Friday, December 2, 2011

OPERESHENI BARAKUDA YARUDI AFRIKA -IILinkNa Marie Shaba,

JUMA lililopita tuliona kitendo cha kumfunga Lumumba na wenzie mwaka 1959 kilifanya Wakongo wapandwe na ari zaidi katika kudai uhuru kamili. Januari, 1960 Serikali ya Eyskens ikasalimu amri na kutangaza Juni 30, mwaka 1960 Kongo itapata uhuru baada ya kushinda vikwazo vingi vya wakoloni isipokuwa kimoja tu.

Wabelgiji walipoiteka Kongo walisingizia eti ni kuokoa maisha ya waafrika kutoka kwa wafanyabiashara ya utumwa wa kiarabu. Kabla ya Juni 30, mwaka 1960, wakoloni wakatambua, kwa nguvu za umma, Lumumba ataongoza Serikali. Ndipo Bunge lao bila idhini ya Wakongo walibadili kipengele kwenye Katiba kuigawa Kongo kimajimbo.

Lumumba alitaka uhuru wa kiuchumi tangu siku ya kwanza ya uhuru. Akasema; “Tutahakikisha ardhi yetu inawafaidisha watoto wetu. Tutafanya tathmini ya sheria zote na kutunga zingine kwa kuzingatia haki na usawa… Wakongo washike hatamu katika kila sekta” na katika hili la hatamu akaanzia afrikanaizsheni jeshini. Hili liliwakera wakoloni.

Wazungu wakuzua propaganda kuwa majeshi ya Lumumba yanawabaka wanawake, na wazungu wanakimbia vikosi vyake katili. Ubeligiji ikatuma majeshi Jimbo la Katanga na machafuko ya Kongo yakaanza Julai 10, mwaka 1960 na siku iliyofuata Julai 11, Jimbo la Katanga lenye tajiri wa madini likajitenga.

Mataifa yenye nguvu za kijeshi ya Magharibi yalibariki “WAASI’ na kumbana Lumumba kwa hila na kwa wazi. Safari hii ilikuwa kuiokoa Afrika kutoka ubeberu wa Wakomunisti! Lumumba hakuwa mkomunisti, alikuwa kiongozi mzalendo lakini walichotaka ‘wakoloni’ ni rasimali za Kongo..

Kikosi cha Belgo-Katanga kilizuia ndege iliyo mchukua Kasa Vubu na Lumumba, isitue Katanga kwa hofu ya kuenea kwa vuguvugu la uzalendo. Lakini migomo ilienea na Balozi wa Ubelgiji, Jean Bosch, akafoka vuguvugu lazima lizimwe na akaanza kutafuta kiongozi atakae shika nchi baada ya kumg’oa Lumumba.

Akampata waziri mmoja wa Lumumba, Justin Bomboko ambaye alikuwa anapeleka taarifa zote ubalozini. Julai 12, mwaka 1960 Serikali ya Lumumba ikatuma simu UNO (Umoja wa Mataifa) kuomba msaada wa kukabiliana na waasi na majeshi vamizi ya kigeni. Katibu Mkuu wa UNO, Dag Hammarskjold, akaueleza ujumbe wa Ubelgiji kwamba “…kama jeshi la wazungu litaingilia, itakua ni kuhalalisha kinachoendelea huko” akimaanisha maasi.

Julai 14, mwaka 1960, Baraza la Usalama likaunda kikosi cha UNO kuisaidia Serikali ya Kongo hadi pale itapotengemaa. Ubelgiji iliondoa askari wake na ikaendelea kuimarisha waasi na hakuna aliyeishutumu. Hammerskjold aliwawekea ‘mikwara’ wote waliotaka kumsaidia Lumumba kwamba wapitishe misaada yao UNO.

Naibu Waziri Mkuu, Antonie Gizenge, alifoka “Wakongo hatuelewi, iweje sisi watendwa katika nchi yetu, tunanyang’anywa na kunyimwa silaha, Ubelgiji ambao ni wavamizi wana silaha….UNO inaruhusu waasi ambao tumewatangaza si halali wajizatiti na Wabelgiji watambe kama Kongo kwao!”

Wakati Lumumba anaendelea kutema cheche Wabelgiji walimuajiri kanali Frederic Vandewalle, kiongozi wa ujasusi kabla ya uhuru aje kuongoza shughuli za maasi. Huyu aliijua Kongo na Wakongo na nyuma ya pazia alifanya kazi kubwa na chafu katika kusambaratisha Serikali ya Lumumba. Mengi ameandika katika kitabu chake kiitwacho “Siku 1004.”

Hammerskjold baada ya kuzongwa sana akawaambia wasaidizi wake kwamba atashauriana na Tshombe ili amhakikishie hatakuwa amepoteza malengo kwa kukukubali majeshi ya UNO. Malengo gani hayo? Picha iliyojengwa ni kwamba Kongo haitawaliki chini ya Lumumba na kuna hatari ya kupoteza mashamba, viwanda na shughuli za kibiashara.

Mfalme Baudounin naye alimponda Lumumba na kumsifia Tshombe kwamba ni mwaminifu, kwa hiyo Ubelgiji ina wajibu wa kumsaidia na UNO kamwe isikubali kuitoa Katanga kwa Serikali ya Kongo. Magazeti kama De Standaard la Julai 16, 1960 liliandika; “Lumumba ni mwanamapinduzi anayetaka kuleta vurugu na fujo, wakati Katanga kuna utulivu na amani kutokana na msaada wa wazungu.”

Julai 26, 1960 likaandika; “ili kuikoa Kongo ni lazima wenye msimamo mkali waondoke ….na kila jimbo lijitawale….” La Libre Belgique lilipakaza Julai 19, 1960 kwamba Lumumba alipokua Marekani alilala nyumba ya wageni wa kiserikali, “… na mtumishi wa pale ni mwanamke, mzee, mzungu. Sijui kama huyo mama atasalimika!”

Marcel de Corte, msomi wa falsafa ya maadili mema alitaka Lumumba auawe akijenga hoja kwamba “…ni mnyama… maafisa wa kibelgiji wanalia kwa hasira kwa sababu wanazuiwa kummaliza” La Gauch baada ya kuuwawa kwa akina Lumumba liliandika Machi 4, 1961; “Vyombo vya habari vimekuwa na hasira na Lumumba kuliko hata Hitler!”

Maasi yaliendelea , Agosti 9, 1960 Kusai Kusini ilijitangazia uhuru chini ya Albert Kalonji. Ilibidi Serikali ya Kongo ichukue hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo viliunga mkono maasi. Ubelgiji ikadai Lumumba anakandamiza uhuru wa habari na sasa ni utawala wa kipolisi na maisha ya wengi yako hatarini.

Agosti 12, 1960 Hammerskjold alitua Kongo kuzungumza na Tshombe, na walidai UNO ichukue nafasi ya majeshi ya Ubeligiji, ili ya Serikali yasiingilie Katanga. Na kama jeshi la Serikali litaingilia, itabidi UNO iwe upande wa waasi.

Hammerskjold aliambiwa wazi na msaidizi wake Bunche, “Tshombe ni kibaraka wa Belgiji na bila UNO asingethubutu kuasi” lakini hakusikiliza kwani msimamo wa wazungu ulikuwa ni kuisambaratisha Serikali ya Kongo na Julai 26, 1960 Hammerskjold alimtambua muasi Tshombe kiongozi halali wa Katanga.

Agosti 15, 1960 Lumumba alimwandikia Hammerskjold wakati yuko Kongo; “…baada ya kuongea na waziri wa nje Ubelgiji, …..na kudharau serikali ya Kongo… watu na serikali ya Kongo tumepoteza imani na Katibu Mkuu Hammerskjold … tunachohitaji ni waangalizi huru waje waangalie hali halisi ya Kongo… na majeshi ya Afrika na Kongo.”

Gazeti la The Times la Agosti 16, 1960 liliandika Hammerskjold alionyesha wasiwasi kuhusu uhalali wa Lumumba kuongea kwa niaba ya Serikali na akamwandikia Rais Kasa Vubu “… tunaimani na busara zako na UNO itaendelea kutoa ushirikiano alimradi masuala ya utaifa na rangi yazingatiwe ili kufikia lengo letu…”

Kwa kutelekezwa na UNO, Lumumba aliwajibika kuzima fujo na uvunjwaji wa sheria uliofanywa na waasi. Agosti 22 na 23, 1960 askari 1,000 wa Serikali walielekea Kusai na Wabelgiji walijua majimbo yote yanawafuasi wazalendo.

Septemba mosi, 1960 Mobutu Mnadhimu Mkuu aliamua kusitisha vita Kasai bila kushauriana na Serikali. Ndege za majeshi ya Serikali zilihujumiwa na UNO ilikataa kuwapa mafuta. Wakati huohuo, kulikuwa na mipango ya kumpindua Lumumba. Septemba 5, 1960 Lumumba alivuliwa madaraka, na kwa msaada wa UNO viongozi wapya wa kisiasa na kijeshi wakasimikwa Mobutu akiwamo.

Machafuko ya Kongo mwaka 1960 hadi 1964 yanadhihirisha UNO ilikubali kutumiwa na nchi za Magharibi kumpindua na hatimaye kumuua Lumumba. Nchi hizo ziliamini kwamba Lumumba aliwakilisha hatari kubwa zaidi katika kufanikisha mipango ya kuitawala kiuchumi Afrika.

Rais wa Marekani Eisenhower, Waziri Mkuu wa Uingereza na mawaziri wao wa nje walijiuliza; “Kwa nini hatumuui Lumumba sasa? Kama atarudi madarakani kutakuwa na shinikizo kuhusu suala la Katanga, ambalo litatuletea mgogoro wa kisheria… sasa ndio wakati mzuri wa kumshughulikia Lumumba”. Juma lijalo tutaona jinsi Lumumba alivyosalitiwa na taadhira ya kifo chake kwa Afrika


RAIA MWEMA

No comments: