charles Kayoka,

KATIKA mlango bahari unaoruhusu maji kuingia hadi ghuba ya Mikindani, Mtwara, kuna kitongoji kimoja ambacho umaarufu wake sasa haupo tena, lakini ni muhimu sana unapozungumzia historia ya kuabiri baharini, uvuvi, ukoloni na biashara ya utumwa.
Hapo kwenye mlango bahari ndipo watumwa waliouzwa pale Mikindani, walikuwa wakipitishwa na mitumbwi mikubwa kuelekea Zanzibar, Mafia, na Uarabuni. Na sio watumwa tu, bali rasilimali zingine za asili. Kitongoji hicho kinaitwa Pemba, kiko katika kijiji cha (kata ya )Naumbu.

Na hata katika miaka michache kabla na baada ya uhuru, Mkonge ulikuwa ukipita hapa, na kulikuwa na gati maalumu la kupakia bidhaa hiyo, Ananieleza mkazi mmoja ambaye ni mwenyeji wa pale, ambaye ni mtunza Msikiti wa urithi kutoka kwa baba yake.
Lakini Pemba hiyo ina makuu gani?

Hapo zamani, aliniambia mhabarishaji wangu, Unguja ndio ilionekana ni mji ambao kama hujawahi kwenda ulionekana hujasafiri, na unaonekana mshamba bado. Ilikuwa kama Dar-es-Salaam ya sasa, kama hujaenda huko basi wewe bado uko nyuma.
Wakati ule mitumbwi mikubwa ya kufanyia safari hizo ilikuwa hapa, na mabaharia mashuhuri walikuwepo hapa Pemba. Sasa hivi hakijulikani sana kama Pemba, bali Mkayula. Ukifika hapo Pemba unaweza kumaizi kuwa ni eneo linalohifadhi historia ambayo kwa sasa si rahisi kujua utaanzia wapi ili kuiandika.

Hili kaburi tumelikuta, na niliwahi kuambiwa na babu yetu mmoja, wakati huo akiwa na miaka mia moja na saba hivi, kuwa na yeye alizaliwa akalikuta hapa, na wakati huo watu walikuwa wakija hapa kufanya maombi na kuacha fedha kama sadaka zao za kukamilishia maombi.
Nilifikishwa hadi hapo, ni wazi limeanza kufukiwa na mchanga kabisa ingawa linaonyesha kuwa limezikwa mtu mwenye asili ya Uarabuni, kutokana na mfumo wake wa ujenzi.

Kijiji hicho kina misikiti miwili iliyochoka kabisa kutokana na umri mkubwa. Mmoja ni msikiti wa Ijumaa, ingawa kwa kweli unaelekea kufikia kikomo cha matumizi kutokana na hali mbaya ndani na nje. Na Mwingine ni msikiti wa kawaida ambao mhabarishaji wangu anaumiliki kama urithi toka kwa baba yake. Yeye hajui Msikiti huo umejengwa lini kwani, hata kaka yangu alipozaliwa mwaka 1947 hivi aliukuta ukiwa unatumika. Nao umechoka zaidi.

Aliniambia kuwa mwaka jana palikuwa na sherehe nzito hapo kijijini, chini ya mbuyu, iliyolenga kuburudisha wageni wa kizungu kutoka Uingereza. Huenda niseme tu kuwa kwenye mlango bahari huo wamepita watu mashuhuri katika historia ya ukoloni na umisionari, akiwemo John Hanning Speke (mtafiti na mwanajeshi wa jeshi la kikoloni huko India) na Dr. David Livingstone, ambao walikuwa watafiti maarufu wa Kiingereza.
Na ukifika Mikindani mjini utakuta nyumba ambayo mtafiti, David Livingstone, alipata kuishi, na sasa iko kwenye ukarabati.

Hatujui John Hanning Spekes aliishi nyumba ipi, na utafiti wangu hauonyeshi alikuja mwaka gani huko Pemba (ingawa inaonyesha alifika mara mbili Zanzibar kwa ajili ya kufanya safari ya uvumbuzi wa Ziwa Victoria na Tanganyika).
Na kuwa haijulikani alikuwa akiishi nyumba gani kwani hakuna kumbukumbu, kwani kama kulikuwa na nyumba ambazo wageni walikuwa wakiishi, sasa hivi hazipo tena.

Lakini nilionyeshwa, hapo kijijini Pemba mti mmoja mkubwa sana wa mbuyu ambapo inasemekana Spekes alikuwa ana tabia kupumzikia na kupata kivuli. Na hiyo ndiyo sababu ya kufanyika kwa sherehe pale Pemba.
Wageni hao walikuja hapo kijijini kutokana na kumbukumbu ya shajara ya Spekes ambayo inaonyesha kuwa alikuwa akiishi hapo na kuwa alikuwa akipumzika kwenye mbuyu huo wenye pacha, kwenye mlango bahari.

Na kuwa katika shajara hiyo alikitaja kijiji cha Pemba, Mikindani Mtwara. Kwa maelezo hayo, kizazi hicho cha Spekes waliweza kusafiri na hatimaye kufika hapo kijijini. Kwa furaha yao walifanya sherehe kubwa kama kumbukumbu ya mtafiti huyo maarufu wakati wa karne ya 19.
Lakini yote haya mtu huwezi kuyafahamu kwa sababu hakuna mahala unapoweza kufika, pale Mtwara au Dar-es-Salaam, kupata taarifa hizo.

Aidha unaona majengo hayo muhimu yenye uhusiano mkubwa na historia yetu, lakini hakuna anayejali kuyatunza. Lakini wakati huo huo tunahimiza utalii wa ndani. Ni utalii upi kama huu wa kihistoria hatuuzingatii. Lakini la muhimu zaidi, hii ni historia yetu, historia ya maisha yetu kama nchi.

No comments: