Thursday, December 29, 2011

MKATE WA USHOGA NDIO HUO UNAPAKWA "BLUE BAND" WAAFRIKA TWAWEZA KUUEPUKA?Kutoka kwa Profesa Matondo,

Inaonekana mabwana wakubwa hawa hawajaridhika na utumwa wa kiuchumi, kifikra, kisaikolojia na kitamaduni waliouanzisha wakati wa biashara ya utumwa, kuupalilia wakati wa ukoloni na kuuendeleza kupitia ukoloni mamboleo hadi leo.

Hawajaridhika:

Pamoja na ukweli kwamba bado tunaendesha mifumo yetu ya elimu kwa kutumia lugha zao – lugha ambazo wala hatuzielewi vizuri; na hivyo kufanya elimu tuwapayo vijana wetu kuwa kichekesho.
Pamoja na ukweli kwamba tungali tunadhani kuwa kila kitu cha
o ni bora kuliko cha kwetu.

Pamoja na ukweli kwamba tungali tunaiga kila kitu wanachofanya: wakitembea uchi nasi tunaiga, wakilegeza suruali zao nasi tunalegeza, wakitoboa masikio na kusuka nyweli nasi tunafanya vivyo hivyo.


Pamoja na ukweli kwamba tumezungukwa na utandawazi wao kila kona.

Sasa wanatulazimisha kuhalalisha ushoga – jambo ambalo naamini katika makabila mengi ya Kiafrika (lilikuwa) linafanyika kwa siri ingawa sasa, kutokana na utandawazi tumeanza kuona “maanti” wakijitokeza waziwazi.
“Blue Band” hii inayopakwa kwenye huu mkate wa ushoga ni nini?

Ni Donge nono la misaada ambalo, kama makinda ya ndege yasiyojiweza, tumezoea kumegewa pamoja na ukweli kwamba Mungu Ametujalia kila kitu; na sehemu kubwa ya donge hili huishia katika midomo mipana ya wachache.


Serikali ya Uingereza imeweka wazi kwamba haitatoa misaada yake kwa nchi ambazo hazikubaliani na ushoga. Serikali ya Marekani pia imetoa masharti kama hayo. Kutokana na mikwara hii, serikali ya Malawi ilibidi kulegeza kamba kuhusu msimamo wake kwa sababu asilimia kubwa ya bajeti yake inategemea misaada kutoka Uingereza na Marekani.

Hata Uganda imeonyesha dalili za kutetereka katika msimamo wake kuhusu suala hili.
Ni nchi chache za Afrika zinazoweza kujiendesha bila “Blue Band” hii ya wakubwa na tusije kushangaa huko mbele tukisikia washika kurunzi wetu wameshatia sahihi mikataba ya kuukubali ushoga – hata kama majukwaani wanajipiga kifua na kulaani.
Msimamo wa sasa wa Tanzania kuhusu suala hili ni wa kutia moyo sana. Natumaini kwamba hautabadilika; na hata ukibadilika basi usiwe ni kutokana na kulazimishwa na hawa wakubwa.
Bila kujali maoni na msimamo wangu kuhusu ushoga, kinachonikera mimi ni kulazimishwa kukubaliana na matakwa ya hawa wakubwa wetu.

Utumwa haukutosha? Ukoloni haukutosha? Ukoloni mamboleo je? Pamoja na yote haya, mpaka tukubali ushoga kweli ndo tupate misaada? Ni lini tutaweza kusimama tisti na kuendesha mambo yetu bila kutegemea mikate hii iliyopakwa "Blue Band"
yenye sumu ???


MATONDO BLOG

No comments: