Wednesday, December 28, 2011

TAHADHARI YA MVUA KUBWA YATOLEWATaarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zinatahadharisha kutokea mafuriko mengine makubwa katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

Taarifa ya TMA imeonya wakazi wa jijini Dar es Salaam kwamba kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini mafuriko makubwa yatatokea kati ya Desemba 29 hadi 31 mwaka huu.

TMA wanasema kwamba mvua kubwa na ambazo zinaweza kusababisha mafuriko zinatarajiwa kunyesha kwa wingi katika mikoa ya Dar e Salaam, Pwani , Mtwara , Lindi na Kisiwa cha Unguja.

Pia maeneo mengine ambayo yatakumbwa na mvua hizo ni Nyanda za Juu Kusini Magharibi katika Mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa na Kanda ya Kati katika Mikoa ya Dodoma na Singida.

Vilevile, taarifa hiyo imetaja kwamba Mikoa ya Kigoma, Tabora, Kilimanjaro, Arusha na Manyara nayo inatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua kubwa

Ni dhahiri kwamba mvua zilizonyesha wiki jana zimeleta madhara makubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, hata kusababisha maelfu ya watu kukosa makazi ya kuishi, kusababisha vifo vya zaidi ya watu 40 na nyumba zao kuzolewa na maji.Kutokana na mvua zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo, udongo umetuama maji mengi hivyo maji yatakuwa hayana sehemu ya kwenda.

Kutokana na hali hiyo ni dhahiri mvua hizo zitakaponyesha zitaweza kuleta mafuriko makubwa hata kuliko yale ya nyuma.Hivyo basi, kutokana na tahadhari hizi za mamlaka ya hali ya hewa, tungependa kuchukua nafasi hii kuwataka wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuhama mara moja ili kuepuka madhara makubwa ya mafuriko ya siku tatu zijazo.

Kwa kuwa tunatambua kwamba mafuriko yanaweza kuleta madhara kwa watu wote hata wale ambao hawaishi mabondeni hivyo tunatoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini katika kipindi hiki kigumu cha kuishi katika Jiji la Dar es Salaam.

Tunaandika maoni haya huku wenzetu ambao walikumbwa na mafuriko katika maeneo ya mabondeni wakiwa tayari wamerejea huko licha ya kupewa tahadhari na Serikali na hata kutengewa maeneo ya kukaa kwa muda wakati wakitafutiwa eneo la makazi ya kudumu na yenye usalama.
Sisi wa Mwananchi tunaona hatua ya wakazi wa mabondeni kurejea katika maeneo hayo ni sawa na kuamua kujilipua wenyewe.

Ndio maana bila kumumunya maneno, tunaziomba mamlaka za Serikali kuchukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuwaondoa kwa nguvu mabondeni ili kuwapusha na maafa yatokanayo na mafuriko.

Tunaamini kwamba Serikali kwa upande wake, imejitahidi kutenga eneo la muda ambalo wahanga wa mafuriko wanaweza kujisitiri, lakini pia imetenga eneo la Mabwepande kwa ajili ya makazi ya kudumu kwa wahanga hao wa mabondeni.

Angalizo ambalo tungependa Serikali ikatafakari ni uwezekano wa familia za wapangaji nao kupatiwa maeneo ya makazi huko Mabwepande baada ya wenye nyumba kugaiwa maeneo.
Tunasema hivi kutokana na uhalisia wa maisha ya watu hao ambao ni wapangaji wa nyumba zilizoko mabondeni.

Kwanza kabisa tunaamini mpaka mtu kuamua kwenda kupanga nyumba ya bei rahisi katika eneo hatari ni kutokana na umasikini uliokithiri. Hivyo basi jaribio lolote la kusaidia wahanga wa mafuriko, lisiwaache nyuma wapangaji ambao mali zao ndogo walizozipata shida kutokana na kipato kidogo zimetekelea.
Link
Vilevile, tunalaani tabia ambayo imejitokeza kwa watu ambao hawakukumbwa na mafuriko kwenda mstari wa mbele ili wapewe viwanja. Tunasema tabia ni kukosa utu na uzalendo.
Ni maoni yetu kwamba Watanzania wote watachukua tahadhari, ikiwa ni pamoja na wale waishio mabondeni kuhama moja kwa moja.MWANANCHI

No comments: