Monday, January 16, 2012

NYALANDU ATAJA VINARA WA URAIS 2015


Geofrey Nyang’oro,

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu amewataja vigogo watatu ambao amekuwa akihusishwa nao kwamba anawaunga mkono katika harakati za mbio za urais wa 2015.Vigogo hao ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.

Nyalandu alitaja majina hayo katika mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia hali ya kisiasa nchini na athari za siasa za makundi katika vyama vya siasa, huku akisema kuwa hali hiyo inaathiri utendaji kazi katika taasisi za umma.

Alisema imefika wakati inakuwa vigumu kuwa na uhusiano hata wa kirafiki na mtu kwani kila unapoonekana ukisalimiana na wale wanaotajwa kuwa katika mbio hizo basi unawekwa alama kuwa mtu mwenye nia hiyo au kuwa katika moja ya makundi.

“Makundi haya yanadaiwa kuwa na wafuasi, endapo haupo kwenye kundi fulani, basi unadhaniwa kuwa adui mkubwa wa kundi hilo, wakitumia dhana isemayo, kama hauko nasi wewe uko kinyume nasi,” alisema Nyalandu na kuongeza:“Taifa limejaa malalamiko, hisia za kupigana vijembe, kutafutana ubaya na kuoneana kisiasa.”

Alisema wanasiasa vijana wanapoonekana kujitolewa kufanya kazi kwa moyo na kujitoa zaidi ya wito wa kazi wanawekwa katika darubini na kupaswa kusema wako katika kundi gani.

Naibu Waziri huyo alisema kuendelea kushamiri kwa siasa za aina hiyo kunaliweka taifa katika hatari kutokana na kuzorotesha shughuli za maendeleo za kila siku.

“Wanapokataa kurubuniwa, wanawekwa kwenye kundi lililo kinyume na kundi husika na kuanza kushambuliwa, kwa kifupi, nchi yetu ni kama nyumba moja na imesemwa zamani, nyumba iliyotengana haiwezi kusimama,” alisema.

Alisema hali hiyo inaliweka taifa katika wakati mgumu na hasa kipindi hiki ambacho inakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii na kukuza demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.

“Tunaowajibu wa kuhakikisha uwajibikaji unaongezeka nchini na kila mtu anatimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii ili taifa liweze kuhimili ushindani utakaotokana na ushirikiano wa Afrika Mashariki, zikiwemo fursa na changamoto zake,” alisema Nyalandu.

Alisema hana nia ya kugombea urais wala kujihusisha na kundi lolote akisema hali ya kuwapo kwa makundi ni hatari kwa taifa na inapunguza kasi ya uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi wenye nia ya kufanya hivyo.

“Hali ya kisiasa iliyopo sasa na hasa kwa baadhi ya viongozi kujikita katika kutafuta urais wa 2015, huku wafuasi wao wakiendeleza mapambano dhidi ya wale wasiokubali kuwa ndani ya makundi husika inasikitisha na ina lengo la kukatisha tamaa viongozi wenye nia ya kufanya kazi walizopewa kwa bidii,” alisema. Nyalandu alisema kwa sasa Rais Jakaya Kikwete bado anatumikia miaka minne katika nafasi ya Urais na kusisitiza hakuna sababu ya kundi lolote wala mtu kufikiria urais wa 2015.

Lowassa, Membe na Sitta
Nyalandu ambaye ni Mbunge wa Singida Kaskazini, alilalamika kwamba amekuwa mwathirika wa siasa hizo kwani amekuwa akihusishwa na makundi mbalimbali ya wanaotajwa kuutaka urais mwaka 2015 na kwamba hali hiyo kutokana na uhusiano alionao na wanaotajwa.

“Wapo walioniona Monduli na kudai kuwa eti ninaelekea kuwa katika kundi la Lowassa. Mimi sina uhusiano na kundi lolote hata kama makundi hayo yapo,” alisema Nyalandu.

Alisema yeye amekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Lowassa kutokana na kufanya naye kazi alipokuwa Waziri Mkuu hasa kufanikisha ujenzi wa shule za sekondari katika Jimbo la Singida Kaskazini.

Kuhusu Membe alisema ni rafiki yake wa muda mrefu. “Membe ni rafiki yangu wa muda mrefu, nimezoeana naye tangu siku nyingi na pia nimefanya naye kazi hata nikifika nyumbani kwake naweza kuingia bila hodi na kula hata chakula bila tatizo lolote,” alisema Nyalandu.

Alitaja pia uhusiano wake na Sitta akisema kiongozi huyo ni kama mshauri wake na mwalimu anayemsaidia katika mambo mengi.Alisema watu kutoka katika makundi tofauti wanapomwona na watu hao wamekuwa wakifikiri kwamba na yeye ni sehemu ya kundi husika jambo ambalo alilipinga.


MWANANCHI

No comments: