Monday, December 19, 2011

MWISHO WA KAFULILA ULIVYOKUWA NCCR


ALISULUBIWA NA WAJUMBE 38, ALIANGUA KILIO ZAIDI YA DAKIKA 40, KINA MBATIA KUMUONA RAIS KIKWETE
Fidelis Butahe
DAVID Kafulila mbunge kijana kutoka Jimbo la Kigoma Kusini juzi aliingia kwenye ukumbi wa mkutano akiwa na nguvu na matumaini ya kumsimamisha uongozi mwenyekiti wa chama chake cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, lakini mwisho, upepo ulivuma vibaya kuelekea upande wake na hatimaye akajikuta anasulubiwa na kisha kuvuliwa uanachama.

Kafulila ambaye alitokea Chadema na kujiunga NCCR- Mageuzi mwishoni mwa mwaka juzi na mwaka jana akafanikiwa kuingia bungeni baada ya kumwaga mgombea wa CCM, Kifu Gullamhussein , ni mwanasiasa kijana ambaye alianza kung’ara katika medani za siasa nchini kutokana na kusimamia hoja zenye maslahi ya umma kama Katiba Mpya, kupinga nyongeza ya posho za wabunge na kutaka wale ambao walisababisha hadi Dowans kupata tuzo ya zaidi ya Sh100 kuchukuliwa hatua.

Safari ya kumshughulikia Kafulila ilianzia Desemba 8 mwaka huu baada ya kuvuliwa wadhifa wa Katibu Mwenezi wa chama hicho na juzi, ilihitimishwa katika Ukumbi wa Proin ambako mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ulifanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi karibu saa tano usiku.

Gazeti hili liliwashuhudia wajumbe 64 wa mkutano huo wakifika katika ukumbi huo huku wakionekana kuwa na shauku ya kutaka kujua hatma ya chama hicho baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya Kafulila, Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia na Katibu wake Samwel Ruhuza.

Kuwasili wa Kafulila
Kafulila alifika katika ukumbi huo saa 2:00 asubuhi akiwa kwenye gari yake aina ya Toyota Altezza na moja kwa moja aliingia ndani baada ya mabaunsa zaidi ya 10 waliokuwa katika geti la kuingilia kumruhusu.

Kuanza kwa mkutano
Mkutano huo ulianza rasmi mnamo saa 3:00 huku ukiongozwa na Dk Sengondo Mvungi, akisaidiwa na Ruhuza na Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Haji Ambari Khamis.

Katika mkutano huo, Mbatia alikuwa mmoja wa watuhumiwa ambao alipaswa kujibu tuhuma zake za kukifanya chama kama CCM B huku Kafulila akituhumiwa kuvujisha siri za chama nje ya utaratibu wa vikao. Moja ya tuhuma za Kafulila ni kueleza vyombo vya habari kwamba ameondolewa katika nafasi ya uenezi.

Baadhi ya wajumbe wadaiwa si halali
Lakini, hali ya mambo katika chumba cha mikutano ilianza kuvurugika ilipofika saa 8:00 mchana wakati wa kupigakura ya za kutokuwa na imani na Mbatia baadhi ya wajumbe walitoka nje ya ukumbi kwa maelezo kuwa baadhi ya wapiga kura hawakuwa wajumbe halali wa mkutano huo.

Habari hizo zilieleza kwamba, waliotoka nje walikuwa saba huku wakiongozwa na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Hashim Rungwe.

Kwa mujibu wavyanzo hivyo, baada ya hali kuwa shwari wajumbe hao walipokea na kujadili utetezi wa Mbatia. Tuhuma dhidi ya Mbatia zilitolewa na Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Mbwana Hassan pamoja na wengine 26 waliosaini hati ya kutokuwa na imani naye kwa madai kuwa ni CCM B.

‘’Katika kupiga kura haki haikutendeka, wajumbe tulipiga kura kwa kunyoosha mikono na sio kura ya siri, pamoja na hayo Mbatia alionekana kuwa safi’’ alieleza mmoja wa wajumbe wa NEC wa chama hicho.

Hata hivyo, akizijibu shutuma hizo mbele ya waandishi wa habari jana, Ruhuza alisema kuwa mkutano huo ulitoa maazimio kwamba Mbatia yuko safi, hodari na shujaa wa chama.

‘’Wajumbe wote waliotoa malalamiko walijiondoa na Mbatia akawa safi hiyo ikiwa ni pamoja na hao waliokuwa wakimpinga awali,’’ alisema Ruhuza.

Hoja ya kumjadili Kafulila
Baada ya kumalizika hoja ya Mbatia na kufanikiwa kuzima kile alichokuwa akikiita uasi dhidi yake, jioni ndipo ilipokuja hoja ya Kafulila.

Zamu hiyo ya Kafulila ilipokuja upepo ulionekana kubadlika ghafla ndipo alipopewa nafasi ya kujitetea kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Alivyojitetea
Habari hizo zilieleza kuwa Kafulila alipopewa nafasi ya kujieleza, alisema kama kweli kuna mvutano baina yake na Mbatia kinachotakiwa ni kukutana na kuzungumza chini ya usimamizi wa wazee wenye busara wa chama hicho.
Habari hizo zilelieza zaidi kuwa Dk Mvungi wakati akitoa maelezo yake alisema kuwa wajumbe wanatakiwa kutumia busara katika uamuzi yao.

Hata hivyo, hali iliharibika zaidi kwani licha ya utetezi huo wa Kafulila, wanachama ndani ya ukumbi huo baada ya kuanza kupiga kura za kuwafuta uanachama makada wa chama hicho akiwemo Kafulila.

Habari zilieleza kuwa baada ya kuthibitisha upepo unavuma vibaya kwake na hakuna njia ya kutokea, Kafulila alikwenda kumwomba msamaha Mbatia huku akiwa amepiga magoti jambo ambalo liliwakera wajumbe ambao walimwita msaliti.

Lakini, wajumbe walipiga kelele, ‘’Anaigiza huyo muda wote alikuwa wapi? Hata kujitetea kashindwa na amekuwa akijibu majibu ya mkato sasa ndio anakumbuka kuomba msahama, muongo huyo’’.

Kafulila alia kwa uchungu
Kilio cha kwikwi kilimtoka Kafulila kuanzia saa 4:48, usiku baada ya mkutano huo kumvua uanachama Kafulila. Mwananchi lilifanikiwa kujipenyeza hadi ndani ya geti la ukumbi na kumkuta Kafulila akilia kwa sauti huku akiwa amepiga magoti na kumshika mmoja wa wajumbe miguuni.

‘’Nisameheni jamani..., naomba mnisamehe jamani nimekosa nitakwenda wapi?,’’ alisikika akilia.

Mbunge huyo alionekana kushindwa kujizuia na kuangua kilio kilicholeta huzuni kwa baadhi ya wajumbe wa mkutano huo ambao baadhi yao walionekana kumwonea huruma

Kutokana na hali hiyo, Mbatia alijaribu kumwombea msamaha kwa wajumbe, lakini walishikilia msimamo wao kwa maelezo kwamba kama Kafulila akisamehewa, wao watarudisha kadi za chama.

Katika wakati fulani Kafulila aliyekuwa amevaa suti nyeusi alikuwa alisimama nje ya mlango wa kuingilia katika ukumbi huo huku akiwa amekunja mikono yake, mfano wa mtu anayemwomba Mwenyezi Mungu
Wajumbe waliokuwa wakitoka katika ukumbi huo walionekana kutomjali na walimpita na kuingia katika magari yao na kuondoka jambo, lililozidi kumwongezea uchungu na kuonekana akizidi kulia mpaka alipokuja kutolewa eneo hilo na Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi wa chama hicho, Faustine Sungura.

Walimtoa eneo hilo na kumpeleka katika gari lake na kuondoka eneo hilo wakati huo ilikuwa saa 5:37 usiku.
Wafuasi wa Kafulila washikwa huzuni

Hayo yakiendelea ndani nje kulikuwa na baadhi ya makada wa chama hicho waliokuwa kundi moja na Kafulila ambao walionekana kuwa na huzuni kubwa baada ya kupata habari hizo.

‘’Wamemfukuza..., wameshakiua chama ndio maana mimi nakuelezeni kila siku hiki sio chama, hakina demokrasia ya kweli, ni bora kwenda CCM tu kuliko hiki chama,’’ alisikika akisema mmoja wa makada hao.

Polisi na mamluki
Awali, wakati zikipigwa kura za kutokuwa na imani na Mbatia ulizuka mtafaruku baada ya wajumbe kushangazwa na kitendo cha kuwepo kwa wajumbe zaidi ya 60 wakati mkutano huo huwa na wajumbe wasiozidi 40.

Baadhi ya wajumbe waliibua hoja ya kutaka baadhi ya watu ambao hawafahamiki kujieleza na taratibu zitumike kuwatambua au kutowatambua.

Kutokana na hali hiyo kuibua mgogoro katika kikao hicho Rungwe pamoja na baadhi ya wajumbe walitoka nje ya mkutano huo, wakionyesha kutoridhishwa na maamuzi yaliyotolewa katika upigaji wa kura.

Habari hizo zilieleza kuwa Rungwe pia alijieleza sababu za yeye kuiandikia barua ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuiarifu kuwa kikao hicho hakikuwa halali

Awali, wakati mkutano ukiendelea habari za ndani kutoka katika mkutano huo zilieleza kuwa wakati ajenda mbalimbali zikijadiliwa Kafulila aliwasiliana na polisi na kuwaeleza kuwa katika mkutano huo kulikuwa na vurugu.

Mwananchi lilishuhudia polisi tisa wakiwa katika gari aina ya Landcruser wakifika katika Ukumbi huo saa 6:05 mchana na kuingia ndani ya ukumbi, ambao walielezwa hakukuwa na vurugu yoyote na wakatoka nje na kuondoka.

Ilipofika saa 6:45 polisi hao walirudi tena na kueleza kwamba, walipigiwa simu nyingine kwamba katika mkutano huo hali si shwari na safari hii walimhoji dereva wa Kafulila, Denis Kalikisha.

Wakati huo huo, chama hicho kimeomba kukutana na Rais Jakaya Kikwete kwa nia ya kutoa mawazo yake kuhusu mchakato wa kutungwa kwa Katibu Mpya ya Tanzania, kama ilivyoahidiwa kwa wananchi na mkuu huyo wa nchi.
Kafulila aliwahi kupinga kukutana na Rais Ikulu kwa madai suala zima la mchakato wa Katiba Mpya umekiukwa.

Lakini, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana ilisema Rais sasa amekubali ombi hilo la NCCR-Mageuzi.

Mbali ya NCCR, Rais pia amekubali kukutana na Baraza la Taifa la Taasisi Zisizokuwa za Kiserikali (NGO’s), ambalo limeomba kukutana na kuzungumza naye.MWANANCHI

2 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mtu unapokuwa huna utashi, ajenda na msimamo basi unageuka mshibisha tumbo tu, mbinafsi, mbishi na LOSER.

Wanasiasa hawa malaya wanaohangaika na kuhamahama kutoka chama kimoja kwenda kingine daima wana matatizo.

Inawezekana Kafulila wa watu Kafulia kweli....
=================>
Mwalimu:

Nilikuwa napita hapa kusema kwamba sasa nimerudi tena rasmi. Tupo pamoja !!!

http://matondo.blogspot.com/2011/12/wanablogu-wenzangu-na-wapenzi-wote-wa.html

Baraka Mfunguo said...

Pamoja kamanda