Tuesday, December 27, 2011

MWAKA WA MAJONZI YA VIFO VYA WASOMI -UDSM


Na Fredy Azzah


PAMOJA na kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 2011 unaaga huku ukiacha majonzi makubwa kwa wanajumuiya wa chuo hicho waliondokewa na wasomi wenzao mbalimbali.

Makala haya yanarejea taarifa kuhusu baadhi ya wasomi hao walioacha pengo kubwa siyo kwa jumuiya hiyo, lakini hata kwa jamii ya Watanzania kwa jumla.


Februari 21
Aliyekuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam upande wa Shule Kuu ya Elimu, Dk Alphonce Ndibalema alifariki dunia jijini Dar es Salaam baada ya kupatwa na shinikizo la damu.
Dk Ndibalema atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kuwapa maarifa Watanzania kuhusu sekta ya elimu aliyokuwa akiyatoa kupitia magazeti mbalimbali nchini.
Hakua mchoyo wa kuwafikishia wengine kile alichokijua. Hakutosheka na kufundisha darasani, kutoa mihadhara au kuandika katika majarida ya kitaaluma. Aliona iko haja ya kugawa utajiri wa maarifa na mawazo yake kwa Watanzania wengi zaidi kupitia vyombo vya habari.
Dk Ndibalema aliyejiunga na chuo hicho mwaka 1991, alikuwa msomi farisi wa taaluma ya elimu hususan nyanja za Menejimenti ya Elimu, Mipango na Sera. Kwa muda wote wa usomi wake, alijipambanua kama mwanazuoni mahiri na makini aliyetoa mchango maridhawa katika nyuga hizo za elimu.
“Alifanya tafiti katika masuala mengi yaliyohusu maendeleo na mipango katika elimu, alitoa makala nyingi katika majarida ya kitaaluma, alishiriki kuandika sura za vitabu, mada za makongamano na ripoti kadhaa za kitafiti,’’ ilisema taarifa ya tanzia iliyotolewa na Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya chuo hicho.
Dk Ndibalema alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1991 akiwa mhadhiri msaidizi katika Kitivo cha Elimu kabla ya kupanda daraja na kuwa mhadhiri mwandamizi mwaka 2025.Kuanzia mwaka 2005 hadi anafariki, alikuwa Mkuu wa idara ya Misingi ya Elimu, Menejimenti na Masomo Endelevu.
Marehemu alizaliwa mwaka 1952. Alisoma shule za msingi Kazi na Kanazi zilizopo mkoani Kagera kuanzia mwaka 1960 hadi 1966 kabla ya kujiunga na shule za sekondari za Ihungo na Mirambo na kuhitimu mwaka 1972.
Mwaka 1975 hadi 1976 alikuwa mwanafunzi katika kilichokuwa chuo cha ualimu Chang’ombe na baadaye kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya kwanza katika elimu na kuhitimu mwaka 1982.
Masomo ya shahada za juu za Uzamili na Uzamifu aliyapata kutoka vyuo vikuu vya Massey cha New Zealand na Toronto cha nchini Canada

Machi 31
Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ikapata tena pigo baada ya mhadhiri wake Dk Justine Katunzi kufariki dunia baada ya kuanguka akiwa anafundisha darasani.

Taarifa iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, ilisema baada ya kuanguka alipelekwa katika zahanati ya chuo hicho ambako alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa.

Dk. Katunzi alikuwa akifundisha katika Shule ya Biashara ya chuo hicho, na alijiunga na chuo hicho mwaka 1976 akiwa mkufunzi msaidizi na baadaye mwaka 1978 alipandishwa cheo na kuwa mhadhiri msaidizi.

Alipanda ngazi na mwaka 1980 alikuwa mhadhiri, na mwaka 1998 alipanda daraja kuwa mhadhiri mwandamizi hadi alipostaafu kwa mujibu wa sheria mwaka 2010. Alikuwa akiendelea na kazi chuoni hapo kwa mkataba.

Kitaaluma alikuwa amebobea katika fani ya menejimenti, akiwa mmoja wa waasisi wa Kitivo cha Biashara na Menejimenti (sasa Shule ya Biashara).

Katika kipindi chote cha utumishi wake alitoa mchango mkubwa katika uandishi wa majarida, utafiti na machapisho mbalimbali ya kitaaluma. Aidha, kati ya mwaka 1990 na 1995 alikuwa mbunge wa Geita.

Julai 23
Kwa mara nyingine jumuiya ya chuo hicho na jamii ya Watanzania kwa jumla ikapatwa na huzuni kubwa baada ya kutangazwa kwa kifo cha msomi nguli wa masuala ya siasa na utawala, Profesa Samuel Mushi.

Profesa Mushi alikuwa mwalimu wa walimu, akigubikwa na sifa kuu ya kuwa mshauri na mwelekezi kwa wanataaluma wenzake na wanafunzi.
Karibu asilimia 95 ya wahadhiri wa idara ya siasa na utawala walipitia katika mikono yake kwa nyakati tofauti wakiwamo wasomi maarufu katika fani ya siasa nchini.
Akitoa wasifu wa marehemu, Profesa Gasper Munishi alisema, Profesa Mushi alikuwa mwanafunzi bora aliyepikwa na kupikika katika vyuo vinavyoheshimika kwa wanataaluma kama Chuo Kikuu cha Yale kilichopo Marekani alichosomea shahada yake ya Udaktari wa Falsafa (PhD).
“ Umahiri wa Profesa Mushi ulitokana na kujituma kwake katika kufanya kazi za kitaaluma zilizozaa matunda ambayo sio tu yalikidhi vigezo vya juu vya kuendelea kuitumikia taaluma, bali yaliweka ziada iliyopanua taaluma yake,” alieleza na kuongeza:
“Profesa Mushi alitengeneza viwango vyake mwenyewe vya umahiri wa juu katika taaluma na mpaka sasa wenzake wengi wanaviona viwango hivyo kuwa ndivyo vya juu kabisa vinavyoweza kufikiwa.’’
Kumbukumbu zinaonyesha marehemu alisoma shahada ya kwanza, shahada ya Uzamili na shahada ya Uzamifu katika vyuo vikuu vya Makerere, California Berkeley na Yale.
Kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1967 wakati huo kikiwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Profesa Mushi alifanya kazi za utawala serikalini kwa kushika nyadhifa kadhaa kama vile mkuzaji wa Kiswahili na Fasihi na Kaimu Kamishna wa Utamaduni katika iliyokuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii.
Kimataifa aliwahi kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa kitengo cha Siasa, Historia na Utamaduni cha taasisi ya Umoja wa Mataifa nchini Namibia na Katibu Mkuu wa Chama cha Wasomi wa Siasa Afrika (AAPS).
Akiwa chuoni alianza kufanya kazi ya utawala katika kitivo cha sheria kabla ya kubadilishwa kazi na kuwa mtafiti msaidizi na kisha mhadhiri msaidizi katika Idara ya Sayansi ya Siasa mwaka 1970 .
Kwa kipindi kisichozidi miaka 10, alipanda ngazi mbalimbali za kitaaluma hadi kufikia daraja la uprofesa aliotunukiwa mwaka 1980.
Pamoja na kustaafu utumishi wa umma mwaka 1999, aliendelea kufanya kazi kwa mkataba hadi mauti yalipomfika

Vifo zaidi vya wahadhiri

Wasomi wengine walioaga dunia mwaka huu katika chuo hicho ni pamoja na Dk Tumaini Kimario, aliyekuwa mhahiri katika kitengo cha uhandisi wa vyanzo vya maji aliyefariki Januari 22.

Pia mwanasayansi nguli katika chuo hicho, Profesa Chrysanth Kamuzora alifariki dunia februari 15 mwaka huu. Juni 22 chuo hicho kilimpoteza tena msomi mkongwe katika fani ya wanyama na utunzaji wa mazingira, Profesa Alfreo Nikundiwe.

Julai 29, mtaalam wa mazingira kutoka koleji ya sayansi asilia, Dk Kristoko Msindai alifariki dunia na baadaye Oktoba 18, Profesa Michael Kishimba aliyekuwa mtaalamu wa Kemia katika koleji hiyo naye akafariki.

Wanafunzi sita wafariki katika ajali
Novemba 19 ilikuwa majonzi tena kwa chuo hicho baada ya wanafunzi sita wa shahada ya uzamili kufariki dunia katika ajali ya basi walipokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Kigali Rwanda kwa ziara ya kimasomo katika Taasisi ya Sayansi na teknolojia ya nchini humo.

Wanafunzi hao waliofariki walikuwa wakisoma shahada ya uzamili ya hesabu kupitia programu maalum ya Hisabati ya Afrika Mashariki (EAUMP)MWANANCHI

No comments: