Thursday, January 5, 2012

HAMAD RASHID ANG'OLEWA CUF


Aziza Masoud na Talib Ussi, Zanzibar


HATIMAYE Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake watatu wamefukuzwa uanachama wa CUF kuanzia jana. Hatua hiyo ilichukuliwa na zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho katika kikao chake kilichofanyika hapa.

Uamuzi huo umekata mzizi wa fitina wa hatma ya Hamad na washirika wake hao kisiasa ndani ya chama hicho, baada ya kuibuka mvutano wa muda mrefu kati yake na uongozi wa juu.

Mvutano huo uliochomoza zaidi baada ya Hamad kutangaza kuwania nafasi ya Katibu Mkuu inayoshikiliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa na Hamad ambaye ameiita kuwa ni ya kihuni kwani imekiuka amri ya Mahakama iliyotangaza kusitishwa kwa kikao kilichochukua uamuzi huo.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alithibitisha kuvuliwa uanachama kwa Hamad na kuwataja wengine walioondolewa pia kuwa ni Mjumbe wa Baraza Kuu (Tanga), Doyo Hassan Doyo, Mjumbe wa Baraza Kuu (Pemba), Shoka Khamis Juma, Mjumbe wa Baraza Kuu Unguja, Juma Saanane na Mjumbe wa Baraza Kuu (Mbeya), Yassin Mrotwa.

“Kwa mujibu wa katiba ya chama, wasioridhika na uamuzi huo wanaweza kukata rufaa kwenye mkutano mkuu wa taifa,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Ismail Jussa akizungumza jana jioni na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Ujerumani (DW), alisema haoni kama hatua hiyo ya kuwafukuza wanachama hao akiwamo Hamad ambaye aliwahi kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kunaweza kuhatarisha mustakabali wa chama hicho.

“Ni kweli Hamad ametoa mchangao mkubwa ndani ya chama. Lakini wakati mwingine unapima faida na hasara sasa hivi Hamad alikuwa anaelekea kuvuruga chama,” alisema Jussa

Hamad: Ni uamuzi wa kihuni

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho, Hamad alisema anashangazwa na kiongozi wa nchi (Maalim Seif), kushindwa kuheshimu amri ya Mahakama na kuendelea na kikao ambacho ilikuwa imeamuru kisitishwe.

“Kiongozi wa nchi anakaidi uamuzi wa mahakama... uamuzi huu mimi nauita ni uamuzi wa kihuni, nimekwenda kwenye kikao naulizwa maswali ambayo wao wamejipanga na mashahidi wao mimi sijajipanga, sina shahidi nawaambia wanipe maswali ili nipate muda wa kuyajibu na kuandaa mashahidi kama wao hawataki, sasa demokrasia ipo wapi hapo?” alisema Hamad.

Hamad alisema hati ya kusimamishwa kwa kikao hicho ilifika ukumbini hapo saa 6:10 mchana, lakini wajumbe wa kikao hicho walionekana kuipuuza na kuendelea nacho na hati iliyopelekwa makao makuu ya Dar es Salaam saa 2:00 jana ilikatiliwa kupokewa akidai kwamba ni kwa agizo kutoka kwa viongozi wakuu.

Alisema hati ya mahakama inaonyesha kwamba wanatakiwa kwenda mahakamani Februari 14, mwaka huu na kusema kwamba uamuzi wa kuaminika utatolewa huko kwani katika chama hicho wanachama wengine wanaonekana hawana nguvu kama katibu mkuu.

Alisema wanachama wote wa CUF wanapaswa kufurahi kwani hajaumizwa na uamuzi kwa kuwa viongozi wake wamekuwa wakionekana kuhubiri haki sawa huku wakienda tofauti na msimamo wa chama.

“Maalim Seif kila siku anaonekana anahubiri haki sawa kumbe hana lolote, anakandamiza tu watu kwa kuharibu chama na kutoa maamuzi kibabe. Mimi sipo tayari kuburuzwa, wakitaka tuelewane haki wanayoihubiri iwe inatendeka kweli,” alisema Hamad.

Kwa upande wake, Shoka Khamis ambaye alikuwa Mbunge wa Micheweni, Kaskazini Pemba katika Bunge la Tisa, alisema kwa mujibu wa katiba ya CUF hamjui aliyemtuhumu kwani haiwezekani mtu asomewe shtaka bila kujua anayemtuhumu.

“Nimejifundisha mengi sana CUF mazuri na mabaya, lakini leo kwa sababu wamenifukuza ngoja niseme mabaya, CUF sisi ni CCM B kama wanavyosema wenzetu. Chama kina sifa mbaya ya kufukuza watu, lakini anayefukuza wenzake, Seif Sharif Hamad yeye anajiona kama mungu hafanyi makosa,” alisema Shoka.

Alisema hawapo tayari kujiunga na chama chochote cha siasa kama maneno yanavyosambazwa kuwa watahamia Chadema. Alisema watafufua Chama Cha Wananchi (CCW) ambacho kiliungana n Kamahuru na kuipata CUF.

“Tuna mpango wa kuanzisha chama kingine kwani CUF kwa sasa kimeshakuwa chama cha mtu ambaye ni Seif na siyo cha wananchi kama kinavyojulikana katika siasa za nchi hii,” alisema Shoka.

Hamad na hujuma

Desemba 27, mwaka jana Hamad aligoma kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Nidhamu, akitoa sababu tano huku akiibua tuhuma nzito za kunasa waraka wa mawasiliano uliotumwa kwa barua pepe na Maalim Seif kwenda kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ukionyesha mpango wa kumshughulikia.

Sababu ya pili, alisema baadhi ya walioteuliwa katika kamati hiyo ya Nidhamu na Maadili walikwisha mtuhumu hadharani na kumtia hatiani hivyo, kikao hicho kisingeweza kumtendea haki.

Alitaja sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa kuwa ni kutoelezwa tuhuma zake hasa vifungu vya Katiba alivyodaiwa kuvikiuka.

Pia alitaka apewe hadidu za rejea za kikao kilichounda Kamati ya Nidhamu na Maadili kwa sababu haipo kikatiba, hakuna chombo kama hicho. Aligoma pia kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa tayari alibaini njama za kumshughulikia zilizosukwa na Maalim Seif na Lipumba.

Hamad Rashid alijikuta kwenye mgogoro huo baada ya kutangaza dhamira yake hiyo ya kugombea nafasi ya katibu mkuu mwaka 2014.

Kuanzia hapo akajikuta ameingia kwenye mgogoro na chama hicho kiasi cha kunusurika kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akigawa misaada katika matawi ya chama hicho, Kata ya Manzese.


MWANANCHI

No comments: