Monday, January 30, 2012

IPO HAJA YA KUOMBA HOJA YA DHARURA BUNGENI ILI KULITATUA SUALA LA MADAKTARINa Subi Sabato,

Ipo haja ya kuomba hoja ya dharura Bungeni ili kulizungumzia suala la mgogoro wa Madaktari na Serikali kwani hili ni suala linalouhusu umma wa Tanzania nzima.Wasipofanya hivyo itakuwa ni usaliti kwani raia wanakufa kwa kukosa huduma za wataalamu, wataalamu ambao wamedharauliwa kusikilizwa na kupewa majibu ya kuridhisha juu ya madai yao, kutoka kwa viongozi wa nchi wenye dhamana.

Nimesikitika sana kusoma mahali ati, Waziri Mkuu na baadhi ya viongozi hawakutaka kuwafuata Madaktari kwenye kumbi walimokuwa wamekutania za Don Bosco wala Star Light hotel kwa kuhofia usalama wa maeneo hayo. Ikiwa Serikali ina waajiriwa wa intelijensia, usalama na polisi wanashindwa kuchunguza raia wao kiasi cha Viongzi kutishika, mwananchi wa kawaida anapaswa kuwa mashakari kiasi gani? Huu si udhaifu wa waziwazi? Hao walinda usalama kazi yao ni kuchunguza mitandao jamii na meseji za simu zinazohusu watu na mahawara zao tu?Ikiwa viongozi walihofia kwenda kwenye kumbi kuonana na madaktari, ni kwa nini madaktari wasihofie kwenda kuwaona viongozi hao? Kwa nini iwe sawa kwao na si sawa kwa wengine?

Dhana ya uongozi kuwa kauli itatoka kwa kiongozi tu na mwananchi shuruti yake ni kupokea maelekezo daima dumu ni ya nchi gani? Sitaraji iwe Tanzania inayohubiri kuwa viongozi wake ni wasikivu kwa wananchi. Raia ndiye anayepaswa kutoa kauli kwa kuwa yote yanayofanyiwa kazi yanamhusu yeye, kawapa tu dhamana viongozi kusimamia. Hii nchi ya kuongozwa kwa kutisha watu haipo. Si sasa. Ile kasumba ya kutisha watu kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu si wakati wake huu. Nayo imekwenda na aliyeileta, tusilazimishane. Huu ni upuuzi mkubwa kabisa kuwatisha watu kana kwamba ni wajinga na hawajui wanachokitaka. Hawa viongozi hawajajifunza yaliyotokea kwenye nchi nyingine?

Uongozi wa mabavu huku mnajitapa mbele ya uso wa dunia kuwa ni nchi ya kidemokrasia ni upuuzi na ujinga wa hali ya juu. Kuwazuia watu kukutana katika kusanyiko la amani, ndani ya nyumba na si mtaani, ni kuua nguvu ya demokrasia ya uhuru wa kukusanyika na kuzungumza. Hawa Madaktari hawajaenda mtaani kuandamana, lakini kuwazuia kukutana ambako wamekuwa wakikufanya kwa amani hadi saa, ni dhahiri kuwa hatatakuwa na jinsi na hivyo wanalazimishwa kwenda mitaani. Nachelea kuamini kuwalazmisha kufanya hivi ni kwa lengo la kuonesha mabavu na ubabe. Ujinga ulioje! Kuwa Madaktari hawa baada ya kulazimishwa kutokukutana katika kumbi huru, basi watalazimika kwenda mtaani na huko ndiko nguvu ya mabavu itakapojidhihirisha kwa kuwapiga virungu, mabomu ya machozi na maji yanayowasha. Inasikitisha na kuhuzunisha kuwa ati hiyo ndiyo njia viongozi wanaojiita wenye upeo na demokrasia, wanaiona i sahihi, na ya kufuatwa.


Madaktari si watu wajinga hadi wadai isiyo stahili kwa kazi zao. Ninaudhika sana kumwona daktari anataraji huruma ya mgonjwa ya kupewa chochote, “chakula cha daktari aka CCD” ili aifanye kazi yake bila kuwaza atakavyotimiza mahitaji ya nyumba yake. Ipo dhana nyingine, kwamba daktari wanapaswa kujiajiri.

Hii ni dhana hafifu kwani maneno wanayosema watu wanaoshinikiza dhana hiyo hayaendani kabisa na 1. Kipato cha wananchi wanaopaswa ‘kukamuliwa’ malipo hayo. Ilivyo tu sasa wananchi hawawezi kujinunulia dawa au kulipia baadhi ya vipimo katika hospitali na zahanati za Serikali, wachilia mbali za binafsi. Watumiaji wakubwa wa huduma hizo ni matajiri na viongozi wa Kisiasa na Kiserikali, hao ni asilimia ngapi ya raia wote wa Tanzania? Raia wanaobaki watajipeleka wapi? Mtu unaposema waanzishe ‘private hospitals’ pia uangalie na jamii inayozungukwa. 2. Kipato cha daktari anayetakiwa kuanzisha hostpiali binafsi.

Mshahara wa dakatri wa kati ya laki sita hadi nane, ni kiasi cha kuweza kutosha kudunduliza kuianzisha hospitali yenyewe? Ingekuwa ni cha kutosha, wangekuwa na haja gani ya kusumbuana na Serikali wakati huu? Unaposema wakakope, umenayafahamu masharti na ukiritimba uliopo katika kupata mikopo hiyo? Wapo waliofanikiwa kufanya hivyo, waulize ni kwa mbinu gani na "connections" gani walizozitumia. Isitoshe, mshahara gani huo utakuwa "guarantee" kumwezesha kupata mkopo Benki wa kutosha kujiunga na wengine kuanzisha hospitali binafsi? Matokeo yake si ndiyo kuwa na hostpiali zisizokidhi viwango? Kamati za Bunge si zimekutana nazo huko mitaani wakati wa ukaguzi na kuzifungia?Ninaudhika kweli ninapomwona daktari anahangaika kufanya kazi hospitali tatu (wenyewe huita viosk) ili aimudu familia.

Si sahihi kumtwisha daktari, mwalimu, askari na kada nyingine mzigo wa kuombaomba na kutegemea huruma za wananchi ili kuendesha maisha. Si sahihi kumsababisha mwajiriwa yeyote aishi kwa kutegemea rushwa kutokana na mshahara usiokidhi mahitaji ya msingi. Ni dhambi na kufuru kumnyanyasa daktari, muuguzi, mwalimu n.k, kuwa kazi zao ni za wito kwa hivyo wanastahili kuwa na uvumilivu kana kwamba walijaaliwa roho ya ziada kuliko binadamu wengine, kwani ukweli ni kuwa walijaaliwa roho ya ziada ya kujali watu na si roho ya ziada ya kuonewa na kukubali uonevu.

Hii dhana ya "kazi za wito" ndiyo inayohubiriwa na viongozi kwa nia ya kuwaziba midomo na kuwakandamiza. Kwani, kazi halali isiyo ya wito ni ipi? Si sahihi kulinganisha kada nyingine kusema mbona walimu, viongozi wa dini n.k. hawadai madai ya ziadana kuacha kumlinganisha na wafanyakazi wa sekta nyingine na viongozi wa Kiserikali/Siasa. Tukilinganisha kwa ‘kizo cha chini’ tukumbuke kulinganisha na kwa ‘kizio cha juu’ vile vile. Isitoshe, kwa kada na sekta nyingine kutokudai stahiki zao, hakumzuii daktari au muuguzi kudai yaliyo yake na yanayompasa.

Kuwa mjinga na kuongozana kwenye kundi la wajinga ni kosa, ila mmoja katika kundi la wajinga anapoerevuka akajua anaonewa, anapodai haki yake, si mjinga huyo tena asilani. Na mjinga akierevuka, mwerevu yu mashakani.Madkatari msitetereke, vitisho havina budi kuja, hakuna popote ambapo imewahi kutokea 'smooth transition' hakuna, ni lazima kukubali kuingia hasara na gharama, pole ikiwa wewe ndiwe itakayekukuta, kumbuka hufanyi hivi kwa faida binafsi bali kwa ajili ya heshima yako ya sasa, kizazi kijacho na heshima ya “the noble profession”.


WAVUTI

No comments: