Monday, January 16, 2012

MAJESHI YA BURUNDI NA WAASI YAPIGANA NDANI YA TANZANIA


Na Frederick Katulanda


MAPAMBANO kati ya majeshi ya Burundi na vikosi vya waasi wanaoipinga Serikali ya nchi hiyo, yamezua hofu kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera baada ya vita hiyo kuhamia na kuanza kupiganwa ndani ya ardhi ya Tanzania.

Habari zinaeleza kuwa wananchi kwenye maeneo hayo wanaishi kwa mashaka kufuatia waasi wa kundi la Forces for National Liberation (FNL), kuvamia vijiji kadhaa vya mpakani wilayani Ngara, huku wakipora mazao na mifugo kwa ajili ya chakula.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Salewi na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu, Fabian Masawe, zilisema mbali ya uovu huo, waasi hao wamekuwa wakifanya mazoezi katika ardhi ya Tanzania.

Taarifa zaidi kutoka Kijiji cha Mumiramira, Kata ya Bugalama zimeeleza kuwa mapigano kati ya Warundi hao yamekuwa yakianzia maeneo ya Kijiji cha Kihinza nchini Burundi, kilichopo umbali wa kilomita moja kutoka eneo la mpaka wa Tanzania na Burundi.

Chanzo hicho kilieleza kuwa waasi hao wanapozidiwa nguvu, wamekuwa wakikimbian na kuvuka mpaka kuingia Tanzania huku majeshi ya Serikali ya Burundi nayo, yakivuka mpaka kuwafuata na kuwasaka.

Hali hiyo imesababisha wanajeshi na waasi hao kukabiliana ndani ya ardhi ya Tanzania, jambo ambalo tayari linadaiwa kusababisha kifo cha Mtanzania mmoja.

Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi waliohojiwa pamoja na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bugalama, Josamu John, walieleza kwamba mapigano makubwa yaliyoleta athari zaidi, yalitokea Novemba 19, mwaka jana ambapo milipuko kadhaa ya mabomu, ilisikika.

Hali hiyo ilisababisha wakazi zaidi ya 40 wa Kitongoji cha Kalamba kuyakimbia makazi yao na kuishi kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Mumiramira.

Mapigano hayo pia yalisababisha mgodi wa Kabamba Nickel uliopo wilayani Ngara, kufungwa kwa siku 15 na wafanyakazi wake kurejeshwa makwao.

Kabla ya mapigano hayo katika ardhi ya Tanzania, waasi hao inasemekana walikimbilia nchini na kufanya mazoezi Oktoba, 2011.

Miongoni mwa vikosi hivyo inadaiwa vilivamia Kijiji cha Mumiramira na kuingia nyumbani kwa Kamanda wa Mgambo wa Kijiji, James Thomas na kumuua kwa madai kuwa alikuwa akifuatilia nyendo zao.

“Ni kweli hali hii ipo. Hawa watu wanavamia kila mara wanaweza kufika na kuiba mazao kweye maghala ya wananchi. Wakifika inategema wanahitaji nini wakati mwingine hufika kijiji na kupora mifungo ya wananchi na kutoweka,” alieleza Mtendaji huyo ingawa alionekana kuwa na hofu ya kutoa taarifa zaidi.

Habari zaidi zimeeleza kuwa wakazi wa vijiji vya mpakani wamekuwa wakishuhudia waasi hao ambao wamekuwa wakiingia kwa makundi nchini nyakati za usiku na kupora mifugo na vyakula.

Baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo, kwa nyakati tofauti waliliambia Mwananchi Jumapili kwamba majeshi ya Serikali ya Burundi yamekuwa yakiendesha operesheni kali kuwasaka waasi hao ndani ya ardhi ya Tanzania kwa lengo la kuwaua.

“Mimi ninaamini kuwa Serikali inaficha ukweli kwa kuogopa kuwapa hofu wananchi. Mfano sisi wafanyakazi wa Mgodi wa Kabanga Nickel tunapokuwa katika shughuli zetu za utafiti wa madini porini, tumekuwa tukikutana nao ndani ya eneo la Tanzania kabisa na tunatoa taarifa lakini hatuoni hatua zozote kuchukuliwa,” alilalamika mmoja wa watumishi wa mgodi wa Kabanga Nickel kwa sharti la kutotajwa jina.

Alisema waasi hao wamekuwa wakionekana kwenye makundi makubwa ya watu zaidi ya 100, huku wakiwa na silaha za kivita.

Alisema mara nyingi wamekuwa wakionekana upande wa Tanzania majira ya asubuhi wakifanya mazoezi na kila inapofanyika hivyo, usiku yamekuwa yakizuka mapambano, huku milio ya risasi ikitawala.


“Sijajua kama ni waasi au la, lakini serikali inapaswa kuchukua hatua zaidi. Kila tunapowaona tunatoa taarifa kwa Serikali, lakini hatuoni utekelezaji kwani hali hii huendelea, kibaya ni pale wanapoingia na kupora mazao kwenye mashamba ya watu na mifugo yao," alilalamika mwananchi huyo huku akisisitiza kuwa iwapo hali hiyo haitadhibitiwa mapema, watu hao wanaweza kuvamia hata mgodi huo.

Mbali na wapiganaji hao inaelezwa kuwa baadhi ya raia wa Burundi wanaokimbia machafuko hayo wamekuwa wakimiminika maeneo hayo kukoa maisha yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Henry Salewi, alisema hali ya mipaka yetu iko salama na kwamba wananchi wamekuwa wakikumbwa na hofu hasa mapigano yanapokuwa yakipiganwa umbali wa kilometa moja nchini Burundi.

Alikiri kuwa hofu kwa Watanzania ni pale milio mikubwa ya milipuko na risasi inaposikika huku baadhi ya risasi na mabomu mengine kuingia nchini.

“Hawa waasi wanapigwa sana. Wakianza mapigano wanapigwa kweli kweli na inapotokea hali imewazidi hukimbilia kwetu na sisi tukiowaona tunawarudisha huko.

"Mfano ni mwezi Novemba (mwaka jana), mapigano yalikuwa makali sana, walikimbilia kwetu na sisi tulituma vikosi maalumu kuwadhitibi na kuwarudisha ambapo kuna baadhi yao tuliweza kuwakamata na kuwakabidhi kwa Serikali ya Burundi,” alieleza Kamanda Salewi.

Alisema kikosi maalumu cha JWTZ kiliingili kati na kurudisha eneo hilo katika hali ya usalama na hadi jana, kilikuwa kinaendelea kuimarisha ulinzi.

Alieleza kwamba hadi sasa, hakuna mwananchi aliyeuawa kutokana na mapigano hayo ya waasi ama risasi na mabomu kufika Tanzania, lakini alikiri kwamba hali hiyo imekuwa ikizua hofu kwa wananchi hao.

Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakipiga simu polisi kuwajulisha kila wanaposikia milio ya risasi usiku.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagara Kanali Masawe, alisema anachojua yeye ni kuwa kuna kundi la majambazi ambalo limekuwa likisakwa na Serikali ya Burundi.

Alisema kundi hilo limekuwa likikimbilia nchini lakini kutokana na ulinzi wa mpaka huo kuimarishwa, wamekuwa wakidhibitiwa na wengine kukamatwa na kurejeshwa Burundi.

“Tunapozungumza katika vikao vya Kamati ya Ulinzi na Usalama vya ujirani mwema, wenzetu wa Serikali ya Burundi wao wamekuwa wakitueleza kuwa kuna majambazi ambayo wamekuwa wakiyasaka kila yapokimbilia kwetu,"Mara nyingi wamekuwa wakiingia kwetu majira ya asubuhi na kurudi kwao usiku ila hakuna madhara ambayo watu wetu wamepata,” alieleza Mkuu huyo wa Mkoa.

Alisema kwa sasa vikosi vya JWTZ viko eneo la mpaka huo kuimarisha ulinzi na jukumu lao kubwa ni kudhibiti watu hao.Alisema wakati huu ambapo hakuna vita, shughuli ya doria na ulinzi imekuwa ikifanywa zaidi na Jeshi la Polisi.

MWANANCHI

No comments: