Friday, January 13, 2012

MADAKTARI MMEZIDI KUDHARAULIWA

Msiposimama pamoja, mtaangamia mmoja mmoja


Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela,

TUKIO la hivi karibuni la Serikali kuamua kuwafukuza madaktari wanafunzi waliokuwa wanadai mafao yao mbalimbali na nyongeza za mafao hayo, linahitaji kulaaniwa na kuoneshwa kuwa ni la kibabe. Madaktari wa Tanzania yawezekana ndio madaktari wanaofanya kazi katika mazingira mabovu zaidi wakitarajiwa kuhudumia maisha ya wananchi huku wanasiasa wa nchini wakiishi maisha ya juu zaidi, wakijiaminisha kuwa wanastahili zaidi! Tujadili suala hili katika maeneo mahsusi kama ifuatavyo.

Tiba nchini India

Mojawapo ya vitu ambavyo vinaonesha dharau na kukosekana kwa heshima ya hadhi ya madaktari wetu ni hili la kupeleka wagonjwa India, kwa matibabu ambayo yangeweza kufanyika hapa nchini. Niliandika juu ya hili miezi michache iliyopita lakini yafaa nirudie.

Ningependa kujua kama viongozi serikalini wamewahi kukaa chini na kujiuliza swali jepesi (wengine wanaweza kuliita la kizushi) la ni kwa nini tunapeleka wagonjwa India na siyo kutibiwa hapa hapa nchini?

Jibu la swali hili lina pande mbili – upande wa kwanza wapo wanaodai kuwa gharama ya kutibiwa India ni nafuu zaidi kuliko nchini. Sijui kama kuna ukweli wa hili na ni nani aliyewahi kufanya utafiti wa kupima hili.

Ni kweli gharama ya nauli ya ndege kwenda na kurudi, chakula na malazi na mapumziko huko India ni ndogo kuliko kutibiwa hapa nchini?

Binafsi sitaki sana kuamini hili kwa sababu gharama inasababishwa na vitu mbalimbali, je, Serikali yetu imeshindwa kabisa kufikiria namna ya kufanya gharama ya afya kuwa nafuu hapa nchini? Na ni kitu gani kinafanya gharama iwe juu Tanzania ambacho hakiwezi kuangaliwa na kushughulikiwa?

Upande wa pili ni lile linalodaiwa ni ubora wa madaktari wa India. Wapo ambao wanaamini kuwa India ina madaktari wenye ujuzi mkubwa kuliko madaktari wetu. Watu wengi hawajui kuwa daktari wa Tanzania ili awe daktari kamili, anasomea kwa miaka saba wakati yule wa India anasomea miaka 5!

Madaktari wa Marekani nao wanasomea miaka saba! Na nchi nyingine zina tofauti ya kati ya miaka mitano hadi saba, huku hadi kuwa Bingwa inakuwa ni miaka karibu tisa ya mafunzo. Sasa ubora wa madaktari wa India unatokana na nini ambacho Tanzania haiwezi kukifanya?

Binafsi ningependa sana kuona chombo huru au taasisi huru kama walivyofanya watu wa taasisi za HakiElimu au Tunaweza, kwenye masuala ya elimu kupitia na kufanya ulinganifu wa madaktari wetu kulinganisha na India.

Nadharia yangu ni kuwa karibu vitu vyote vinavyofanywa India vinaweza kabisa kufanywa Tanzania. Watu wanapenda kwenda India kwa sababu zaidi ni hisia ya kuwa wanaenda “nje” kutibiwa.

Lakini nyuma ya hili ninaamini kuna hisia kuwa madaktari wa Tanzania hawaaminiki. Kuwa hawana uwezo – japo wanaweza kuwa wamesoma vizuri na hata kuzidi wale wa India na vile vile kuwa kutokana na maslahi yao duni hujikuta wakiendekeza taasisi zao binafsi zaidi kuliko kufanya kazi kwa weledi katika taasisi za ajira zao.

Hili la mwisho laweza kuwa na ukweli zaidi kwani wapo watu ambao wamewahi kujikuta wanaambiwa waende hospitali ya dokta kwa uangalizi zaidi. Lakini kwenye nchi ambayo maslahi ya daktari ni duni sana, daktari huyo afanye nini zaidi ya kujipatia kipato chake cha ziada pembeni?

Namfahamu Daktari mmoja (sasa Marehemu) ambaye alisomeshwa na fedha za Watanzania lakini baada ya kujitahidi kujitolea sana kufanya kazi ya udaktari aliona kuwa hailipi na matokeo yake alianzisha biashara yake ya baa na maduka na hadi anafariki, alikuwa ni Daktari wa cheo tu akikataa kabisa kurudi hospitali kutoa huduma. Wapo madaktari ambao udaktari ni sehemu tu ya kazi zao lakini wanapotengeneza fedha zaidi ni kwenye miradi yao mbalimbali.

Kutoboresha maslahi yao ni kejeli kwa utu wetu

Ndugu zangu, ni kweli walimu ni muhimu (sitaki kuingia mjadala wa ‘nani bora kati ya daktari na mwalimu’) lakini katika kujenga taifa la kisasa na lenye watu wenye afya bora hakuna nafasi ya pekee kama ya madaktari.

Ni wao ndio wanatupa nafasi ya kuishi na kutumikia taifa tukiwa na afya bora zaidi. Ni watu ambao kutokana na ujuzi wa kazi zao na vipaji walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu hujikuta wakiokoa maisha yetu (iwe katika ajali, magonjwa au dharura fulani).

Ni watu muhimu sana kiasi kwamba katika Wagiriki na Wayahudi wa kale uponyaji ulikuwa ni sifa ya kimungu. Waebrania walimuita Mungu Yehova Rapha (yaani Bwana Anayeponya) wakati Wagiriki walikuwa na mungu aitwaye Askelpias ambaye alikuwa ni mungu wa tiba na uponyaji. Kati ya mabinti zake mmoja aliitwa Hygeia (tunapata neno la Kiingereza Hygiene – usafi) na Panacea yaani “tiba ya magonjwa yote”. Ile fimbo yenye nyoka hujulikana kama fimbo ya Asklepias. Hivyo basi, madaktari si watu wa kudharauliwa au kufanywa duni.

Serikali inawaafanya madaktari wetu duni

Sizungumzii suala la kufukuzwa kwa hawa madaktari wanafunzi tu, nazungumzia jinsi tunavyowaangalia madaktari na kuwatendea. Ni kweli hatuwezi kuwalipa sana lakini ukweli ni kuwa kutokana na idadi yao, madaktari wanastahili kulipwa zaidi kwa ajili ya kuwavutia zaidi lakini vile vile kuwafanya wafanye kazi yao ambayo ni wito wao kwa kweli.

Unajua watu wengi hatuna wito wa kukaa na kufumua miili ya wanadamu, kuona uchafu wao na madamu yao na kuwapo pale kuwasaidia kurudi kwenye uzima au kuwasaidia wanapoelekea mauti. Ni wito wa ajabu sana ambao tusipoonekana kuuelewa tutaona kama “ajira nyingine tu”.

Daktari wa Tanzania anayeingia kwenye ajira tu asingelipwa chini ya mshahara wa kama dola 5,000 hivi kwa mwezi pamoja na mafao mengine. Ni lazima tumtoe huyu daktari kutoka kwenye miradi yake ya nyumbani na vibarua na kumhakikishia usalama wa maisha yake.

Hatuwezi kuwa na madaktari ambao ili wawahi hospitali kutoa huduma inabidi wadandie daladala au kununua gari mkweche. Haiwezekani leo tunajenga majumba ya wanasiasa lakini hatujawa na programu ya uhakika ya kuwajengea madaktari wetu nyumba za kudumu.

Hivi katika miradi yote ya Jiji la Dar es Salaam ni wapi wana mpango wa kujenga nyumba za makazi kwa madaktari? Huko mikoani ni wapi ambapo wana miradi ya kujenga nyumba za madaktari karibu na hospitali au kwenye maeneo ya kisasa ambayo yatawapa nafasi ya kupumzika na kutulia na kujifunza kabla hawajarudi kukimbia kuokoa maisha ya wananchi wetu?

Hivi watu wamewahi kujiuliza kuwa Tanzania ina madaktari wangapi? Katika Tanzania yetu hii ambayo watu wanaamini ina neema tuna daktari mmoja kwa kila watu kama 30,000 hivi. Marekani ina dokta mmoja karibu kwa kila watu 400 hivi. Sasa kweli tunaweza hata kufikiria kusimamisha madaktari wanafunzi zaidi ya 200 kwa sababu za kipuuzi – kwamba wamedai kuboreshewa maslahi yao? Kweli? Ni taifa gani ambalo tunajenga?

Yaani, wanasiasa wanaweza kujiongezea posho bila kuhojiwa na yeyote tena kwa asilimia zaidi ya 300, lakini hawa madaktari wetu hata ‘kiduchu’ wanachodai imekuwa ni nongwa? Hivi, kuna mwanasiasa wa CCM anayeweza kusimama na kutuambia akiwa na macho makavu kuwa madaktari wa Tanzania wanalipwa vizuri na mazingira yao ni bora?

Huyu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wa CCM) aliyedai kuwa wamejiongezea posho kwa sababu maisha ni magumu Dodoma alikuwa hafikirii kuwa huko Dodoma nako kuna madokta? Nani atawapigania madaktari wetu?

Naomba nitoe taarifa mbaya - madaktari wa Tanzania hawatopiganiwa na wanasiasa wetu! Wanajidanganya wale madaktari waliokaa Wizara ya Afya na ambao wanaishi maisha ya furaha kwa sababu wanakula na wakubwa! Hawa madaktari waliotupwa porini huko Katavi, Bukoba, Mbeya na sehemu nyingine waishi kwa kuombea kudura (kudra) tu! Hawana mtetezi. Na bahati mbaya sana hata vyama vyao haviwezi kuwatetea.

Kuna wakati, madaktari lazima wasimamie maslahi yao kwani kwa kufanya hivyo watasimamia maslahi ya wagonjwa wao na wale watumishi wa afya wa kada nyingine. Na kuna namna moja tu ambayo italazimisha watawala wetu kuangalia maslahi ya madaktari na kuwarudisha mara moja wale wanafunzi na kuhakikisha kuwa madaktari wa Tanzania wanapewa heshima na hadhi wanayostahili – mgomo.

Mimi si shabiki wa migomo ya aina hii lakini tulipofika sasa inaonekana hoja hazitoshi kuwashawishi watawala kufikiri. Mgomo siyo wa kukataa tu bali pia wa kudai kile kinachowezekana.

Kama taifa linaweza kutenga posho ya karibu bilioni 28 kwa watu 350 hivi na wakahalalisha inawezekana, nina uhakika taifa hilo hilo lina uwezo wa kutenga kiasi kikubwa tu cha fedha kuboresha mishahara na posho za madaktari karibu 2,000 tu ambao tunao!

Mgomo ni njia pekee na sahihi ya kutuma ujumbe wa kisiasa ambao umeshindikana kupokewa kwa njia za kidemokrasia na mazungumzo. Mazungumzo yamefanywa miaka nenda rudi lakini bado watawala wetu wanaona kama wanasumbuliwa na ‘madai’ ya madaktari.

Nasema madaktari hamna cha kupoteza isipokuwa utu wenu na hadhi yenu kama waponyaji. Mtaendelea kudharauliwa, kunyanyasika na kudhulumiwa huku na ninyi mkitamani muwe wanasiasa!

Si mmewaona madaktari wenzenu walivyoingia siasa wanavyonona. Hamna mtetezi wala wa kuwapigania isipokuwa ninyi wenyewe! Tangazeni mgomo na simameni pamoja mtasikilizwa. Msiposimama pamoja, mtaangamia mmoja mmoja!


RAIA MWEMA

No comments: