Wednesday, January 4, 2012

MASKINI DR. MWAKYEMBE: ANYONYOKA NYWELE KILA KUKICHA
HALI ya afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, inasikitisha kwani licha ya kupata matibabu nchini India na kuendelea na tiba hiyo hapa nchini, hali yake siyo ya kuridhisha.

Watu wa karibu na Dk. Mwakyembe waliopata fursa ya kumwona, waliliambia Tanzania Daima Jumatano kuwa afya ya waziri huyo maarufu nchini bado siyo ya kuridhisha kwani amenyonyoka nywele, kope, nyuzi na hata vinyweleo vyote mwilini.

Mbali ya hali hiyo, Dk. Mwakyembe hulazimika kuvaa gloves mikononi na miguuni, fuluna au mashati marefu pamoja na traksuti au suruali ili kufunika mikono na miguu yake ambayo licha ya tiba anayoendelea kuipata, ngozi yake ina hali mbaya kutokana na kuathirika na ugonjwa wa ajabu uliompata.

Kwa mujibu wa habari hizo, kucha za vidoleni na miguuni zimeoza na zina rangi nyeusi, miguu na mikono yake imepasuka mithili ya mtu mwenye magaga ambayo wakati mwingine hutoa damu na kumsababishia maumivu makali.

“Kwa jinsi alivyo, Dk. Mwakyembe hawezi kwenda ofisini leo au kesho. Siha yake ukimwangalia ni nzuri na anaongea kwa sauti kama kawaida, lakini ngozi yake iko vibaya, kichwani hana nywele wala kope, nyusi…

“Anahitaji muda zaidi wa kupumzika na kuendelea na matibabu,” alisema mmoja wa watu waliofanya ziara ya kwenda kumwona nyumbani kwake Kunduchi Mtongani, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya watu wa karibu na waziri huyo walioshuhudia mkanda wa matibabu yake akiwa India, waliliambia gazeti hili kuwa ukiuangalia, utatoa machozi kwani picha zake zinatisha.

Mkanda huo ambao Dk. Mwakyembe hupenda kuwaonyesha watu wanaofika nyumbani kwake Kunduchi Mtongani kumjulia hali, unamwonyesha katika sura na muonekano tofauti kabisa na jinsi alivyo na kama unauangalia leo bila kuambiwa, huwezi kubaini kama ni Waziri Mwakyembe.

“Ukiuangalia mkanda wa matibabu yake, unaweza kutoa machozi, unasikitisha sana. Kwa kifupi Dk. Mwakyembe amepata mateso makubwa yaliyotokana na ugonjwa ambao hadi sasa haujulikani,” alisema mtoa habari wetu.

Hata hivyo ingawa taarifa rasmi ya serikali haijatolewa, ripoti ya ugonjwa wa waziri huyo kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali maarufu ya Apollo nchini India ambayo hadi sasa imebaki kuwa siri, inadaiwa kueleza chanzo cha ugonjwa wa Dk. Mwakyembe kuwa umetokana na sumu kali aliyowekewa hapa nchini.

Taarifa za Dk. Mwakyembe kuwekewa sumu, mara ya kwanza ziliibuliwa rasmi nchini na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye ni rafiki mkubwa na mshirika wa karibu wa Dk. Mwakyembe katika mapambano dhidi ya ufisadi nchini katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ITV katika kipindi chake cha dakika 45 kilichorushwa hivi karibuni, alisema wasiwasi huo unatokana na mabadiliko ya ngozi na nywele aliyoondoka nayo nchini kwenda India.

Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), alisema alipokwenda kumwona Dk. Mwakyembe nyumbani kwake, alipata mshtuko mkubwa kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza katika umri alionao kushuhudia ngozi ya mtu ikitoa unga.

Sitta alikaririwa akisema, “Kuna kitu kama mba kwenye nywele na kwenye ngozi ya Dk. Mwakyembe. Akishika hivi, baadhi ya nywele zinadondoka. Mkono umevimba, sehemu mbalimbali. Mke wake alichukua video. Alikuwa anatuonyesha kwenye laptop (kompyuta ndogo). Kwa kweli inatisha.”

Hata hivyo, Sitta alihojiwa na polisi kuhusiana na taarifa hiyo kwa madai kuwa ingeweza kuhatarisha amani, lakini alipotakiwa kutoa ushahidi anadaiwa kutoa ushahidi wa habari za kwenye mitandao ya kijamii.

Kabla ya Dk. Mwakyembe kwenda India kutibiwa, kulikuwa na uvumi kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa kiongozi huyo kulishwa sumu, ingawa yeye binafsi hajakanusha wala kuthibitisha habari hizo.

Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu aliporejea nchini, Dk. Mwakyembe alisema ripoti ya ugonjwa wake iko serikalini.

Hata hivyo, serikali hadi sasa imekataa kuitoa hadharani ripoti hiyo ya madaktari bingwa wa Hospitali ya Apollo, India, waliomtibu Dk. Mwakyembe.

Habari zaidi zinasema kuwa mwanasiasa huyo amepania kuianika ripoti hiyo hadharani kama serikali itaendelea kuifanya kuwa siri.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, alipoulizwa kuhusiana na ripoti hiyo, alisema kuwa suala hilo haliwahusu na kama wameipokea hawezi kuzungumzia.

Alisema Dk. Mwakyembe ndiye anaweza kuzungumzia na hajui kama imepokelewa au la.
“Hata kama tumeipokea, sina ruhusu ya kuzungumza, mfuate mwenyewe Dk. Mwakyembe akueleze kwani sisi hatuwezi kutaja ugonjwa uliokuwa unamkabili,” alisema Nyoni.

Mwakyembe alipelekwa India Oktoba 9 mwaka jana na kurejea nchini Desemba 11 mwaka jana.

Taarifa za awali, zilisema Dk. Mwakyembe alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari ambapo alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Lakini, taarifa hizo za ugonjwa wa kisukari zilipingwa na baadhi ya washirika wake wa karibu kisiasa ambao waliamini naibu waziri huyo alilishwa sumu.

TANZANIA DAIMA

No comments: