Friday, December 30, 2011

RIPOTI YA UDA KUTOLEWA JANUARY

Aidan Mhando
na Fidelis Butahe,

MKAGUZI na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema ripoti ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), ipo katika hatua za mwisho na ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao, kila kitu kitawekwa wazi.
Wakati CAG akiweka wazi kuhusu ripoti hiyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametoa taarifa ambayo pamoja na mambo mengine, inasisitiza ripoti hiyo kutolewa haraka

Agosti 13 mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), George Mkuchika alimwagiza CAG kufanya ukaguzi huo ndani ya mwezi mmoja, lakini kutokana na majukumu mengi ya ofisi hiyo, kazi hiyo ilikabidhiwa Kampuni ya Kimataifa ya KPMG.
Akizungumzia na gazeti hili jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, CAG Utouh, alisema kuchelewa kukamilika kwa ripoti ya UDA kunatokana na jitihada kubwa zinazoendelea za kutafuta namna ya kupata ufumbuzi wa kina wa tatizo hilo.

Hata hivyo, Utouh alisema ukaguzi wa shirika hilo unakaribia kufikia tamati na kuongeza kwamba, kwa sasa upo katika hatua za mwisho.

“Najua watu wanahamu ya kufahamu ukaguzi wa ripoti ya UDA unavyoendelea hasa kujua kitu gani kimejiri katika ukaguzi huo, lakini nataka niseme sio kazi nyepesi kama wanavyofikiria na kwamba inahitaji muda mwingi ili kuifanya kwa umakini na kutoa majibu sahihi,” alifafanua CAG Utouh.

“Ukaguzi unaendelea na sasa umefikia katika hatua za mwisho kukamilika, itakapofika mwezi wa kwanza (Januari) mwishoni, nitawafahamisha kipi tulicho kiona katika ripoti hiyo ukaguzi wa UDA bila kuficha jambo lolote,” aliahidi Utouh na kuongeza:

“Watanzania wote hasa watu wa Dar es Salaam najua wanapenda kufahamu kitu gani kinaendelea mpaka sasa, lakini nataka niwatoe shaka, kila kitu kitakwenda sawa na nitaiweka wazi (ripoti) itakapo kamilika kwa muda huo nilioutaja.”

Kwa mujibu wa Utouh, hatua ambazo zimeshafikiwa katika ukaguzi huo ni nzuri na kinachotakiwa ni Watanzania kuwa na subira katika jambo hilo kwani kila kitu kitaelezwa katika ripoti ya ukaguzi itakapo kamilika rasmi.

“Ukaguzi ni jambo ambalo linahitaji muda ila kitu ambacho naweza kuwaambia Watanzania kwa sasa ukaguzi wa UDA ujumuisha vitu vingi hivyo unahitajika umakini wa hali ya juu ili kutoa majibu sahihi,” alisisitiza.

Kauli ya Mnyika
Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo, Mnyika ameitaka Serikali kutoa taarifa kuhusu hatua iliyofikia juu ya ukaguzi na uchunguzi wa tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa UDA

Katika taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Mnyika ameitaka Serikali kuagiza kusitishwa mara mojakwa kile alichokiita, mkataba batili na uamuzi haramu uliofanyika kukabidhi hisa, mali na uendeshaji wa kampuni ya UDA kwa Kampuni ya Simon Group Limited.

Alisema katika kipindi cha uchunguzi, masuala yote ya kampuni hiyo yaratibiwe na bodi huru, itakayoundwa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria.Taarifa hiyo inaeleza kuwa ukimya huo umeanza kupoteza matumaini juu ya hatma ya ukaguzi na uchunguzi huo ambao Serikali iliahidi ungefanyika katika kipindi cha mwezi mmoja, lakini mpaka sasa, miezi minne imepita.

“Pinda anapaswa kutoa taarifa kwa kuwa alitoa agizo bungeni Agosti 4, 2011 wakati wa kipindi cha maswali kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 38 (4), ” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mnyika alisema agizo hilo lililenga kuvielekeza vyombo vya dola kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) , CAG na Ofisi ya Mkurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma husika.Alisema tangu agizo hilo litolewe, umma wala wabunge hawajaelezwa hatua ambayo Takukuru na Ofisi ya DCI imefikia katika uchunguzi wa tuhuma hizo.

Mnyika alisema mpaka sasa kilichofanyika ni ile hatua ya Agosti 13, mwaka huu ambayo Mkuchika alimkabidhi CAG barua ya kumtaka afanye ukaguzi maalumu katika kipindi cha mwezi mmoja.

“Miezi miwili ilipita bila ukaguzi husika kukamilika na hatimaye mwezi Oktoba, CAG akatangaza kwa umma kwamba ameshindwa kumalizia ukaguzi husika kutokana na kutingwa na majukumu mengine,” inaeleza taarifa hiyo.
Alifafanua kwamba kutokana na hali hiyo, CAG alieleza kwamba ofisi yake imeiteua kampuni binafsi ya KPMG kufanya ukaguzi husika katika kipindi cha mwezi mmoja.

“Takribani miezi miwili imepita bila ukaguzi huo kukamilika hivyo CAG anapaswa kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa juu ya ukaguzi huo na kuhakikisha kwamba ukaguzi unakamilika kwa haraka,” alisema katika taarifa hiyo.

Mnyika aliongeza kwamba mpaka sasa, uchunguzi uliokuwa ufanywe na Kamati iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), bado haujaanza kutokana na uongozi wa Bunge kuelekeza kwamba uchunguzi huo unapaswa kusubiri ukaguzi wa CAG.

Alisema hali hiyo imevifanya vyombo vya uwakilishi wa wananchi, Bunge na baraza la madiwani kubanwa kiufundi kuchukua hatua kwa kuwa vinasubiri uchunguzi huo.

“Wakati ambapo ukaguzi haujakamilika na Kampuni ya Simon Group imeshaingizwa katika umiliki na uendeshaji wa kampuni ya UDA,” alisema na kuongeza:

“Wakati ukaguzi huo ukiendelea kuchelewa, maofisa waliohusika katika jiji, kampuni ya UDA, wizara mbalimbali na taasisi za serikali wanaendelea na utumishi kama kawaida katika mazingira ambayo yanaacha mianya ya hujuma kwa mali za kampuni na vielelezo mbalimbali.”

Inaeleza kuwa maamuzi yote yaliyofanywa na Mstahiki Meya wa Dar es Salaam, Didas Masaburi kuhusu kampuni ya UDA yanayotajwa kuridhiwa na vikao vya jiji ni batili kwa kuwa yalifanyika kwenye vikao visivyokuwa halali bila kuzingatia sheria na yalifanyika bila ridhaa ya wabunge ambao ni Wajumbe wa Baraza la Halmashauri ya Jiji.

Taarifa hiyo ilisema kwamba katika kufanya ukaguzi na uchunguzi ni muhimu kwa serikali kuzingatia kuwa pamoja na udhaifu kwenye uongozi wa Jiji la Dar es salaam, matatizo ya UDA yamechangiwa pia na Ofisi ya Msajili wa Hazina kutokuwa makini katika hatua zote kwa kushirikiana na CHC katika masuala ya ubinafsisaji wa UDA.

Sakata la kuuzwa kwa UDA liliibua mjadala mzito bungeni na kuwaingiza katika vita ya maneno Meya wa Jiji la Dares Salaaam Dk Masuburi ambaye aliwaambia baadhi ya wabunge wa mkoa wa Dares Salaam kwamba, wamekuwa wakifikiri kwa makalio badala ya ubongo.MWANANCHI

No comments: