Thursday, December 8, 2011

PALE POLISI WANAPOJIONA WAKO JUU YA SHERIA

Na Baraka Mfunguo,

Hivi majuzi kuna tukio la kusikitisha limejitokeza baina ya raia na Jeshi la Polisi mkoani Mtwara. Na Jeshi la Polisi kwa kuamua kuupotosha umma kupitia vyombo vya habari wameamua kupotosha kabisa na kujiona wao ndio wametendwa ilihali wao ndio chanzo cha tukio lenyewe.
Tukio lenyewe liko hivi, Maaskari ambao hupiga doria kwa kutumia pikipiki maarufu kama tigo walikuwa wakipiga doria maeneo ya Stendi na soko kuu mjini Mtwara.

Kwa kuwa Jeshi la Polisi ndilo lenye dhamana ya kusimamia sheria na usalama wa raia, basi wao wanajiona wako juu ya kila kitu, wakapita na pikipiki yao wakamgonga mtu na mtoto aliyekuwa akivuka barabara na kuwajeruhi wote vibaya. Kibaya zaidi baada ya wao Polisi kugundua wamefanya kosa, wakaanza kukimbia. Hali hiyo ikaamsha hisia na hasira miongoni mwa wananchi na wakazi waliolizunguka eneo hilo na kuanza kuwashughulikia. Tukio hilo liliendelea mpaka walipoitana na kuja nao kuwapiga wananchi waliomo na wasiokuwamo. Ikafikia wakati mpaka wananchi wakataka kukipiga kituo chao kidogo moto kwa hasira ya unyanyasaji na uonevu wao.

Mpaka sasa Jeshi la Polisi kupitia msemaji wao ameshatangaza kupitia vyombo vya habara kwamba wamewakamata watu kadhaa waliohusika na tukio hilo na watapelekwa mahakamani muda wowote ili sheria ya kumpendelea Polisi ichukue mkondo wake. Nasema sheria ya kumpendelea Polisi ichukue mkondo wake kwani kwa mujibu ya maelezo ya msemaji huyo, inaonekana ameegemea katika upande wa Polisi kwani naye ni mmoja wao na hakuangalia upande wa raia ambao wanadai wanawalinda pamoja na mali zao.

Suala hili lililotokea linanipa mashaka na maswali mengi. Kwa nini matukio mengi ya fujo baina ya raia na Polisi yajitokeze maeneo ya soko kuu na Stendi? Je zaweza kuwa ni sababu za kisiasa, Je zaweza kuwa ni sababu za kijamii ambapo wananchi wamekuwa hawasikilizwi kero zao hata pale wanapoamua kuziweka wazi, Je Jeshi la Polisi limekuwa Jeshi la kuwalinda matajiri, watu wenye vyeo na mafisadi na kuwaonea watu wa chini? Picha inayoonekana na picha inayotaka kufichwa na Jeshi la Polisi kwa kutumia vitisho vyao ni kwamba, wao ndio walianza kwa kugonga watu na kukimbia na hatima yake ikaanzisha jazba miongoni mwa wananchi na pia inaelekea ndio tabia yao na wananchi wakipeleka malalamiko yanayowahusu wao wamekuwa hawasikilizwi na matokeo yake kuonekana wao ndio wakosaji na kupelekea kuchukua sheria mikononi. Lakini tujiulize Sheria ni kitu gani na Haki ni Kitu gani? Sheria na Haki ni vitu viwili tofauti. Hapa tunaona wananchi wanadai Haki yao na kwa upande mwingine Polisi wakidai sheria yao.

Mahusiano baina ya Wananchi na Jeshi la Polisi ni ya mashaka. Kwani hata mimi binafsi ukiniuliza kama nina imani na jeshi langu sitaweza kukupa jibu la moja kwa moja kutokana na uzoefu wangu mdogo nilio nao juu ya Jeshi hilo. Na sasa Je Mwananchi mwingine atalichukuliaje Jeshi hilo? Ni jeshi lililojaa uonevu, Rushwa,vitisho na kujiona wao wako juu ya sheria dhidi ya wananchi wengine. Na wapo wale ambao aghalabu utawasikia wakilisifia Jeshi hili ni lazima uanze kuwatilia mashaka na kujiuliza kuna jipya lipi ambalo wameliona na hata kama itatokea basi hiyo itakuwa ni bahati nasibu.

Mpaka sasa biashara zote soko kuu zimefungwa wananchi wa kawaida wanashindwa kwenda kununua bidhaa zao sokoni kwa sababu eti polisi wamepigwa kwa kugonga mtu , waendesha pikipiki na bajaji wamenyang'anywa vitendea kazi vyao kwa sababu ya tukio hilo. Wao Polisi wanadhani wamewakomoa wananchi wasijue mbegu ya chuki wanayoipandikiza na ambayo itakayokuja kuwatafuna wao wenyewe kwa kudhani hayo magwanda yao watayavaa milele. Magwanda yao watayavaa kwenye kaunta zao vituoni mwao wakati nguo za kawaida watazivaa uraiani maisha yao yote. Sasa sijui tuseme ni nani ambaye yuko juu wao ama raia?

Ifikie wakati sasa wananchi tuamke na tusimame na kukemea upotoshwaji huu ulio dhahiri unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa kigezo cha Kutetea, kuilinda na kuisimamia sheria , ulinzi wa raia na mali zao kama kauli za kwenye makaratasi tu. Hali halisi inajulikana na matukio mengi yanajulikana. Ifikie wakati mwananchi wa kawaida aheshimiwe, athaminiwe na ifikie wakati hao wanaojiita Wana Jeshi wajione wao ni raia wa kawaida na pindi janga, vita au lolote litakalotokea katika nchi hii Mwananchi wa kawaida atashiriki na ataathirika na janga hilo kuliko wao wanavyofikiri itakuwa. Na ifikie wakati vyombo vya sheria kama mahakama viangalie na upande wa pili wa sarafu na ifikie wakati katika nchi hii tuwe na wapelelezi binafsi badala ya kuwategemea hawa Polisi ili haki iweze kutendeka.

No comments: