Wednesday, January 11, 2012

INASHANGAZA WANA -CCM KUGOMBEA HOJA WASIZOWEZA KUTEKELEZANa Elias Msuya,


KIKIWA chama tawala, kinachounda serikali, CCM kina majukumu makubwa mbele ya wananchi.
Kwa kufuatilia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010/2015, CCM iliahidi mambo mengi kwa wananchi huku kukiwa na kibwagizo cha maisha bora kwa kila Mtanzania.
Hadi sasa imebaki miaka minne tu ya utekelezaji wake, chama hicho sasa kimesahau wajibu wake, huku makada wake wakigombea hoja.

Tumeshuhudia hivi karibuni makada wa chama hicho wakigombea hoja huku kila mmoja akitaka kujionyesha kuwa msemaji hodari mbele za wananchi.
Kwa mfano, suala la posho za wabunge, tangu awali suala hilo lilikuwa likipingwa na Chadema ambapo wabunge wake hicho wakiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe waligoma hata kusaini karatasi za mahudhurio ili kukwepa posho hizo.

Wabunge wa CCM walikuwa mstari wa mbele kuunga mkono posho hizo. Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni Spika wa Bunge, Anna Makinda alitangaza azma ya kuongeza posho za wabunge kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000 kwa siku kwa kila mbunge.
Japokuwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alikanusha taarifa hizo, lakini Spika Makinda alikiri.
Jambo la ajabu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akatangaza kupinga posho hizo huku akieleza kuwa huko ni kuwasaliti wananchi.

Ni ajabu kwasababu, Spika wa Bunge (Makinda) ni kada wa CCM na ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Iweje watu wa chama kimoja watofautiane kimsimamo kwa suala nyeti kama hilo?
Kwanini Kamati Kuu ya CCM isimwite Makinda na kumwonya kwamba suala hilo siyo la kupigia debe wakati huu kutokana na hali ngumu ya maisha?
Kwanini CCM isiwe na msimamo mmoja kama chama wa kupinga posho hizo kama walivyofanya wenzao wa Chadema?

Matokeo yake sasa kila mtu anajifanya kuwa msemaji wa posho. Leo, ataibuka huyu na kujifanya kuwa mwema kwa wananchi, eti posho ni haramu, posho zimezidi mno. Mara mwingine ataibukia huku akimpinga.
Yametokea hivi karibuni ambapo Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye alipinga suala la posho wakati akihojiwa na kituo cha televisheni ITV. Kesho yake, Naibu Spika, Job Ndugai akampinga.

Hao wote wanatoka chama kimoja ambapo wangeweza kabisa kukaa na kukubalia lipi ni bora la kuzungumza mbele ya umma, badala ya kukurupuka tu.
Sikatai, inawezekana kabisa watu kutofautiana kwa hoja katika chama kimoja. Lakini, afadhali tofauti hizo ziwe kwenye vikao, siyo hadharani.

Mfano mwingine ni suala la ongezeko la nauli za kivuko cha Kigamboni, ambapo wabunge wa Dar es Salaam (wakiwamo wa upinzani) walipinga kauli ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ya kutangaza ongezeko hilo huku akiwabeza wananchi kuwa wakishindwa kulipa nyongeza hiyo, wapige mbizi, au wazunguke Kongowe au warudi vijiji walikotoka.
Hapo napo wanasiasa wakapata pa kushikia. Mbali na wabunge wa Dar es Salaam, waliompinga Dk Magufuli, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita naye ameibuka na kumpinga Dk Magufuli.

Ni kweli kama kiongozi Guninita naye ameonyesha kuguswa na maisha ya wananchi. Lakini, amesahau kabisa kwamba Magufuli ni kiongozi wa Serikali na pia ni kiongozi ndani ya chama.
Guninita kama kiongozi wa CCM alipaswa kuwasiliana na uongozi wa chama au kamati ya nidhamu ya chama hicho na wakiweza wamwite Dk Magufuli ili kumuuliza kulikoni.
Baada ya kumjadili chama kitoke na msimamo wake mbele ya wananchi. Hiyo ndiyo nidhamu ndani ya chama.

Lakini, mambo yalivyo kwa sasa ni shaghalabaghala. Msimamo wa CCM kama chama haueleweki katikia suala la Kigamboni. Waziri Magufuli anayetoka CCM ana msimamo wake, Wabunge wana msimamo wao na wenyeviti wa chama wana misimamo yao.
Hivi kweli hiki ndiyo chama kilichoahidi kuitekeleza ilani yake ya uchaguzi ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania? Kitayatekeleza vipi wakati kila kada anasema lake?

Wakati makada hao wakiendelea kulumbana kuhusu kero za wananchi, mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete amekaa kimya. Hadi leo hatoi msimamo wake kuhusu nyongeza ya posho za wabunge, wala kuhusu kero zinazowasumbua wananchi.
Rais kama kiongozi wa chama na Serikali hapaswi kukaa kimya bali awaite watendaji wake wanaolalamikiwa na kupanga mambo sawasawa.

Haya malumbano yanayofanywa na makada wa chama chake yanakidhalilisha chama mbele ya umma.

Viongozi wake ( CCM) wanapaswa kujadiliana mambo yao kwenye vikao na kutoka na msimamo wa pamoja. CCM ndiyo chama dola kinachounda Serikali.
Viongozi na watendaji wa serikali wanatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM. Wanapokwenda kinyume waitwe wahojiwe, siyo kupingwa kwenye majukwaa ya siasa. Afadhali kazi hiyo wawaachie wapinzani.


MWANANCHI

No comments: