Friday, December 9, 2011

NYAMA CHOMA ZA TUMETHUBUTU,BIA ZA TUNAWEZA NA HASA WISKI ZA TUNASONGA MBELE.
Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.

Frank,
SITAKI maneno yako marefu kama tegu. Nataka uje hapa tuonane. Ni rahisi sana kuwa kama waheshimiwa na kukana kwamba hukupokea posho hili au lile na kwamba watu wanakuandama tu, lakini siwezi kujua hadi nikutazame jicho kwa jicho. Nilikufunulia moyo na kukuelezea wasiwasi wangu, kwa nini huwezi kuja angalau mara moja maana bila kukuona na kupima ukweli wako, siko huru hata kidogo.

Hata mimi ningependa kuacha kazi na kuja nyumbani mara moja maana kilichonipa moyo ni kwamba nafanya kazi hapa kwa ajili ya kujenga maisha yetu ya baadaye. Sasa kama wewe umethubutu na kusonga mbele kwa wengine, basi ufaidi mwenyewe huko huko, achana na mimi nipambane na dunia duni ambamo wachache wanatambia mafanikio na sisi tulio wengi tunakanyagwa-kanyagwa.

Ndiyo. Kwanza, nyinyi wanaume ndivyo mlivyo! Mwanamke akifiriki amepata, kumbe amepatikana na juhudi zake zote za kudumisha upendo zinagonga mwamba. Na kwa mabosi msiseme. Yaani karibu sijalala wiki mbili maana kila siku bosi anafanya sherehe eti amethubutu, anaweza na kusonga mbele. Kwa kweli siwezi kukataa ingawa sijui alithubutu nini zaidi ya kugombea uheshimiwa. Lakini kusonga mbele. Mungu akupe nini wakati unapewa pesa za kusherehekea. Hivyo siku za pekee ninazopumzika kidogo ni pale akialikwa kwenye sherehe za wengine. Lakini hapa nyumbani kazi mtindo mmoja. Nyama choma za tumethubutu, bia za tunaweza na hasa wiski za tunasonga mbele.

Kwa kweli siwezi kukataa. Najua huwezi kulinganisha hata kijiji chetu na kile cha zamani. Nakumbuka baba alivyoeleza kuhamishwa kwao ili wawe karibu na shule, na kituo cha afya na maji na barabara. Walikuwa hawataki mwanzoni lakini baadaye waliona faida yake. Na huenda nisingeenda hata shule ya msingi bila hiyo maana tulikaa porini sana. Kwa hiyo wale wa enzi zile kweli walithubutu. Na kwa mawazo yangu hawakuthubutu kwa ajili yao bali kwa ajili ya nchi kwa ujumla ndiyo maana tukapiga hatua.

Sasa najiuliza uthubutu huo ulipotea wapi? Walithubutu kujenga shule tukafaidi lakini uthubutu wa kuendeleza shule ulipotea wapi? Hata wakati tuko shuleni kule vitabu vilikuwa vimeanza kuadimika na sasa vimepotea kabisa. Labda tunathubutu kuendelea kujenga majengo na kusema ni shule, lakini shule hasa iko wapi? Na kituo chetu cha afya. Wanathubutu kutuambia hakuna dawa hivyo Panadol ni hirizi ya kuponyesha magonjwa yote.

Au uthubutu umegeuka uthubutu binafsi. Nikiangalia kijiji chetu na jinsi kwanza serikali ya kijiji inavyothubutu kuuza ardhi yetu kwa hawa wa nje wanaoitwa wawekezaji, najiuliza wanathubutu kwa ajili yetu au kwa ajili ya nani? Tumeona faida gani wakati tunawaangalia wakiporomosha nyumba zisizofanana na kilimo chao au kipato cha watoto wao. Na sasa hata akina baba wameambukizwa uthubutu huo na kuuza mashamba yao kwa hao hao ili tuwe vibarua ndani ya ardhi yetu yenyewe. Sijui hapa kama wanasonga mbele wao au wale wenye vilabu maana naona vijana wenzetu wanazidi kuja mjini kutafuta chochote maana baba zao wamethubutu kutafuna kila kitu.

Inanikera Frank. Ni sawa na wewe kutamba kwamba biashara yako inaanza kukua wakati sioni mabadiliko yoyote. Ndipo hapo inabidi nijiulize biashara inapanuka kwa faida ya nani? Ya mimi mwenzio au …. Njoo nakuambia tusemezane kabisa.

Na nchi tusemezane pia. Tangu tuanze kuimbiwa uthubutu, nani amejaribu kuhoji msemo wenyewe. Hapa kwa bosi mtu mmojamoja asiye na shukrani kwa zile nyama zilizochomwa na Hidaya anauliza lakini bosi na wenzake wanamshushia maneno ya kushushua hadi anashaa.

Hata juzi mmoja alithubutu kuuliza: ‘Mbona katika sherehe za nchi nyingine tunaona sherehe za mtaa? Yaani watu wa mtaa fulani wanakusanyika na kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa nchi na kadhalika lakini hapa sherehe zinafanyika kwa wanene tu.’

Bosi akasikia. ‘Unasema nini?’ Alivyokunja uso nilidhani yule jamaa atanywea lakini baadaye nilisikia ni mtu asiyeogopa kuchanja mbuga kabisa hata mbele ya vitisho.

‘Usinielewe vibaya mheshimiwa mkuu. Tunashukuru sana kufika kwako na kufaidi miaka hamsini ya nchi yetu hata kama imepokonywa jina lake. Lakini najiuliza wananchi watafaidi vipi zaidi ya kuangalia picha za watu wanaokula kwa niaba yao? Watajisikia kwamba ni siku yao ya kusherehekea pia?’

Basi watu wakaanza kushambulia. ‘We vipi? Mbona unataka kuwalemaza wananchi. Hizi hela zitatoka wapi?’

‘Hela za maonyesho na maadhimisho ya sherehe zote zimetoka wapi? Mbona wakati wa kampeni za uchaguzi, hela za pilau zinapatikana? Kwa nini kusiwe na pilau kitaifa kuadhimisha miaka hamsini hii?’

‘Wacha zako wewe. Unatafuta umaarufu tu.’ ‘Sitafuti umaarufu wala harufu ya umaarufu. Nasema kwamba tufurahie kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru mikono mitupu si njia nzuri. Mwisho watu wataanza kunung’unika badala ya kufurahi.’

‘Si wapike pilao kule kwao tu. Kwa nini wategemee kuletewa tu.’

‘Mbona sisi tunalete …’ Hapo bosi aliingilia kati.

‘We Bwana mdogo kweli fadhila ya punda ni ushuuzi wa kipuuzi. Nimejitahidi, nimehangaika kutafuta wawakilishi waweze kusherehekea uhuru wetu, hadi nimekualika wewe lakini badala ya kushukuru unaponda tu.’

‘Si kweli mheshimiwa. Nimeshukuru sana. Lakini natoa wazo kwamba ni muhimu wananchi wote wafaidike si kuwaangalia wengine wakibugia minofu bila hofu wakati wao wanajiuliza watapata wapi chakula cha siku. Hasa vijana. Kwao uhuru ni historia, ni wa kisimuliwa. Kweli nimefurahia vipindi vinavyoonyesha tulikotoka na nadhani hata vijana wamejifunza mengi. Lakini wao wanauliza … na leo, uthubutu umetupeleka wapi huku tunakaa ndani ya madarasa yasiyo na kitabu wala mwalimu, tunaangalia wengine wanaendelea kwa niaba yetu katika shule za binafsi na hospitali za binafsi, na uwekezaji wa binafsi, na ubinafsi wa binafsi …’

Bosi alikuwa ameanza kubadilika sura hapa na weusi ule wa mkaa ulikuwa dalili ya mlipuko lakini mgeni aliendelea tu kama vile ni mwanasiasa asiyetaka kujua hali halisi.

‘Ndiyo, kijana ataelewaje dhana ya kusonga mbele wakati anazongwa mbali. Hana ajira, hana …’

Hatimaye bosi alilipuka na kwa kuwa alikuwa anatafuna nyama nyingi wakati ule athari za mlipuko zilikuwa mbaya maana vipande vidogovidogo vya nyama vilitoka kwa kasi na kusambaa kila mahali na kuwagonga watu, utadhani Gongo la Mboto.

‘Hebu nyamaza mpumbavu wewe. Daima kukosoa, daima kukosoa. Tumethubutu kweli na tumweza sana katika uthubutu wetu ndiyo maana tunasonga mbele. Huwezi kumaliza maendeleo kwa siku moja na kadiri tunavyopata tunaelekeza kwa wananchi li wasonge mbele nao.’

Mgeni yule alicheka, jambo ambalo lilizidi kumkasirisha bosi.

‘Toka hapa na usaliti wako. Wewe sema tu, sema tu, maneno ya kijinga, sisi tutazidi kusonga mbele na wananchi wetu.’

Mgeni akageuka na kutoka. ‘Sawa mheshimiwa. Tuone nani anasonga nani anazongwa. Uhuru ni kwa ajili yetu sote, si kwa kuonyeshwa tu bali kwa kushiriki.’

Kidogo bosi amtupie glasi yake lakini alijizuia. Na kadiri nyama choma na vinywaji vilivyozidi kuletwa watu wakasahau haraka maneno ya yule jamaa. Lakini mimi bado yaniwasha sana. Mtu hawezi kushangilia kwa kuambiwa tu ni muhimu kushangilia, au kwa kuonyeshwa mambo yanayowahusu watu wengine tu. Ameshiriki vipi? Na amefikia hali ipi ili aweze kushangilia?

Ni sawa na wewe kuniambia kushangilia biashara yako tuliyojenga pamoja huku naambiwa ni wengine wanaofaidi hii biashara si mimi …. Njoo uniambie sivyo!

Hidaya


RAIA MWEMA

No comments: